Na Juma Choloi
BAADHI ya Waislamu Jijini wameonyesha kushangazwa na mwelekeo wa kampeni za Chama cha NCCR-Mageuzi katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Ubongo.
Wakiongea na mwandishi wa habari hizi kando kando ya barabara ya Morogoro jirani na maungio ya barabara ya Ubungo inayoelekea nyumbani kwa mgombea katika uchaguzi huo kupitia chama hicho, Bwana Abdulkarim Ali Atik, Waislamu hao walisema kampeni za chama hicho zenye kulenga kumpaka matope mgombea kwenye uchaguzi huo kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Bw. Hussein Mmassy usio na maana na umekosa pa kushika.
Wakifafanua wamesema kuwa pamoja na kampeni nyingine katika siku za hivi karibuni, kampeni za chama hicho zimekuwa zikiwaomba Waislamu kutompigia kura mgombea wa CUF kwa madai kwamba si Muislamu bali ni Mkristo anayejisingizia Uislamu kwania ya kupata kura za Waislamu.
"NCCR wanatushangaza sana kwa sababu haihitaji akili za ziada kuona kuwa kinachogombewa katika uchaguzi huu ni Ubunge na wala si Uimamu! Sasa suala la dini ya mgombea awe yeyote yule linakuja vipi?" Alihoji Bwana Saad Sabu.
Akiunga mkono, Bwana Twahir Msangi alisema kuwa kama Waislamu wameonyesha kukiunga mkono Chama cha CUF katika uchaguzi huo hilo halitokuwa na sababu nyingine zaidi ya sera za chama hicho zinazolenga kuleta haki sawa kwa Watanzania wote bila kujali dini zao au hana dini.
"Waislamu siku zote wamekuwa na madai kuwa wanaonewa kwa ajili ya Uislamu wao. Serikali ya CCM badala ya kushughulikia madai hayo imekuwa ikiongeza unyanyasaji. Sasa kama CUF wanasema wako kwa ajili ya haki sawa kwa wote ni wajibu wa Waislamu kukiunga mkono chama hicho kwa nguvu zao zote", alimalizia Bwana Msangi.
Naye Bwana Riziki Kibakaya alikitaka chama cha NCCR-Mageuzi kuachana na kauli zinazotoa picha kwamba chama hicho ni wakala wa CCM na badala yake kiungane na CUF katika juhudi zake za kuwakomboa Watanzania kutoka kwenye minyororo ya CCM.
"Mwaka huu ni wa kihistoria. Ukombozi wa pili wa Mtanzania unaanzia hapa Ubungo na Temeke. Kama wazee wetu walivyochangishana shilingi moja moja zao, nasi tutachangishana mia mia zetu mpaka CCM ing'oke", alisema.
Alimalizia Bwana Kibakaya kwa kuvitaka vyama vingine vya upinzani kuziunga mkono juhudi hizo za wananchi chini ya uongozi wa CUF ili kesho na keshokutwa visije vikawekwa kwenye kapu moja na CCM.
Bwana Said Kapera yeye alikiomba
chamacha CUF kuongeza jitihada zake kwa kuwa wananchi wanakielewa na wamejitoa
muhanga kukiunga mkono.
Na Mwandishi Wetu
HALI mbaya ya njaa inayowakabili wananchi wa Tarafa ya Mzenga, wilayani Kisarawe, imedaiwa kutumiwa 'kikampeni' na serikali hivi karibuni ikiwa ni jitihada ya kudhibiti juhudi za wanawake wa Kiislamu kuzindua jamii.
"Kampeni" hiyo ya serikali imedhihirika wiki iliyopita baada ya kulazimika kuwapelekea msaada wa mahindi wananchi waishio katika vijiji kadhaa vya tarafa hiyo walioathirika na njaa isiyosemeka tangu serikali ya awamu ya tatu iingie madarakani.
Ugawaji huo wa mahindi tarafani hapo umedaiwa kuwa umetokana na msukumo wa hofu ya serikali baada ya kupokea taarifa ya ziara ya kinamama wa Kiislamu wa Jijini iliyofanyika wiki iliyopita tarafani hapo, iliyoandaliwa na Kamati ya Wanawake wa Kiislamu Tawi la Gongo la Mboto ikiwa ni katika juhudi zao za kuwazindua walioghafilika katika dini na dunia.
Taarifa iliyotolewa na kamati hiyo, imeeleza kuwa hatua hiyo ya serikali ilimfanya Katibu wa Msikiti wa Kijiji cha Nyani, Tarafani hapo, Bw. Mohamed Amiri Kupo kuwaomba radhi wageni waliofika kijijini kwake kwa kushindwa kujumuika pamoja nao katika muhadhara wao kutokana na kulazimika kuungana na makundi ya wananchi waliokimbilia mgao huo wa mahindi.
Taarifa hiyo imemkariri Katibu huyo akieleza kuwa wana kijiji hicho walistushwa na kupatwa na kiwewe kwa kuuona msaada huo umeletwa ghafla kijijini kwao ambao alisema kamwe hawakutegemea kuupata maishani mwao baada ya kukata tamaa kutokana na serikali kuwatelekeza na njaa kwa muda mrefu na hivyo kutokuwa na imani nayo tena.
Msaada huo wa mahindi ulitolewa na taasisi ya World Food Programme.
Taarifa za kufanyika kwa mihadhara ya kinamama hao kutoka Jijini Dar es Salaam katika tarafa ya Mzenga zilitolewa katikati na mwishoni mwa mwezi Juni na kusambazwa maeneo ya tarafa hiyo.
Kufuatia kuenea kwa taarifa hizo tarafani hapo, mamia ya waumini wake kwa waume walimiminika stesheni ya Mzenga kuulaki msafara wa kinamama hao ambapo Alhamisi ya Julai 1, mwaka huu walifanya muhadhara wao katika kijiji cha Mitengwe, Masjid Samaawiyya Mitende, kwa Sheikh Kondo Maulid Jokolo.
Ijumaa ya Julai 2, msafara huo ulielekea katika kijiji cha Mzenga A na baada ya kuswali Adhuhuri Msikitini hapo, waadhi ulitolewa kwa wanakijiji hao na kisha msafara huo ulielekea katika kijiji cha Turini na kupata mapokezi makubwa kutoka kwa kinamama wa Kiislamu wa kijiji hicho. Muhadhara kijijini hapo ulifanyika siku hiyo kuanzia saa 9.00 mchana hadi saa 12.00 magharibi.
Msafara huo pia ulipata mapokezi mengine makubwa katika kijiji cha Bepele kutoka kwa waumini wake kwa waume wa kijiji hicho waliokuwa wakiusubiri kwa hamu kubwa ambapo walipata fursa ya kusikiliza muhadhara kutoka kwa msafara huo.
Msafara huo ulihitimisha
ziara yake hapo, katika kijiji cha Nyani ambako ni saa 1.30 kufika kwa
mwendo wa miguu kutoka stesheni ya kijiji cha Bepele.
Na Idd Kikong'ona
WAKATI madai ya Waislamu dhidi ya serikali ya Chama tawala kuhusu haki zao za kikatiba pamoja na mauaji ya Mwembechai bado yanasota katika foleni yakisubiri uchunguzi wa kisayansi, polisi imedaiwa kuendeleza vitisho kwa wanaotaka kushuhudia ukweli wa mauaji hayo kupitia mkanda wa hiyo sakata.
Taarifa zilizopatikana hivi karibuni zinadai kuwa zaidi ya askari watatu wilayani Kilosa mjini Morogoro waliwavamia waumini kadhaa wa Kiislamu wanaoishi Kimamba na kuwapekua majumbani mwao kwa madai ya kuutafuta mkanda unaoonyesha mauaji ya ria wasiokuwa na hatia yaliyofanywa na jeshi la polisi mwaka jana pale Mwembechai.
Aidha, imeripotiwa kuwa askari waliofanya zoezi la upekuzi uliolenga kuzitia nguvuni kanda pamoja na wahusika ili kudhibiti athari za kushuhudiwa kwake, walifanya hivyo baada ya kupata fununu kuwa wananchi wa Kimamba nao wanapata fursa ya kuyashuhudia mauaji yaliyopongezwa na viongozi wa serikali ya chama tawala.
Kwa mujibu wa maelezo ya Muislamu mmoja aliyeponea chupuchupu kupitiwa na pekua pekua hiyo, mkanda unaobainisha namna ya Waislamu walivyouawa pale Mwembechai, takriban ulionyeshwa kwa siku mbili na kuwafanya wananchi waliobahatika kuhudhuria wapigwe na butwaa kutokana na ile operesheni tungua tungua iliyoongozwa kwa sauti ya "piga shaba", iliyorudiwa rudiwa.
Miongoni mwa sababu zilizodaiwa kutolewa na polisi walioshiriki harakati za kudhibiti kuenea kwa athari ya mkanda wa mauaji, ambazo wananchi wengi wanazitafsiri kama ni jitihada za serikali katika kuifunika aibu iliyolikumba taifa zinasema kuwa mkanda huo unahatarisha kuvurugika kwa amani endapo utaachwa utazamwe na wananchi.
Vile vile imesemwa kuwa wananchi watapoteza imani yao juu ya uadilifu wa serikali katika kuwatendea haki raia zake ikiwa yale yaliyofanyika kwenye sakata ya Mwembechai yatapata nafasi ya kutafakariwa kwenye akili za watu kupitia milango ya macho na masikio yao.
"Ikiwa kitendo kilichofanywa na serikali dhidi ya Waislamu ni sahihi kiasi cha kupongezwa na kuwapa haki ya kutofikishwa walioshiriki mauaji ili wasikutane na sheria, kwanini basi serikali inajawa hofu pindi wananchi wakipewa fursa ya kuyashuhudia mauaji yaliyopongezwa?" Alihoji Bw. Zuberi Ginde ambaye ni mkazi wa Kimanda wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi.
Imeripotiwa kuwa miongoni mwa Waislamu waliosachiwa na polisi ni Bw. Said Mwangoro na Salehe Simon wakifuatiwa na Bwana June Sengo. Wote hao ni wakazi wa Kimamba ambao walihisiwa kuwa wanamiliki mikanda hiyo inayodaiwa na vyombo vya dola kuwa inahatarisha amani ya Taifa.
Hata hivyo, taarifa zimedai kuwa hakuna miongoni mwao aliyekutwa na nakala ya mkanda wa mauaji ya Mwembechai, ijapokuwa hakuna haki inayowkataza wao na Waislamu wengine pamoja na wananchi kwa ujumla wasijue uhalisia wa tukio hilo la kihistoria kwa kutumia sayansi na teknolojia iliyopo.
"Inasikitisha kuona vyombo
vya dola vikiripotiwa kutenda yote haya wakati madai ya Waislamu kuhusu
haki zao za kiraia pamoja na mauaji ya ndugu zetu pale Mwembechai bado
yanasota kwenye foleni huko Ikulu yakisubiri kukamilika kwa uthibiti wa
kisayansi", alimalizia Bwana Zuberi.
--
|
|