Ndugu Mhariri
SISI waumini wa Msikiti wa Ibaadhi Tabora mjini tunaiomba serikali ya CCM kupitia gazeti lako la ANNUUR iache sera ya vitisho kwa Waislamu na viongozi wake. Hivyo tunaomba utupatie nafasi tuwaeleze wananchi vitisho hivyo.
Msikiti wetu huu upo karibu sana na soko, una idadi kubwa ya watu. Kutokana na hali hiyo hapa Msikitini kumekuwa na vikundi vya dini vingi ambavyo sehemu mkubwa hufanyia shura zao hapa.
Kutokana na kuwepo vikundi hivyo tumekuwa tunazushiwa mambo ya kila aina.
Mojawapo ya uzushi uliotupata hapa ni katika ziara ya Makamu wa Rais Dk. Omar Ali Juma aliposomewa risala na Madiwani wa Mjini ya kuwa baadhi ya Misikiti inagawa kadi za Chama cha Wananchi (CUF) na kuwa viongozi wa Msikiti ndio wanaogawa kadi hizo. Wakati huo ni uzushi na uongo mkubwa na wala Msikiti huu hauusiani na Chama chochote.
Hata kwenye ziara ya Alhaj Ali Hassan Mwinyi alidokezwa kuwa Misikiti hii miwili ya Ibaadhi na Msimbazi ni ya CUF asitembelee, lakini alikuja hapa Ibaadhi tu kwa sababu alikuwa hana Ratiba baada ya hapa ndipo akaja, lakini Msikiti wa Msimbazi hakwenda.
Suala ambalo limetufanya tuandike barua hii ni kule kuchukuliwa Imamu wetu Mkuu Sheikh Ahmed Saidi Khilla na Amiri wetu wa Mkoa Amiri Issa Haji na kushutumiwa vikali kuwa eti wao wanagawa kadi za CUF kwa waumini wake. Viongozi hao walitishwa na kuelezwa wataletewa polisi ili uzungukwe Msikiti na waumini tuwekwe ndani.
Vitisho hivyo dhidi ya viongozi wetu wa hapa Misikitini yaani Amiri wetu na Imamu wetu, kudhalilishwa mbele ya Mkuu wa Wilaya, ambaye pia ni Muislamu mwenzetu ndugu Mikidadi Ulaya pia na Afisa Usalama Bwana Haji wasizungumze lolote.
Kitendo hicho ambacho kilifanyika Juni 25, mwaka huu Ijumaa kimetuudhi sana sisi waumini wa Msikiti huu, kwani itikadi ya vyama ikitaka kupandikizwa kwa watu huwa ni sehemu za ibadatu, ni popote pale, sisi waumini tuna uamuzi wa kuchagua chama chochote kile chenye maslahi na sisi ya kidunia hata ya kiakhera, na tutazifuata kadi hizo kwenye ofisi zao wala hatulazimishwi kufuata chama chochote, sisi binafsi ndio waamuzi.
Tunaitaka serikali iache vitisho hivyo kabisa dhidi ya viongozi na sisi waumini.
Tunaawambia sisi tuko huru kuchagua chama chochote bila kulazimishwa na nguvu za dola wala mtu yeyote. Na watuwache tufanye ibada zetu bila kubughudhiwa kwa lolote.
Waumini wa Msikiti wa Ibaadhi,
P.O. Box 116,
Tabora.
Ndugu Mhariri
NAOMBA nafasi katika gazeti lako nipate kuwakosoa wale wote wanaosambaza propaganda ya udini dhidi ya vyama vya siasa vinavyohatarisha mustakabali wao.
Mimi huwa nakerwa sana nisikiapo kauli za kuinasibisha dini ya vyama vya siasa! Nijuavyo ni kwamba dini zinazoongozwa na maandiko matakatifu na vyama vya siasa na katiba yaani mawazo ya kibinadamu.
Aidha, malengo ya vyama vya siasa ni kushughulikia mambo ya kidunia tu wakati ambapo dini zinashughulikia mambo ya dunia na akhera.
Katika chama, hakuna sharti la kubatizwa au kusilimishwa. Mtu anaingia tu kwa kukata kadi. Lakini katika dini kuna masharti. Ama mtu abatizwe au asilimishwe, na zaidi ya hivyo afanye ibada.
Katika katiba za vyama vyote vya siasa, hakuna vipengee vya ibada kama vile sala, saumu, zaka, sadaka au hija ambavyo huitwa nguzo za dini.
Sasa kama katiba ya chama haina misingi hii, kuna mantiki gani kukiita chama hicho ni cha kidini? au kuna mantiki gani kukinasibisha chama na dini ya kiongozi wake?
Kisheria dai kama hilo linamtia hatiani msajili wa vyama. Yaani afikishwe mbele ya sheria kama kweli alipata kusajili chama cha kidini! Kwa upande mwingine na yeye kwanza anapaswa kukanusha hilo kupitia vyombo vya habari.
Na pili ana haki ya kumshitaki mtu yeyote hata kama ni kiongozi wa serikali, anaezusha dai hilo dhidi ya chama ambacho yeye kama msajili, alikisajili kwa misingi ya kisiasa kulingana na katiba ya chama husika.
Binafsi nawasihi wanapropaganda watafute mbinu nyngine lakini hii propaganda ya udini haina msingi wowote. Nina hakika kwamba wana CCM hivi sasa wanahaha kutafuta mbinu za kujinusuru na mweleka wa mwaka 2000 kutokana na madhambi waliyoyafanya.
Wahenga wamenena "usidharau wakunga uzazi ungalipo". Kosa kubwa la CCM ni lile la kuthamini kura badala ya wapiga kura. Umuhimu wa mpiga kura wao wanauona wakati wa uchaguzi tu.
Baada ya uchaguzi, mpiga kura hana maana tena kwao kiasi cha kumpiga risasi, mabomu ya kutoa machozi, kumtia gerezani, kumdhalilisha, kummwagia chakula chake cha biashara, kumzuia kufanya biashara zake, kumvunjia kibanda chake cha biashara, kumbomolea nyumba yake ya kuishi na kumpa machungu mengineyo.
Siamini kama mtu aliyefanyiwa hayo anaweza kumpa kura yake yule aliyeyafanya hayo hata kama muhanga na dhalimu huyo ni watu wa dini moja.
Kwa hali hiyo, CCM wasijaribu kuudanganya umma ambao sasa unaonyesha kutohadaika eti chama chao kinapingwa kwa sababu za kidini, la hasha, ukweli ni kwamba CCM inapingwa na wananchi kwa sababu ya udhalimu wake.
Isitoshe, waumini wa dini wakiwa kama raia wana haki ya kutumia kibali chao cha uraia kuchagua chama chochote cha siasa ambacho kwa mtazamo wao, wanaona kitawatendea haki sawa raia wote sambamba na kuwaletea maendeleo.
Ndio maana huko nyuma waumini wa dini ya Kiislamu waliviunga mkono vyama vya TAA na TANU na hata mtaliki wao CCM. Hivyo, kiungwana badala ya kuwashutumu waumini hao, viongozi wa CCM wanapaswa kuwashukuru sana Waisalmu kwa jinsi walivyoshiriki kukipigia kura chama hicho kwa wingi na kukiwezesha kudumu madarakani kwa karibu miongo minne sasa.
Jambo hilo linathibitisha uzalendo wa dhati wa Waislamu na linatupa ushahidi madhubuti kuwa viongozi wote wa nchi hii yaani Nyerere, Mwinyi na Mkapa walichaguliwa kwa misingi ya uraia au Utanzania na si kwa dini zao.
Halikadhalika, ikubalike pia kuwa, kwa msingi huo huo wa uraia au Utanzania, Waislamu wana haki ya kushirikiana na raia wenzao wa Tanzania kumpigia kura raia au Mtanzania yeyote mwenye haki na sifa za kutosha za uongozi, atokee, Ubungo, Temeke, Ilolanguru, Unguja, Pemba au mahala pengine popote mradi tu awe raia wa Tanzania na awe na tiketi ya chama chenye sera ya haki na usawa kwa wote, sio CCM. Kwa msingi huo isionekane ajabu wakimpa kura mgombea wa CUF.
Napenda kuwahimiza raia wote wapendao haki na maendeleo wasisikilize maneno ya uongo ya CCM na wala wasihadaike kwa propaganda za viongozi wa chama hicho zenye lengo la kuwalinda wachache waliopo madarakani ili waendelee kulihujumu taifa lenye rasilimali chungu nzima na lenye raia wavulimivu na wapendao amani.
Naomba Watanzania wote tushirikiane bega kwa bega kuing'oa CCM kwani sisi wapiga kurandio waajiri japo hatutahaminiwi. Hebu safari hii tuwaonyeshe na wao uchungu wa "lidandansi" kwa sababu hakuna wanachofanya zaidi ya kutuumiza na kutudhalilisha kitaifa na kimataifa.
Tuwapige vita washirika wote wa CCM wakiwemo madalali wanaopita kwenye majumba ya ibada.
Wakati wa ukombozi ni huu.
Salim S. Mohamed,
Jimbo la Temeke,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri
NAOMBA nafasi katika gazeti lako kuzungumzia mawaidha aliyoyatoa kiongozi wa Ansaar Sunnah Tanga katika ukumbi wa mikutano wa sekondari ya Thaqafa, Mwanza kwamba kupiga kura katika nchi hii ni ukafiri. Hiyo si sawa kabisakwa sababu hajatoa aya yeyote ya Qur'an wala hadithi ya Mtume, kwa sababu mwongozo wa Waislamu ni Qur'an na Hadith za Mtume (s.a.w.).
Napenda kumfahamisha kiongozi wa Ansaar Sunnah Tanga aelewe kwamba Waislamu wote wa Tanzania hivi sasa tuna majonzi makubwa sana ambayo hayajatufika kwa kuuawa Waislamu wenzetu kwa kupigwa risasi katika Msikiti wa Mwembechai.
Sasa kutokupiga kura kwa Waisalmu ina maana tunaona ni haki na sawa kwa haya tunayotendewa na kama si sawa basi suluhisho nikupiga kura ili kuwachagua viongozi watakaotutendea haki.
Kwani aelewe kwamba Mtume Muhammad (s.a.w.) amesema katika Hadithi yake: "Yeyote mwenye kuona miongoni mwenu jambo la munkar basi alizuie kwa mkono wake na akishindwa alizuie kwa ulimi wake na akishindwa alizuie kwa moyo wake, na huko kuzuia kwa moyo ni kudhaifu mkubwa wa imani".
Sasa ili Waislamu tuzuie jambo hili kwa mkono ni lazima tupige kura, na kama tusipopiga kura itakuwa tumezuia vipi au tukubali tuwe madhaifu wa imani?
Sasa napenda kuwafahamisha Waislamu wote nchini wapige kura ili tuwachague viongozi watakaotutendea haki kwa sababu waliopo madarakani hawatutendei haki, na bila kupiga kura hawatatoka madarakani na kamwe huwezi kutatua tatizo kwa kukimbia tatizo.
Pia Waislamu waelewe kwamba wapo watu miongoni mwa Waislamu unapokaribia uchaguzi hutumiwa na viongozi waliopo madarakani kuwalaghai Waislamu wasipige kura au wawachague viongozi hao hao (madhalimu) kwa manufaa yao, kwa hiyo Waislamu tuwaepuke watu hao ili kuwalinda Waislamu na Uislamu.
Vile vile watu waelewe kwamba Waisalmu tunachotaka ni haki itendeke kwa dini zote, tusikandamizwe na wakati huo huo kuwa na upendeleo ulio wazi kwa dini nyingine.
Maneno M. Ally,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri
MWANZONI mwa wiki ya pili ya mwezi Juni, 1999 nilipokea vitabu toka Jamhuri ya Switzerland.
Kwa vile hapakuwa na karatasi au barua yoyote ya maelezo na vile vile kwa kuwa sina yeyote ninayemfahamu huko nimeonelea nipitishe taarifa yangu hii ya shukrani katika gazeti letu tukufu AN-NUUR kwa matarajio kuwa huenda huyo mtumaji ni msomaji wa gazeti hili na kwamba yeye kanifahamu mimi kupitia kurasa za gazeti hili.
Ikiwa dhana yangu ni sahihi namuomb apokee shukrani hizi zangu za dhati kwa zawadi hiyo aliyonitumia na namuomba pia kuniandikia ili tufahamiane na kuweza kubadilishana mawazo.
Jihad R. Saballa,
Box 347,
Shinyanga.
--
|
|