MAKALA
 
Jamaatul Kheir: Taasisi iliopo Tanga kumkwamua Muislamu
 

Na Faki A. Faki, Tanga
 

JAMAATUL Kheir al Alamiya ni taasisi ya Kiislamu iliyoanzishwa mjini Tanga katika miaka ya hivi karibuni. Kwa mujibu wa mmoja wa viongozi waandamizi wa taasisi hiyo Sheikh Said Mazrui ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya ofisi, amesema malengo makubwa ya taasisi hiyo ni kuwaendeleza Waislamu katika nyanja za elimu na uchumi.

"Matatizo makubwa yanayowakabili Waislamu wengi hivi sasa ni kupata elimu na nyenzo za kuwaendeleza kimaisha hivyo kwamba taasisi yetu imechukua majukumu ya kukabiliana na matatizo hayo", alieleza Sheikh Mazrui wakati wa mahojiano na gazeti hili hivi karibuni.

Katika kutekeleza malengo yake, taasisi hiyo ina kamati kadhaa zilizopewa majukumu mbalimbali. Kiongozi mkuu wa taasisi hiyo anayetambulikana kama Amir ni Sheikh Shauri Abubakar. Chini yake kuna kamati ya Maulamaa inayoundwa na Sheikh Shauri mwenyewe kama Mwenyekiti, Sheikh Abdallah Bawazir na Sheikh Ramadhani Idi.

Aidha, kuna bodi ya wadhamini ambayo Mwenyekiti wake ni Sheikh Abdallah Bawazir. Kamati ya utendaji ya taasisi hiyo inaongozwa na Abdallah Nasir kama Mwenyekiti. Makamu wake ni Yusuf Alawi, Katibu ni Mgambo Kombo na Mweka hazina ni Athman Jambai. Kamati nyingine ni kamati ya ofisi, kamati ya da'awa na kamati ya ujenzi.

Mwandishi wetu ambaye alitembelea makao ya taasisi hiyo alikuta madrasa na maktaba iliyokuwa na vitabu mbalimbali vya kidini. Kwa mujibu wa maelezo aliyopewa madrasa iliyopo inatoa mafunzo ya kuhifadhi Qur'an pamoja na huduma bure za vitabu.

Mbali na kuendesha madrasa hiyo, taasisi hiyo kupitia kamati zake mbalimbali imekuwa ikijishughulisha na kukarabati Misikiti na madrasa mbalimbali, kutoa futari kwa shule za sekondari katika mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wa Kiislamu pamoja na kutoa misaada ya hali na mali kwa walimu wa madrasa ndogo ndogo za mjini.

Hata hivyo, malengo makubwa ya taasisi hiyo yamekuwa ni kuwasaidia vijana wa Kiislamu kupata nafasi za masomo ya juu ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya ofisi Sheikh Said Mazrui, vijana kadhaa wameshasaidiwa na taasisi hiyo kupata nafasi za masomo ya juu kwa kugharamiwa vitu mbalimbali na taasisi hiyo.

Katika ukamilishaji wa malengo yake, taasisi pia ina mpango wa kuwatafutia vijana wa Kiislamu nafasi za masomo nje ya nchi, kujenga shule zake na pia kuanzisha shule za chekechea.

Mipango mingine ni kuwasaidia kiuchumi vijana wa Kiislamu wenye nia ya kujiendeleza kwa kuwapatia nyenzo na mitaji ilikuanzisha miradi ya kujitegemea. Mpango huu una nia ya kuwakwamua vijana wa Kiislamu kuchumi ili kuepuka kuwa ombaomba na wazururaji hali ambayo inawakosesha msimamo.

Taasisi hiyo pia inaangalia uwezekano wa kuwaendeleza kielimu walimu wa madrasa ndogo ndogo za mjini ambapo hivi sasa inao walimu kadhaa wa fani mbalimbali za elimu ya kidini.

Katika juhudi za kuendeleza Uislamu taasisi pia imekuwa ikitoa mihadhara mbalimbali ya kidini pamoja na kuendesha semina za mara kwa mara.

Kufuatana na maelezo yaliyotolewa na kiongozi huyo mwandamizi Sheikh Mazrui, huduma za taasisi ya Jamaatul Kheir zimekuwa zikisonga mbele pole pole kadiri wafadhili wanavyojitokeza kusaidia kwani hadi sasa taasisi hiyo imekuwa ikiendesa shughuli zake kwa kutegemea zaidi michango ya wanachama wake pamoja na moyo wa kujitolea ambao ndio uliofanikisha kwa kiasi kikubwa malengo ya taasisi ya Jamaatul Kheir.

Jamaatul Kheir al Alamiya ni miongoni mwa taasisi chache hapa nchini zilizoanzishwa na Waislamu ambazo zimeonyesha malengo yakinifu ya kumkwamua, kumkomboa na kumuendeleza Muislamu katika nyanja mbalimbali za maisha.

Baadhi ya Waislamu wa Manispaa ya Tanga waliohojiwa na gazeti hili wameielezea taasisi hii kama mkombozi anayepaswa kuendelezwa na Waislamu na kutoa wito kwa Waislamu wenye uwezo pamojana mashirika ya misaada ya Kiislamu kuisaidia taasisi hii ili iweze kutekeleza mipango yake kikamilifu.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook