Na Mussa Ally, Morogoro
HEBU tuutazame mpango wa nguvu kazi kwa macho mawili, wananchi wengi waliohojiwa na gazeti hili wameweka wazi hisia na fikra zao kuwa licha ya uzuri wa jina la mango wenyewe (nguvu kazi) na ndoto za walioubuni kwamba utamtoa mwana Morogoro katika shimo la umaskini na kumuingiza katika mwanga wa maendeleo kiuchumi, bado haukuwashirikisha kikamilifu walengwa ambao ndio watekelezaji wakuu.
Ni kikubwa zaidi hakukuwa na mawasiliano mazuri kait ya viongozi na wananchi (wakulima) kabla na baada ya mpango huo kupitishwa.
"Mpango wa nguvu kazi ulikwepa kabisa hatua za msingi za mawasialino na wakulima badala yake ukaegemea katika amri bila kutazama athari zake mbeleni".
Kiuhakika ardhi ya mkoa wa Morogoro tunaweza kuigawa katika makundi makubwa matatu, yaani eneo la milima na nyanda za juu, sehemu ambayo hulimwa sana mazao kama mahindi, migomba, matunda, mboga za majani, viazi mviringo,ngano na kahawa kiasi. Kundi hili linaibeba milima ya Uruguru, Rubeho, Unguu na Mahenge (sehemu ambayo njaa iliacha zaidi ya watu 45 wakiwa marehemu hivi karibuni!).
Eneo la ardhi tambarare na mabonde ni sehemu nyingine ya ardhi ya Morogoro ambapo mazao kama maharage, kunde, vitunguu, pamba, alizeti, ufuta, choroko, miwa na korosho hupatikana kwa wingi. Wilaya ya Morogoro na Kilombero kwa kiasi kikubwa ziko katika eneo hilo.
Sehemu zenye miinuko chini ya milima hasa katika wilaya ya Morogoro (mjini na vijijini) na Kilosa ni kundi lingine la ardhi ya mkoa huo. Matunda, mboga, mpunga, mahindi, migomba, mbegu za mafuta na mkonge.
Soko si la uhakika, usafiri wa kutatanisha, utalaam duni wa kusindika mboga, matunda na mazao kwa ujumla kuwa ni miongoni mwa vile 'vinavyowanyonga' wakulima wa Morogoro.
"Hatuna hata kiwanda kimoja cha kusindika vyakula mkoani kwetu, usinambie wataalam wa kilimo ambao wangeweza kutupa njia rahisi na bora za kusindika mazao yetu", alilalamika mzee Mtenga.
"Ni aibu kwa mkoa wenye Chuo Kikuu cha Kilimo halafu wakulima wake wanakosa wataalam hali hii inautusi mkoa huu na Taifa kiujumla", mkulima mwingine Sewando Josephat Mwinyigoha ametoa lawama zake kwa serikali.
Bwana Sewando pia anaililia serikali kwa kutoa huduma ya mahandaki na migodi isiyo rasmi badala ya barabara kwa maana ya barabara, aidha anailaumu kwa kuwawekea magogo ya minazi, micharalia, vyuma vya reli na mihimili ya magari mabovu badala ya madaraja kwa maana ya madaraja.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala hii umegundua kuwa huduma za mawasiliano ya barabara katika mkoa wa Morogoro zinatisha ukiacha barabara kuu za kutoka Morogoro kwenda Iringa na Dodoma, maeneo yaliyobaki hayana chochote zaidi ya 'vilami vya kuchombeza' na changarawe za kuombea kura nyakati za uchaguzi.
Uchunguzi unaonyesha kuwa tangu mwaka 1988 hadi hivi leo hakuna ujenzi wa barabara mpya au kukarabati vilivyo zilizopo. Mkoa ulikuwa na Kilomita 605 za barabara za kimataifa miaka kumi iliyopita., hali ambayo hadi hivi leo haijabadilika. Morogoro mjini na vijijini kimgawanyo zilibeba Kilomita 215, Kilosa Kilomita 238, Kilombero itambaliwa na Kilomita87 za "barabara ya kimataifa" na kilomita nyingine 65 zikatambaa juu ya ardhi ya Ulanga.
Kwa upande wa barabara za mkoa Morogoro ulibeba jumla ya kilomita 985 za barabara.
Wilaya za Morogoro mjini na vijijini zilikusanya 331 kilomita, Ulanga kilomita 212, Kilosa 215 na Kilombero kilomita 227, kwa barabara za wilaya za Morogoro mjini na vijijini zilikusanya kilomita 376 za barabara, Kilosa kilomita 377, Kilombero kilomita 163 na Ulanga kilomita 192 jumla ikiwa ni kilomita 1,108 kimkoa.
Na kwa barabara za vijijini ambako ndiko mazao ya wananchi yanapoozea mashambani kwa kukosa usafiri na hivyo kutopatikana masoko, mkoa ulibeba jumla ya kilomita 310 tu za barabara!!?
Kwa ujumla mkoa huo watatu kwa ukubwa nchini ulibeba jumla ya "vijikilomita" vya barabara 30008 tu; ambapo wilaya za Morogoro mjini na vijijini zilikusanya kilomita 1,232, Kilosa 830, Kilombero 477 na Ulanga 467.
Tukiangalia kwa undani suala la kilimo tunajiuliza tena suala jingine la msingi, je, Morogoro haina maeneo ya kutosha yanayofaa kwa Kilimo cha umwagiliaji maji? Swali hili linakuja kufuatia hoja za baadhi ya "watetezi" wa sera za serikali kuwa eti ukame nao umechangia kwa kiasi kikubwa kuwafanya wana Morogoro ambapo wengi wao ni wakulima wabaki katika dampo la ufukara uliopea.
Gazeti hli lilipopoiga hodi katika ofisi za Chama tawala (CCM) mkoa wa Morogoro limepata bahati ya "kunusa" taarifa za kazi za chama tangu Januari 1982 hadi Desemba 1985, ambapo suala hilo hapo juu linajibika kiurahisi, "Morogoro ina maeneo ya kutosha kwa ajili ya kilimo cha aina hiyo ambacho si tu kingelisha mkoa huu, bali eneo kubwa la Tanzania na ziada kuuzwa nje huku likituacha na akiba kubwa ya chakula katika maghala yetu. Si chini ya hekta 424,000 tu ardhi ya mkoa huu zinafaa kabisa kwa kilimo cha kiangazi".
Hadi mwishoni mwa mwaka 1985 ni eneo lisilopungua asilimia tatu tu ya hekta hizo ndizo zilizotumika kwa kilimo hicho! Na makisio yasiyoshaka yanaonyesha kuwa ni asilimia isiyozidi tano tu ndiyo inayotumika "kwa kusuasua" hivi leo! Jambo ambalo wapenda maendeleo wengi mkoani hapa wanaliona kuwa ni kichekesho cha "mahoka".
Maeneo husika, kwa Morogoro vijijini ni pamoja na Mgongoda palipotengwa hekta 10,000 ambapo hulimwa mpunga na mahindi. Na Mlali palipotengwa jumla ya hekta 160 kwa kilimo cha mboga mboga na mpunga ambapo hadi Desemba 1985 ni hekta 70 ambazo zilikuwa tayari zimekwisha shughulikiwa.
Huko Kilosa eneo la Manyenyele kumetengwa ekari 3000 kwa kilimo cha mahindi, mboga na mpunga, zaidi ya hekta 2000 tayari zimekwishashughulikiwa.
Hekta 500 zimetengwa huko Madato Kilosa kwa ajili ya mahindi na mpunga. Eeneo la Lumuma kumetengwa hekta 720 kwa kilimo cha migomba, maharage na mboga mboga kiujumla. Wakati Malolo kuna hekta 750 kwa ajili ya mahindi, ambapo hekta 540 kati ya hizo zimekwishafanyiwa kazi.
Wilayani Ulanga eneo la Itete (Mtimbira) kuna hekta 750 kwa ajili ya mpunga, mboga na mahindi. Sofi (majiji) kumetengwa ekari 1500 na kufanyiwa kazi hekta 80 tu katika kilimo cha mboga za majani, maharage, mpunga na mahindi.
Kilombero katika eneo la Kidatu kumetengwa hekta 500 kwa ajili ya mpunga na miwa. Chita na Kumemo kuna ekari 800 kila sehemu ambapo Chita hulimwa mpunga na mahindi, wakati Lumemo zaidi ya mazao hayo pia hulimwa maharage na migomba.
Kwa jumla mkoa umeandaa si chini ya hekta 19,780 na kuzifanyia kazi hekta 2,620 tu! Sasa kwa nini watu wasife njaa ukame unapopiga hodi? Majibu sahihi unayo.
Zaidi ya hapo kuna jumla ya maeneo kumi ndani ya mabonde makubwa manne yenye jumla ya hekta 424,790 yanayofaa kwa kilimo cha kiangazi mkoani Morogoro.
Mabonde hayo ni pamoja na bonde la mto Ruaha lenye jumla ya hekta 45,000. Hekta 15,000 zikiwa katika uwanda wa Kiberege na hekta 30,000 zilizobaki ni katika uwanda wa Msolwa na Kidatu.
Bonde la mto Kilombero lina jumla ya hekta 336,740. Hekta 146,940 zikiwa Lumemo, Ruipa, Kihanzi na Mgeta. Hekta 17,960 zikiwa Mchilipa, uwanda wa Lwasesa na Lur. Hekta 36,740 ni katika eneo la uwanda wa Sofi na Furuwe, huku Mpanga, Ruhiji na Mnyera likibea hekta 134,700.
Hekta 10,500 za kule Wami-Dakawa pamoja na hekta 15,600 za uwanda wa Mgondola na Mkindo zinajumuisha jumla ya hekta 26,100 za bonde lote la mto Wami ambalo ni eneo mojawapo muhimu "lililochuja hivi leo" kwa kilimo cha kiangazi Morogoro.
Bonde la mto Lumwengu pia ni eneo lingine linalofaa kwa kilimo hicho. Eneo hili linajumla ya hekta 26,950, hekta 10,450 zikiwa kwenye uwanda wa Chilombola na Ruaha, hekta 16,500 zipo Luhombero na Luwengu.
Ukiacha matatizo haya na yale, hadi mwaka 1988 mkoa ulivuna jumla ya tani 351,260 za mazao ya chakula ambayo ni mahindi tani 135,970. Mpunga tani 79,790, mtama tani 37,380 na Muhogo tani 98,120.
Kwa upande wa mazao ya biashara ulivuna tani 18,255 za pamba, kahawa tani 200 na alizeti tani 266, jumla ikiwa ni tani 21,115 tu! Sasa kwanini mkoa usiwe duni kiuchumi? Kawaida leo hii mavuno hayo yamekuwa kama wastani wa uvunaji kimkoa kila mwaka.
Itaendelea toleo lijalo
|
|