APRILI 26-30, 1999 ulifanyika mkutano wa Kimataifa nchini Uingereza uliopewa anuwani Uingereza na Uislamu. Kutoka Tanzania walihudhuria Mabwana Issa Mnenge na Ismail Abdullah. Fuatana na Bwana ISMAIL ABDULLAH katika makala hii uelewe lengo na yatokanayo na mkutano huo.
NILIPATA mwaliko mimi na mwenzangu Sheikh Issa Mnenge kuhudhuria mkutano wa kimataifa nchini Uingereza uliozungumzia "Mutuality Britain and Islamic World". Pia ilikuwa ni wakati huo huo Msikiti Mkuu wa London ulikuwa unatimiza miaka sitini tokea serikali ya Uingereza ilipowapa Waislamu wa Uingereza, kibali kujenga Msikiti na pia ulikuwa ni umri huo huo wa miaka sitini tokea kuundwa kwa "British Council" kitengo cha Uingereza kinachoshughulikia kukuza utamaduni, sayansi, teknolojia, elimu kwa nchi za nje ya Uingereza kwa ushirikiano wa pande zote mbili, na ndani ya Uingereza, na ndio walotugharamia safari yetu mimi na Sheikh Mnenge.
Ni nini Dunia ya Kiislamu
Pengine ndugu msomaji angeuliza ni zipi au ni ipi maana ya Dunia ya Kiislamu kama ilivyokuwa imekusudiwa na mkutano huu.
Dunia ya Kiislamu inaundwa na Waislamu waliotapakaa dunia nzima kama "minorities" vikundi vya wachache na idadi yao inakisiwa kuwa ni robo ya idadi ya watu wote duniani, pamoja na wingi wao "concetration" kila nchi 54 zinazounda benki ya Uislamu ya dunia. Dunia ya Kiislamu ina utajiri wa mali ipatayo Dola 1.5 trilioni.
Hii ndio dunia ya Kiislamu, ambayo Uingereza ilifanya mkutano nazo, kuzungumzia ushirikiano. Mataifa yaliyodhuhuria ni kama 36.
Ni msukumo gani ulipelekea Uingereza kuandaa huu mkutano
Swali lingine ambalo msomaji angejiuliza ni kwanini Uingereza iliingia katika gharama kubwa kuandaa huu mkutano na ni kutokana na msukumo wa aina gani?
Kujibu swali hili, ni lazima kutambua ushirikiano mkubwa wa siku nyingi wa kibiashara kati ya Uingereza na nchi za Dunia ya Kiislamu.
Uhusiano huu wa mshikamano wa kibiashara ni wa kihistoria kuanzia karne ya 15 na 16, zama zile za Bara Hindi na Arabuni, zilipoitumia Uingereza kama soko lao kuu la viungo (spices) na hariri n.k.
Katika karne ya 18 na kuendelea Uingereza iliimarisha katika nguvu za usafiri baharini na ukuaji wa viwanda "Industrialization". Na nchi hizi za Kiislamu nazo zikabadilika na kuchukua nafasi muhimu za kuzalisha mali ghafi kama pamba na kadhalika kwa ajili ya viwanda vya Uingereza, na hapo hapo nchi hizo hizo za Kiislamu, kuwa miongoni mwa wanunuzi wakuu wa mali kutoka viwandani (manufactured goods).
Katika miaka ya 70 baadhi ya nchi za Kiislamu ziligundua mafuta yaliyosababisha mambo matatu muhimu:
1. Uchumi wa nchi hizi husika ulianza kukua na kukomaa kwa ukubwa huo.
2. Makampuni ya Uingereza yakapata nafasi ya ukandarasi, ujenzi wa mabarabara nyumba, visima vya mafuta na kadhalika.
3. Ziada ya fedha za nchi hizi zikawekwa katika mabenki yenye usalama zaidi nako ni Uingereza.
Mshikamano wa hawa wawili ukakomaa na kuimarika, hasa kwa vile Uingereza ilikuwa tayari ina mabenki yake nchini Arabuni kama vile "British Bank to the Middle East". Hata mwishoni mwa mwaka 1980 nchi za Arabuni zilikuwa na mabenki 36 na vyombo vya fedha (Financial Institutions) 29 nchini Uingereza, na ukijumuisha na zile za nchi zingine za Kiislamu kama vile Indonesia, Malasia na kadhalika zinadidi mia.
Pia ni mazoea ya kihistoria kuwa akiba ya dhahabu "Gold Reserve" ya nchi hizi za Kiislamu huwekwa kwenye mabenki ya Uingereza.
Pia ripoti ya baadhi ya mabenki binafsi nchini Uingereza, ni kuwa kuna Waislamu 200,000 watu binafsi, wenye akiba 'Liquid Asset' kwenye mabenki ya Uingereza yenye thamani ya $ 8000 bilioni.
Uingereza ni mshiriki na ni mwenye kufaidika vikubwa, kutokana na biashara (Trade Flow) na uwekezaji (Investment Flow), unaofanywa na nchi za Kiislamu nchini Uingereza. Kwa mfano:
1. Ubia wa 20% kwenye Kampuni ya BP unaofanywa na wawekezaji wa Kuwait.
2. Ununuzi wa Dorchester Hotel ulifanywa na wawekezaji kutoka Brunei.
3. Ununuzi wa Lngham Hilton uliofanywa na wawekezaji wa Abu Dhabi.
4 Viwanda vya kuunda magari kama vile Lotus Car Manufactures, Malaysia Car Company na kadhalika zote zikiwa ni za wawekezaji kutoka nchi za Kiislamu.
Nadhani mpaka hapa msomaji, utakuwa umepata sura, ya nguvu ya uchumi iliyonayo nchi za Dunia ya Kiislamu, na sehemu muhimu ya uchumi wa nchi hizo ndani ya uchumi wa Uingereza.
Uingereza inatambua hilo na haiko tayari, mbele ya washindani wake, kumpoteza mteja wake mkuu wa mabenki yake, na mwekezaji mkuu wa viwanda vyake, au muwekezaji mkuu wa nyumba za makazi (Real Estate), ambapo mpaka mwishoni mwa mwaka 1998 na mwanzoni mwaka 1999 nchi za Kiislamu, zilikuwa zimewekeza asilimia 20 (20%) kwenye makazi.
Muingereza anaitambua uzuri dhana ya: Mteja ni Mfalme na ndio akapanga kukaa na mshiriki wake kuzungumzia jinsi ya kuimarisha uhusiano. Tutarudia tena swali hili muhimu huko mwishoni pia.
Mambo yaliyozungumzwa:
Mambo yaliyozungumzwa katika mazungumzo hayo ni ya nyanja mbalimbali kama vile:
Vyombo vya habari: Malalamiko yalielekezwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari, hususan tabia ya kuwazulia mambo Waislamu na kuwahusisha na ugaidi na magaidi, ili jamii iwaone Waislamu na Uislamu kama tishio, na kwa hiyo, wasikubalike ndani ya jamii.
Mfano mzuri ulitolewa ni wa gazeti moja la mjini London la tarehe 24 Septemba 1998, lenye kichwa cha habari "Moslems plot bomb London". Tafsiri ni yangu "Waislamu wakusudia kuulipua mabomu mji wa London".
Katika kutoa mfano huu mkutano ulijulishwa kuwa Baraza la Waislamu Uingereza (Muslim Council of Britain) ulimpelekea Mhariri wa Gazeti hilo malalamiko ya Waislamu na jinsi walivyokerwa na jambo hilo. Na kesho yake Mhariri aliomba radhi kama ifuatavyo:
"There is a danger that whole communities, sometimes whole races, are deemed at worst guilty, at best specious because of the (elleged) actions of a few their members. It is wrong to suggest that all Muslims are extremists... In our headline yesterday on the arrest of several men in London by Anti Terrorist Police it was not our intention to cause offence to the Muslim Community. We're Sorry". (From the Newletter of the Muslim Council of Britain Volume I I issue I of March 1999).
Tafsiri yangu:
"Kuna hatari kuwa jamii yote, wakati mwingine wanachukuliwa kuwa wavunjaji sheria au baya zaidi kutuhumiwa kwa sababu tu ya tuhuma dhidi ya wenzao wachache.
Ni makosa kusema kuwa Waislamu wote ni wenye msimamo mkali...
Katika kichwa cha habari jana kuhusu kukamatwa kwa baadhi ya watu mjini London na Polisi wa Kikosi cha Kupambana na Ugaidi, haikuwa nia yetu kuudhi jamii ya Waislamu. Tunasikitika".
Islamaphobia:
Jambo jingine lililojitokeza katika mkutano huo na kujadiliwa ni "Islamaphobia".
Islamaphobia kama inavyojulikana ni maradhi ya kisaikolojia ambayo mtu aliye nayo huchukia Uislamu na hata chochote kile chenye ishara au kuashiria Uislamu. Jambo hili limekuwa gumu kukubalika kama vile ilivyo rushwa kuwa lipo mahali popote pale, hata kama lipo, kwa vile panahitajika ushahidi ambao si rahisi kuupata, kwa vile hufanyika kimya kimya, na kwa mbinu za hali ya juu, na mikakati thabiti, kama vile mikakati ya baadhi ya vyombo vya habari kama ilivyokwisha tajwa hapo awali.
Islamaphobia imekuja baada ya Xzenophobia iliyokuwa dhidi ya Mayahudi, na Mayahudi walipolalamika, jamii iliyohusika haikukubali kuwa kiti cha namna hiyo kilikuwepo, lakini ni hivi sasa tunaona Mayahudi wakiombwa radhi. Hii inathibitisha kuwa Xzenophobia ilikuwepo japo ilikataliwa wakati ule.
Wakati Waislamu wanalazimika kutambulika (Identity) na hasa katika mavazi yao kama ilivyoamriwa na dini yao. Islamaphobia hulizama hili kwa mtazamo tofauti, na wa chuki, kwa hiyo hujitokeza Maphobia mengine madogo madogo, lakini yenye athari kubwa katika kuvunja mshikamano wa jamii nazo ni kama: Hijabphobia chuki dhidi ya hijab au Kanzu phobia chuki dhidi ya mvaa kanzu kwa sababu ile ile kuwa inaashiria Uislamu, au hata kofiaphobia chuki dhidi ya anaevaa kofia kwa ajili ya Uislamu na kadhalika.
Ili jamii iwe na mshikamano "mutuality" hii ni maradhi ambayo kama yapo basi hayafai na kama hayapo basi na yasije.
Kimsingi Islamaphobia ilikataliwa na kuwa haipo kutokana na ripoti ya tume ya "Runnymede Trust" iliyokuwa imeteuliwa kuchunguza jambo hilo nchini Uingereza na kile kilichojitokeza ni "Racism" ubaguzi wa rangi.
Secularism:
Nyanja nyingine iliyogusiwa na kuzungumziwa katika mkutano huu ni Secularism.
Hii ni hali ambapo mipango yote na taratibu zote za utawala au za kumuendeleza mwanadamu katika nchi, zinatenganishwa na dhana au fikra ya dini yoyote ile.
Mtizamo wa Uislamu una ukingani na mipango yoyote ile, inayomhusu mwanadamu, lakini hapo hapo haimtayarishi au kumpa mazingira ajitayarishie maisha ya akhera.
Kwa mfano, Uislamu unaamini kuwa hali mbaya tuliyonayo sasa hivi ya kushuka kwa maadili ni matunda ya mtizamo wa maisha kisekularism au kisayantism (kisayansi tu).
Kwa hiyo palijitokeza maana mbili ya secularism ndani ya mkutano:
1. Kwa maana ya kutotilia maanani dhana ya dini yoyote ile.
2. Kwa maana ya kutilia maanani dhana ya dini, na kuruhusu kwa upana dini zote kuwatayarisha vijana wake kwa misingi ya dini zote mashuleni na popote pale bila kukumbatia ama kuelemea dini yoyote ile maalum.
Mtizamo huu wa pili ndio ulipendwa na wengi katika mjadala.
Waislamu waliomba katika mkutano huo kuwa tarehe za mitihani mashuleni ziahirishwe, pindi zinapogongana na sikukuu za Kiislamu. Kama vile haki hiyo ilivyo kwa jamii ya Kiyahudi na ya Masingasinga nchini Uingereza hivi sasa.
Uingereza kama Kisiwa cha Elimu ya Kiislamu
Katika mkutano huu wa siku tatu ni mambo mengi yalijitokeza na kujadiliwa na lingine lilikuwa ni jinsi Uingereza ilivyojidhatiti katika kutoa elimu ya Kiislamu katika vyuo vyake mbalimbali na ikatajwa kuwa hivi sasa ilikuwa na vyuo vikuu kumi na sita vyenye kutoa shahada ya juu (masters) katika fani mbalimbali za Kiislamu.
Nitatoa mfano wa vyuo na taasisi chache:
Oxford Centre For Islamic Studies: Hiki ni kitengo chenye uhusiano na chuo kikuu cha Oxford. Kilifunguliwa mwaka 1985 na hotuba aliotoa HRH The Prince of Wales hapo mwaka 1993 kuhusu Uislamu na nchi za magharibi ilisisimua Waislamu wengi duniani na hata hapa Tanzania. Mpaka ilipelekea kusema kuwa Prince Charles amesilimu.
University of Leeds: Post Graduate Programmes in Islamic Studies.
University of Durham: Centre for Middle Eastern and Islamic Studies.
Westhill College of Higher Education Birmingham: BA Degree with qualified Teacher Status of Primary Teaching (Islamic Studies).
Orodha ni ndefu ndugu yangu
msomaji, lakini nadhani unaipata picha kamili jinsi Uingereza iliyojidhatiti
na hasa ukitia maanani kuwa wao, lugha ya Kiarabu, kwenye masomo hayo si
tatizo kwao, bali ni mabingwa wa lugha hiyo hivi sasa.
--
|
|