MAKALA YA UCHAMBUZI
 
Tutawapata wapi wagombea wasio na dini

Na A.S. Chachika

WATANZANIA tumefundishwa, tumekaririshwa, tumefanyiwa mrajaa juu ya kuwa Tanzania haina dini lakini Watanzania wana dini zao. Tukaelewa na baadhi yetu tukatamka 'naam! Tumekubali, tumesadiki Tanzania haina dini lakini sisi tuna dini zetu". Somo hilo limeeleweka vizuri ila kilichopungua ni kule kutofahamishwa maana halisi ya neno dini.

Wataalam wa lugha na wa masuala ya Theolojia wanatufahamisha kuwa, ukitaka kulipa neno Dini maana yake halisi itakulazimu kusema, "Dini ninjia au mfumo wa maisha". Na kwa tafsiri hiyo basi, Uislamu, Ukristo, Unasara, Uyahudi, Uhinduu, Ujamaa, Ubepari na kadha wa kadha, yoote hiyo ni mifumo ya maisha au kwa kifupi zote hizo ni dini. NI mfumo upi ulio sahihi lisitushughulishe kwa leo.

Sasa tunapouliza swali: "Tuwapate wapi wagombea wasio na dini?" Tunawaomba wasomaji wetu wasihangaishe akili zao kwa maana swali hili tumelielekeza kwa viongozi na wazee wa CCM. Aidha, kilichotusukuma kuuliza hivyo ni kutokana na vyombo vya habari kadhaa kumnuku mzee wa CCM Alhaj Ali Hassan Mwinyi wakati akimtambulisha mgombea wa CCM katika uchaguzi mdogo huko Ubungo akitamka kwamba baadhi ya vyama vimewasimamisha wagombea wao kwa misingi ya dini.

Kauli hiyo ambayo kimsingi ni kauli ya CCM imetusukuma kuuliza swali hilo kwani inavyoonekana wagombea wote pale Ubungo wana dini zao. Na tukitumia kigezo cha majina kuwa kitambulisho cha udini wa mtu, tunaamini kuwa wako Wakristo wawili na Waislamu wawili. Labda tungefahamishwa kuwa ni chama kipi kilitakiwa kiwe na mgombea wa dini ipi?

Inawezekana kabisa tusiwajue watu dini zao, lakini kwa kutumia utamaduni wa majina kama vigezo, tunaweza kufikia uamuzi huu: Mgombea wa NCCR Bwana Abdulrazaq ni Muislamu, mgombea wa CCM Bwana Venance ni Mkristo, mgombea wa CUF (Chama cha Wananchi) Bwana Hussein ni Muislamu na mgombea wa CHADEMA Bibi Justin ni Mkristo. Ugomvi uko wapi?

Lakini kwa mgombea wa CCM kuwekwa katika hali ya kutokuwa mdini au labda mzee Mwinyi kafahamishwa kuwa huyo hana dini kuna maana ya undani zaidi. Tunataka kumfahamisha mzee wa CCM kuwa mgombea aliyekuwa akimtambulisha, Bwana Venance Ngula ni Mkristo wa Kanisa teule. Bwana Ngula ni Mkatoliki, Kanisa ambalo lina vibali na baraka zote za kutamba nchini hapa. Kwa mantiki hiyo CCM inampomteua mgombea wake ambaye ana dini yake, na papo hapo mzee wa CCM akatuambia kuwa vyama vingine vimesimamisha wagombea kwa misingi ya dini, haitushangazi bali inatukumbusha tu zile ahadi kuu tatu ambazo zimetolewa na wakubwa watatu.

Chama Cha Mapinduzi kina mafungamano mazuri na ya karibu na Kanisa la Kikatoliki. Tunamkumbuka sana Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alivyowaahidi viongozi wa Kanisa lake kwa kuwaambia, "Waambieni wakuu wa Kanisa kuwa nitalipa Kanisa fursa nzuri". Utekelezaji wa hili ulianzia tangu wakati wa kudai uhuru na unaendelea hadi leo.

Hatujasahau maneno (ahadi) mazito yaliyosemwa na Papa Paulo juu ya Tanzania wakati wa ziara yake hapa nchini. Siku Papa alipokuwa anaaga pale uwanja wa ndege aliwaambia viongozi w serikali, wakuu wa dini, wazee na wananchi wote maneno haya: "Naikabidhi Tanzania chini ya ulinzi wa Bikira Maria". Ni hivi karibuni tu Mheshimiwa Rais Mkapa alipokuwa akimpongeza Muhashamu Kadinali Pengo kwa kuteuliwa kuwa Kadinali alipomwambia: "Tutasaidiana kuongoza nchi". Na kwa misingi hiyo hiyo, aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa mwisho katika sreikali ya awamu ya pili, alimwandikia barua aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania mnamo Januari 28, 1995 na kumwambia: "Natumaini utaendelea kunisaidia kwa sala, ushauri na maoni mbalimbali.... naendelea kutumaini kwamba ushirikiano mzuri kati ya serikali yetu na Kanisa Katoliki utaendelea kwa manufa ya wananchi wetu".

Tunatumai sasa wasomaji wetu mnaweza mkaona ni kwa mantiki gani CCM inapomsimamisha mwanachama wake Mkatoliki iwe si udini lakini NCCR ikimsimamisha Abdul iwe kawekwa kwa misingi ya dini. Hii ni ahadi ambayo CCM tangu enzi za TANU ilitoa kwa Kanisa kupitia Baba wa Taifa kupewa fursa nzuri. Na Papa kuikabidhi Tanzania katika ulinzi wa Bikira Maria. Hiyo ndiyo hali iliyompelekea mzee Mwinyi kumtambulisha mgombea wa CCM akiwa na dini yake na kujasirika kuwaambia wengine kuwa wagombea wao ni kwa misingi ya udini. Swali letu bado halijapatiwa jibu. Tuwapate wapi wagombea uchaguzi wasio na dini?
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook