Maimamu Dar waijia juu CCM
 

Na Mwandishi Wetu
 

MAIMAMU Jijini wamelaani kauli iliyotolewa na Katibu Mkuu wa CCM Bwana Philip Mangula ikinasibisha Misikiti na vitendo vya vurugu na rushwa.

Wamesema kauli hiyo ililenga kuudhalilisha Uislamu na kuwatukana Waislamu.

Katika taarifa yao kwa vyombo vya habari iliyosambazwa jana ambayo imesainiwa na Amir wa Shura Sheikh Juma S. Mbukuzi, Maimamu hao wamesema kauli ya Katibu Mkuu wa CCM imekashifu Misikiti.

"Ni kiwango cha juu kabisa cha kuudhalilisha Uislamu kuunasibisha Msikiti na pango la wala rushwa", imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Maimamu hao wamesema majibizano ya kisiasa yana viwanja vyake kwa hiyo haikuwa busara kwa Katibu huyo kuelekeza mashambulizi yake dhidi ya Waislamu.

"Endapo CCM wanahisi wamezidiwa katika viwanja hivyo wasiwaparamie Waislamu na kuwatukana", taarifa hiyo imeonya.

Ikikumbusha madhila yaliyofanywa na serikali ya CCM dhidi ya waumini wa dini ya Kiislamu mapema mwaka jana, taarifa hiyo imesema Katibu huyo angeona uzito kutamka maneno hayo kwa kuchelea kuzidi kuwaudhi Waislamu.

"Katika hali ya kawaida baada ya baadhi ya vyombo vya dola vya serikali ya CCM kuvamia Msikiti, kuwadhalilisha akina mama, kuwatia vilema Waislamu na kuwaua wengine kwa risasi na baadhi kufa baada ya mateso gerezani, isingetegemewa leo viongozi wake kuja na kauli hizi za kuwatukana na kuikashifu dini yao", imedai taarifa hiyo yenye vifungu tisa.

Aidha, imesema ni fikra potofu kudhani kuwa Muislamu mzuri ni yule anayekubali kutukaniwa dini yake akasema hewala.

Wiki mbili zilizopita, Katibu Mkuu wa CCM Bwana Philip Mangula aliripotiwa na vyombo vya habari akiishutumu Misikiti kuwa ilikuwa ikitumika kufanya kampeni za chaguzi ndogo katika majimbo ya Temeke na Ubungo.

Bwana Mangula alidai kuwa kuna fujo zimeandaliwa katika baadhi ya Misikiti na waumini kuhonga kanzu na kofia ili kukiunga mkono chama ambacho hakuweza kukitaja.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook