SERIKALI ina hiari ya kujiunga na OIC au kuacha. Aidha serikali ina hiari yake kuendelea kuwa na cheo cha Muft au iingie karne ya 21 na cheo cha Kadhi.
Hivi sasa wananchi wanakamuliwa kodi mpaka mikanda waliokaza viunoni haishiki tena kwa viuno kuwa nyembamba. Kodi hiyo ikienda kusaidia kulegeza kitanzi cha madeni kilichoikaba koo nchi yetu kutokana na misaada na mikopo ya riba.
Wajanja kama Uganda na Msumbiji wenye uchungu na hali mbaya inayowakabili wananchi wake walishajiunga na OIC ili kunufaika na misaada na mikopo isiyo na riba.
Misaada na mikopo hiyo kama ilivyo sera ya OIC haipitii katika mashirika ya dini au binafsi kama ilivyo kwa misaada ya baadhi ya nchi za Ulaya kama Ujerumani ambazo hupitia Makanisani baada ya 'Memorundum of Understanding'.
Misaada hiyo hupitia serikalini na ni serikali inayopanga itumike vipi kwa manufa ya wananchi. Na kwa manufaa ya jumuiya hiyo huwezi leo kumwambia Museven atoke OIC akakubali.
Kwa nchi kama yetu Tanzania Waislamu watanufaika zaidi na misaada ya OIC kama serikali haitajiunga. Waislamu kwa kupitia taasisi zao wakiomba misaada toka OIC itawanufaisha wao kama Waislamu. Lakini nchi ikishajiunga misaada yote hupitia serikalini.
Zikija nafasi za masomo nchi za nje hamsini, wataenda Wakristo 49, Waislamu mmoja kama ilivyo ada Waislamu kupunjwa. Zikija fedha za mradi wa maji, kilimo au barabara maofisa watakaozipokea na kuzifanyia kazi na hivyo kuwanufaisha ama kwa mishahara, marupurupu na mengineyo kwa mfumo uliopo wengi watakuwa Wakristo.
Nasaha za Waislamu kwamba serikali ijiunge na OIC ni kutaka serikali na wananchi wanufaike na misaada hii isiyo na tone la riba na wala si kwamba kwa kujiunga serikali inawafanyia Waislamu fadhila au kwamba Waislamu watapata manufaa zaidi ya wananchi wengine.
Sasa serikali yenyewe ina hiari kujiunga au kuacha. Linalowashughulisha wanaoibuka na matawi ya Kosovo, Hamas, Chechnya, Usama bin Laden na Bosnia si OIC wala kadhi. Hawa wanapigania ukombozi. Wanataka kutambuliwa kwamba nao ni watu wasiostahili kuuliwa kama swala.
Wenye tawi lao la Albania hawapiganii ukadhi. Wanataka kuikomboa nchi hii kutoka makucha ya wale wenye dhana potofu kuwa kuchagua Wakatoliki watupu kugombea Ubunge ndio Utanzania ila wasipokuwa wao ni udini. Kadhi wa nini katika serikali iliyo tayari kuona vyombo vyake vya dola vikivamia Misikiti ya Waislamu na kuwaua baada ya kuwadhalilisha waumini wanawake.
Katika mazingira haya kadhi ni kwa manufaa ya serikali kama ilivyo Muft leo anavyowagawia watu vyeo vya Najash.
NATO, Soweto na matawi mengine kama 'mashujaa wa Mwembechai' na mengine yatakayoibuka, agenda zao si Kanisa dhidi ya Msikiti au kinyume chake. Lao ni moja; kupigania haki za wanaochomewa nyumba zao moto kisha zikaitwa 'vidunda'; kuhoji mantiki ya wao kukamuliwa kodi huku wakifa kwa kipindupindu na homa ya matumbo kwa kukosekana kwa huduma safi za maji na zile za afya.
Hawa ni watetezi wa wale wanaosutwa katika vyumba vya kujifungulia (Martenity ward) kwa vile hawana pamba au gloves na mshiko wa 'nesi' wakati wenyewe ni hohehahe na kodi ya maendeleo washalipa.
Sura inayojitokeza katika kampeni za uchaguzi Ubungo na Temeke ni kuwa wananchi wanapigania haki zao. Wanaitaka serikali izindukane iwatizame na kuwathamini wananchi walioiingiza madarakani.
CCM inageuza agenda kuwaambia wananchi kuna tatizo la udini 'Ni Waalbania wasio wataka Waserbia'. CCM inadhani yaweza kunufaika na propaganda hizi lakini gharama yake ni kubwa kwa taifa.
Na pengine kinachotisha
zaidi ni kuwa serikali ambayo ina hamu ichaguliwe tena kwa kipindi kingine
cha miaka mitano haielekei kuona kuwa kuuliwa watu Mwembechai ni tatizo.
Je ikianza kipindi kingine ambacho haitarajii tena kurejea kwa mujibu wa
katiba ya nchi!
--
|
|