Na Sufiani Mbaga
KUFUATIA kauli zinazoendelea kutolewa na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi kuwa baadhi ya vyama vya upinzani vimekuwa vikiendesha kampeni ndani ya Misikiti katika chaguzi ndogo za Ubungo na Temeke, Chama hicho kimetakiwa kusitisha hali hiyo mara moja.
Wito huo umetolewa na mwananchi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Revocatus Bagandesho, mkazi wa Ubungo Kibangu na mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi katika eneo la Manzese Jijini.
Bwana Bagandesho alitoa wito huo katika ofisi zetu zilizoko mtaa wa Mahiwa, Kariakoo Jijini mnamo siku ya Jumatano, saa nane adhuhuri katikati ya juma hili.
Bwana Bagandesho alisema kuwa ameamua kuzitembelea ofisi za gazeti hili kutoa dukuduku lake kwa kile alichokiita kuchoshwa na matamshi ya uongozi ya viongozi hao na kufumbiwa macho na vyombo vingine vya habari.
"Unajua kwa mkazi wa Ubungo na mfanyabiashara kama mimi inakera kweli kweli unaposikia kauli kama hizi zikirudiwa rudiwa wakati hali halisi inajulikana kwa kuwa tunalala nayo, tunaamka nayo na tunashinda nayo. Vyama vinavyoambiwa vinaendesha kampeni Misikitini ndivyo vinavyojaza watu kwenye viwanja vya kampeni, ndivyo vinavyozungumzwa kwenye mikusanyiko mbalimbali ya watu, na ndivyo hivyo vinavyosababisha kufungwa kwa barabara kila siku jioni katika eneo la Manzese kutokana na shamra shamra za wananchi. Kweli inaingia akilini kuwa vyama hivi vinahitaji kura za Misikitini?, alihoji Bwana Bagandesho kwa uchungu.
Bwana Bagandesho pia alivilaumu vyombo vya habari hususan magazeti kwa kile alichokiita kuwa ni kushirikiana na CCM kuwadanganya wananchi.
"Vyombo vya habari hususan magazeti vyote vinaelewa ukweli wa mambo kwa sababu ukweli huo uko hadharani. Badala ya magazeti kuandika ukweli, ndio kwanza yanakuza uongo", alisema.
Baada ya kuulizwa na mwandishi wa habari hizi ni kitu gani ambacho anadhani kinasababisha hali hiyo, Bwana Bagandesho alijibu bila kusita kuwa ni sababu za udini.
Alifafanua kuwa baada ya CCM kuwanyanyasa Waislamu kwa muda mrefu na sasa Waislamu wamezinduka tegemeo lao limeegemea kwenye kura za Wakristo.
"Wanatumia 'triki' kuwaghilibu Wakristo kuwa kura za wapinzani zimeegemea kwa Waislamu, hivyo Wakristo waelekeze kura zao kwenye kukinga mkono. Hata hivyo nadhani Wakristo wenzangu wataishtukia hii 'gemu'", alisema.
Alimalizia kwa kuitaka CCM
kuacha kucheza na udini na badala yake ijiunde upya katika misingi ya kutoa
haki sawa kwa kila mwananchi na kuacha ubabaishaji katika kujenga hali
bora katika maisha ya wananchi.
--
|
|