Na Muhibu Said
KATIKA makala iliyopita, pamoja na kuhitimisha hoja ya utukufu wa mji wa Yerusalem na mji wa Makka, tuliendelea kuona udhaifu wa hoja nyingine miongoni mwa hoja kadhaa za Bw. Elia Batendi zilizochapishwa katika gazeti hili akidai kwamba Allah si Yehova! (Rejea AN-NUUR Na. 205 Uk. 8). Hoja hiyo dhaifu, aliyoitunga ilihusu upendo wa Mwenyezi Mungu (Yehova/Allah) kwa Mayahudi (wana wa Israeli) kama uelezewavyo na Qur'an takatifu na Biblia tukufu. Endelea...
Kuabudia (Kusai') mahala walipofanyia ibada washirikina
Bw. Batendi akiendelea kudai kwamba Allah si Yehova, anasema:
"Yehova amekataza uhusiano na washirikina, ameagiza mahala wanapofanyia ibada pabomolewe, pavunjwe vunjwe (Kut. 34:10-14) Allah ameagiza mahala hapo pafanyiwe ibada ya Kusai (Qur. 2:158)". Mwisho wa kunukuu.
Kwanza, ili kuzidi kumdhihirishia Bw. Batendi kwamba Allah ndiye yule yule Yehova anayekataza uhusiano na washirikina, asome vile vile aya ya Qur'an takatifu ifuatayo:
"Enyi mlioamini! Hakika washirikina ni najisi, kwa hiyo wasiukaribie huo Msikiti mtukufu baada ya mwaka wao huo...". (Qur. 9:28)
Licha ya kuwepo mafundisho kama hayo ya Mwenyezi Mungu (Allah/Yehova) hapo juu yanayovunja kabisa uhusiano kati ya watu wake na washirikina katika masuala ya kiimani, Bw. Batendi akumbuke kwamba ni dini ya Kikristo inayounga mkono na kuipa nguvu imani ya kishirikina (kipagani) kwa kuamini mungu-mtu Zeu au Herme kwa jina lingine "Yesu Kristo" na ibada zake! Neno hili nilikwishalielezea kwa undani katika matoleo ya nyuma yenye kichwa cha habari: "Je, Yehova na Allah ni miungu tofauti?" (Rejea AN-NUUR na 203, 204 na 205, uk. 15).
Pili, mahala hapo walipokuwa wakifanyia ibada washirikina alipopaeleza Bw. Batendi kutoka ndani ya kitabu cha Kutoka 34:10-14 kwamba Yehova ameagiza pabomolewe na pavunjwe vunjwe, maandiko ya Biblia yanaonyesha hapo ni mahala ambapo washirikina wenyewe ndio waliopajenga na kupafanya kuwa ni mahala pao pa kuabudia, kama maandiko hayo (ya Kutoka 34:10-14) yanavyojieleza yenyewe hapa chini:
"... Liangalie neno hili ninalokuamuru leo; tazama, mbele yako namtoa Mwamori, na Mkanani, na Mhiti, na Mperizi, na Mhivi na Myebusi. Ujihadhari nafsi yako, usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi ile unayoiendea, lisiwe mtego katikati yako. Bali utabomoa madhabahu zao na kuvunja vunja nguzo zao, na kuyakata kata maashera yao..."(Kutoka 34:10-14).
Kutokana na maandiko hayo juu, tunaona wazi kuwa mahala hapo kwenye hayo madhabahu, nguzo na maashera ni pa hao washirikina (wapagani) watajwao na maandiko hayo- yaani hapo ni mahala pao walipopajenga wenyewe na kupafanya kuwa ni mahala pa kufanyia ibada zao. Kwa hiyo, Yehova ndio akaamuru pabomolewe na pavunjwe vunjwe.
Tofauti na mahala hapo, Majabali mawili ya "Swafaa" na "Marwaa" yaliyoko Makka ambayo Mwenyezi Mungu ameamuru pafanyiwe ibada ya Kusai (kwenda mbio mara saba baina ya majabali hayo) wakati wa Hijja, hayakujengwa wala kuwekwa na washirikina. Lakini hayo yamekuwepo kizazi na kizazi, tangu Mwenyezi Mungu alipoyaumba mahala hapo yalipo.
Na kwa kuwa hapakuwa ni mahala pao, baada ya washirikina kuyavamia majabali hayo na kuweka juu yake masanamu na kuyaabudu, Mtume Muhammad (s.a.w.) alipokuja, baada ya kupewa ibada ya Hijja aliwaondoa washirikina hao na masanamu yao na ndipo akaamriwa na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) apafanyie ibada hiyo ya Kusai (Rejea Sira na Qur'an 2:158).
Kwa kuzingatia ukweli huu ili kumdhihirishia zaidi Bw. Batendi kwamba Allah ndiye Yehova kwa "kigezo" chake hicho, kama Qur'an Takatifu, Biblia tukufu nayo vile vile haionyeshi mahali popote ambapo Yehova ameagiza nyumba yake (Hekalu takatifu) ibomolewe na kuvunjwa vunjwa kwa sababu ya washirikina kuivamia na kuendesha ibada zao ndani yake. Uthibitisho wa Hekalu lake kuvamiwa na washirikina tunaupata katika maandiko ya Biblia tukufu yafuatayo:
"Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka hamsini na mitano. Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, sawa sawa na machukizo yote ya mataifa, aliowafukuza BWANA mbele ya wana wa Israeli... Akajenga madhabahu katika nyumba ya BWANA, napo ndipo alipopanena BWANA, katika Yerusalemu litakuwako jina langu milele. Akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la mbinguni katika nyua mbili za nyumba ya BWANA... Akaiweka sanamu ya kuchonga aliyoifanya, katika nyumba ya Mungu ambayo Mungu alimwambia Daudi, na Sulemani mwanawe, katika hii, na katika Yerusalemu, niliouchagua miongoni mwa kabila zote za Israeli, nitaliweka jina langu milele". (Mambo ya Nyakati 33:1-7).
Maandiko hayo juu yanaonyesha wazi jinsi Mfalme Manase wa Yerusalemu wa zama hizo alivyoivamia nyumba takatifu (Hekalu) ya Mwenyezi Mungu (Yehova/Allah) na kuingiza ndani yake ibada za kishirikiana yakiwemo pia masanamu ya kuchonga. Pamoja na hayo,k hatuoni mahali popote ndani ya Biblia tukufu ambapo Yehova anaamuru Hekalu hilo libomolewe au livunjwe vunjwe.
Sambamba na ukweli huo, Biblia pia haionyeshi Nabii Yesu (s.a.) akilibomoa au kulivunja vunja Hekalu hilo baada ya kuwakuta watu katika zama zake wakifanya biashara ndani yake badala ya sala, kama tunavyosoma maandiko ya Biblia Tukufu yafuatayo:
"Na Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu, naye Yesu akakwea mpaka Yerusalemu. Akaona pale hekaluni watu waliokua wakiuza ng'ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi. Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng'ombe, akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao; akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara". (Yohana 2:13-16)
Hapa tunaona Nabii Yesu (a.s.) akidhihirisha hasira yake kwa kuwafukuza wote waliovamia hekalu la Mungu na kufanya biashara ndani yake kwa kupindua meza zao na kumwaga fedha zao tu; na si kubomoa hekalu lenyewe au kulivunja vunja. Kwa shuhuda hizo chache, Bw. Batendi kudai kwamba Allah si Yehova kwa kutegemea hoja hiyo, ni sawa na kujikinga na baridi katika nyumba ya buibui.
Maagano ya Mungu na damu!
Bwana Batendi anaendelea kupinga Allah ni Yehova kwa kusema:
"Yehova hufanya maangano yake kwa damu. Alifanya agano na Ibrahimu akamwagiza achinje njiwa (Kut. 15:7-10) ili kumhakikishia Ibrahimu kuwa uzao wake utarithi nchi ya Kanaani, katika tukio hilo Mungu Allah anawafufua njiwa hao kuonyesha uwezo wake wa kufufua na wala siyo agano". Mwisho wa kunukuu.
Kwanza, yaonyesha dhahiri Bw. Batendi hakuyasoma kwa moyo wa kutaka kuelewa ukweli maandiko hayo ya Qur'an takatifu na Biblia tukufu aliyoyataja hapo juu ambayo yanaeleza bayana jinsi Mwenyezi Mungu alivyomwamuru Nabii Ibrahim (a.s.) kuchinja katika mawili matukio tofauti.
Tukio linaloelezwa na Qur'an takatifu lilihusu agizo moja la Mwenyezi Mungu kwa Nabii Ibrahimu (a.s.) la kuchinja ndege tu wanne ili Mwenyezi Mungu kumuonyesha (Nabii Ibrahm a.s.) uwezo wake wa kufufua, moyo wake (Nabii Ibrahimu a.s.) upate kutulia; kama aya zenyewe za Qur'an takatifu zinavyojieleza hapa chini:
"Na (kumbuka) Ibrahimu aliposema: "Mola wangu! Nionyeshe jinsi utakavyofufua wafu". (Mwenyezi Mungu) akasema: "Huamini?". Akasema" "La (naamini), lakini (nataka kuona hayo) ili moyo wangu utulie (zaidi)". Akasema: Basi chukua ndege wanne na uwazoeshe kwako (uwadhibiti vizuri sura zao hata wasikupotee popote unapowaona), kisha (wachinje) uweke juu ya kila jabali sehemu katika wao. Kisha waite, watakujia mbio. Na ujue ya kwamba Allah ni mwenye nguvu, na mwenye hikima". (Qur'an 2:260).
Tofauti na tukio hilo (lielezewalo na Qur'an hapo juu), tukio linaloelezwa na Biblia tukufu linahusu amri nyingine ya Mwenyezi Mungu kwa Nabii Ibrahimu (a.s.) si kuchinja njiwa tu kama adaivyo Bw. Batendi hapo juu, bali ni kuchinja ndama, mbuzi, kondoo na hua pia, ili Mwenyezi Mungu kumhakikishia (Nabii Ibrahim a.s.) kwamba uzao wake utarithi nchi ya Kanaan, kama maandiko hayo ya Biblia tukufu yanavyojieleza hapa chini:
"Baada ya mambo hayo neno la BWANA likamjia Abrahamu katika njozi, likinena, usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako na thawabu yako kubwa. ... kisha akamwambia, Mimi ni BWANA, niliyekuleta kutoka Uru wa Wakaldayo nikupe nchi hii ili uirithi. Akasema, Ee Bwana Mungu, nipateje kujua ya kwamba nitairithi? Akamwambia, unipatie ndama wa miaka mitatu, na mbuzi mke wa miaka mitatu, na kondoo mume wa miaka mitatu, na hua, na mwana njiwa. Akampatia hao wote, akawapasua vipande viwili, akaweka kila kipande kuelekea mwenzake,ila ndege hakuwapasua... siku ile BWANA akafanya agano na Abramu, akasema uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati..." (Mwanzo 15:1-21)
Kwa uchache, huu ndio utofauti ulio mbali kabisa kati ya agizo hilo la Mwenyezi Mungu (Yehova/Allah) kwa Nabii Ibrahimu (a.s.) la kuchinja, lililoelezwa na Qur'an takatifu na hilo lililoelezwa na Biblia tukufu.
Laiti Bw. Batendi angeliyasoma maandiko hayo juu (ya Qur'an takatifu na Biblia tukufu yanayoonyesha utofauti wa matukio hayo mawili kwa Nabii Ibrahim a.s.) kwa akili huru na kwa moyo wa kutaka kuelewa ukweli, asingediriki kabisa kutumia "kigezo" cha matukio hayo mawili tofauti kupinga Allah ndiye Yehova, huku akijua wazi kwamba kufanya hivyo ni kutegemea hoja dhaifu isiyokuwa na msingi wowote.
Pili, siyo kweli kabisa kwamba Mwenyezi Mungu (Yehova/Allah) siku zote hufanya maagano yake kwa damu kama adaivyo Bw. Batendi hapo juu. Kwa ujumla, damu haina uzito wala ulazima katika dini ya Mwenyezi Mungu kama ambavyo Wakristo wamekuwa wakiipa uzito. Uthibitisho kwamba damu haina ulazima katika dini ya Mwenyezi Mungu (Yehova/Allah) tunaupata katika maandiko ya Qur'an takatifu na Biblia tukufu yafuatayo:
"Naye Samweli akasema, Je! BWANA hzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu sawa sawa na kuitii sauti ya BWANA? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu". (1 Samweli 15:22)
"Huu wingi wa sadaka zenu mnazonitolea una faida gani? asema BWANA. Nimejaa mafuta ya kafara za kondoo waume, na mafuta ya wanyama walionona, nami siifurahii damu ya ng'ombe wala ya wana-kondoo wala ya mbuzi waume... Haya, njoni, tusemezane, asema BWANA. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu. Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha BWANA kimenena haya". (Isaya 1:11-20)
"Na ngamia (na ng'ombe na mbuzi na kondoo wa sadaka) tumekufanyieni kuwa katika alama za (dini ya) Allah; kwa hao mnayo kheri (nyingi). Basi litajeni jina la Allah juu (kutii) yao wasimamapo safu safu (mnawachinja); Na waangukapo ubavu, kuleni katika hao na mlishe makafiri, wanaoomba na wanaoroandearondea bila ya kuomba. Namna hivi tumewatiisha kwa ajili yenu ili mpate kushukuru. Nyama zao (wanyama hao wanaoachinjwa) hazimfikii Allah wala damu zao, lakini inamfikia taa yenu...". (Qur. 22:36-37)
Kulingana na maandiko hayo juu, Mwenyezi Mungu (Yehova/Allah) anatuthibitishia wazi kwamba utii (ucha Mungu) kwake ni bora kuliko damu; na kwa hiyo damu kwake siyo lazima.
Uthibitisho mwingine unaoonyesha kwamba damu haina uzito wala ulazima wowote katika dini ya Mwenyezi Mungu, si Qur'an tu bali Biblia pia haionyeshi mahali popote Mwenyezi Mungu akimwagiza Nabii Zakaria (a.s.) kuchinja alipomwahidi kumpa mtoto kama alivyomwamuru Nabii Ibrahimu (a.s.) kuchinja alipomwahidi uzao wake utarithi nchi ya Kanaani.
Tofauti na amri ya kuchinja aliyopewa Nabii Ibrahim (a.s.) alipotaka uhakika wa ahadi hiyo (ya uzao wake kuirithi nchi hiyo ya Kanaani), Nabii Zakaria (a.s.) naye alipotaka uhakika juu ya ahadi ya Mwenyezi Mungu kumpa mtoto, hakumwambia achinje. Lakini maandiko yanaonyesha alipewa amri iliyo kinyume chake, kama tunavyosoma maandiko yafuatayo ya Biblia tukufu na Qur'an takatifu:
"Lakini yule malaika akamwambia, usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana.... Zakaria akamwambia malaika, Nitajuaje neno hilo?Maana mimi ni mzee, na mke wangu ni mkongwe wa siku nyingi. Malaika akamjibu akamwambia, Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele ya Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha habari hizi njema. Na tazama! Utakuwa bubu, usiweze kusema, mpaka siku ile yatakapotukia hayo; kwa sababu hukuyasadiki maneno yangu; nayo yatatimizwa kwa wakati wake". (Luka 1:13-20).
"(Akaambiwa) "Ewe Zakaria! Tunakupa habari njema ya (kuwa utazaa) mtoto, jina lake ni Yahya: Hatujafanya kabla yake aliye na jina namna hilo. Akasema: "Mola wangu! Nitapataje mtoto, hali mke wangu ni tasa, na mimi nimekwisafikia uzee wa kupita kiasi"... Akasema: Mola wangu, Nifanyie ishara (ya kujua kuwa sasa mke wangu amekwishashika mimba)". Akasema: "Ishara yako ni kuwa hutaweza kusema na watu kwa siku tatu, na hali wewe ni mzima"" (Qur. 19:7-10).
Maandiko hayo juu yanaonyesha wazi amri aliyopewa Nabii Zakaria (a.s.) baada ya kutaka uhakika wa kupata mtoto, ni kufunga kusema (kuwa bubu) na siyo kuchinja. Kwa shuhuda hiyio pia, ni wazi kuwa damu katika dini ya Mwenyezi Mungu haina ulazima wala uzito wowote.
Wakristo (akina Batendi) wanapong'ang'ania damu katika kila penye fununu ya mambo yahusuyo "damu" katika maandiko ya kale, ni katika kutapatapa kwao tu katika kuitafutia uhalali ibada yao ya kipagani ya kuua wana kama kafara ya dhambi zao katika mafundisho ya kale ya Mwenyezi Mungu.
Ibada hii (ya kuua wana ambayo i sawa na kuunga mkono kwa Wakristo dhana ya kuuliwa mwana wa Mariamu a.s. kama kafara ya dhambi zao) ni ibada ya kipagani ambayo ni batili, najisi na ni machukizo makubwa kabisa katika dini ya Mwenyezi Mungu (tazama Kumbukumbu la Torati 18:9-11; 2 Wafalme 16:1-3; Zaburi 106:35-38; Yeremia 10:1-3). Kwa uchambuzi wa kina juu ya ibada hii ya kipagani (ya kuua wana kama kafara ya dhambi) ambayo imo pia ndani ya Ukristo, rejea AN-NUUR namba 204, ukurasa wa 15).
|
|