CUF yashutumu kauli ya Sumaye Bungeni
 

Na Mwandishi Wetu

CHAMA Cha Wananchi (CUF) kimeshutumu hatua ya serikali kutoa matamshi ya vitisho dhidi ya wapiga kura sambamba na madai kwamba hairidhishwi na kampeni za CUF katika majimbo ya uchaguzi.

CUF imeyasema hayo katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika eneo la Mabibo Juzi.

Chama hicho cha Wananchi kimesema serikali kuwa mzungumzaji katika masuala ya kampeni ni kuingilia utendaji wa Tume ya Uchaguzi yenye jukumu la usimamizi wa shughuli hiyo.

Imesema hatua hiyo ya serikali dhidi ya vyama vya upinzani inaleta wasiwasi wa kutokuwepo haki na huenda zipo njama za kutaka kukisaidia chama tawala (CCM) ambacho hivi sasa kinaonekana kuwa taabani katika majimbo yote, hivyo kupoteza matumaini ya ushindi kwa wagombea wake,

Katikati ya wiki hii Waziri Mkuu Mheshimiwa Frederick Sumaye alisimama Bungeni na kutoa kauli ya kuvishutumu vyama vya upinzani katika majimbo ya uchaguzi mdogo Jijini kwa kuendesha kampeni alizodai kuwa zinahatarisha amani na kumuombea mabaya Rais Benjamin Mkapa.

Aidha, Waziri Mkuu aliviagiza vyombo vya dola kuweka ulinzi mkali siku ya uchaguzi ili kudhibiti kile alichokiita uwezekano wa kutokea vurugu.

Kauli ya Waziri Mkuu ilikuja siku chache baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Bibi Rita Mlaki kudai kwamba Rais Benjamin Mkapa anakashifiwa katika kampeni za Chama cha CUF.

Pamoja na shutuma za Bibi Rita Mlaki, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam naye alitoa ilani ya kuwepo ulinzi mkali siku ya uchaguzi ambao haujapata kuonekana. Lengo la ulinzi huo ni kudhibiti chama ambacho kimeagiza wasimamizi wa kura kutoka nje ya Dar es Salaam.

Hivi karibuni CUF imeripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa inampango wa kuagiza kundi la wanachama wake kutoka sehemu nyingine ili kusimamia kuhesabu kura kwa kuchelea wizi wa kura unaofanywa na chama fulani.

Uchaguzi mdogo wa viti vya ubunge katika majimbo ya Temeke na Ubungo unatazamiwa kufanyika Jumapili Julai 11, mwaka huu.

Wakati huo huo, CUF imewataka wananchi wajitokeze kwa wingi kama walivyojiandikisha kupiga kura na wasiogope vitisho vya CCM na serikali yake. Chama hicho kimesema mikiki, vitisho na propaganda zinazofanywa na CCM ni ushahidi wa kushindwa na kwamba sasa inataka kuzuia wananchi wasipige kura.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana Mkurugenzi wa habari wa Chama hicho aliwataka wananchi wanaowaunga mkono wagombea ubunge majimbo ya Ubungo na Temeke wahakikishe kuwa wanawahi mapema kabisa vituoni kupiga kura zao na wala wasitishike na mikimikiki watakaoiyona ya polisi.

Mkurugenzi huyo wa habari alisema kuwa chama chake kishapeleka malalamiko rasmi kwa Tume ya Uchaguzi juu ya njama zinazolenga kuwapokonya wananchi haki yao ya kumchagua kiongozi wamtakaye.

Malalamiko yao amesema yamejumuisha njama za CCM, vitendo vya baadh ya vyombo vya dola na utaratibu uliopangwa na Tume yenyewe.

Katika masiku ya hivi karibuni serikali imekuwa ikitoa kaui kwamba itaweka ulinzi mkali ili kudhibiti hujuma yoyote inayoweza kufanyika siku ya kupiga kura.

Nayo taarifa ya CCM iliyonukuriwa na vyombo vya habari jana imedai kuwa chama hicho kimetangaza vita dhidi ya CUF. 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook