KUTOKA MAGAZETI YA ZAMANI
 
Makaburu wadhibiti habari
Mzalendo, Jumapili, Novemba 3, 1985
 

JOHANNESBURG, Afrika Kusini
 

UTAWALA wa makaburu wa Afrika Kusini jana ulipiga marufuku vyombo vya habari kupiga picha na kutangaza habari za ghasia za Wazalendo ambazo zimeikumba Afrika Kusini kwa muda wa mwaka mmoja na miezi minane na kutangazwa katika magazeti ya dunia nzima pamoja na kwenye televisheni.

Waziri wa sheria wa makaburu Louis Le Grange alisema kuwa wapiga picha hawaruhusiwi kupiga picha za mapambano na migomo katika maeneo ambayo yamewekwa chini ya amri ya hali ya hatari isipokuwa tu kwa kibali maalum kutoka kwa polisi na kwamba waandishi wa habari hawaruhusiwi kuandika habari katika maeneo hayo. Hayo yalitangazwa katika gazeti la serikali lililotolewa jana.

Rais Peter Botha, ambaye serikali yake inavilaumu vyombo vya habari kwa kuandika habari zinazohusu ghasia nchini Afrika Kusini ambazo zimeifanya Afrika Kusini ishutumiwe na dunia nzima, Alhamisi iliyopita alivionya vyombo vya habari vya nchi za nje visiandike mabaya tu kuhusu Afrika Kusini.

Hatua hiyo ya Afrika Kusini ambayo itainyima dunia kufahamu unyama unaofanywa na polisi kwa wazalendo imechukuliwa wakati askari wa makaburu wamesambaa kwenye mitaa ya Johannesburg baada ya kuwepo na ghasia katika siku za hivi karibuni.

Waandishi wa habari kutoka nje ambao wamekuwa wakiandika habari kuhusu ghasia ambapo zaidi ya watu 800 wamekufa, wameshutumiwa na serikali ya Afrika Kusini kwa kile inachokiita upendeleo wakati wanapoandika habari zao.

Zaidi ya waandishi wa habari 170 kutoka nje wako Afrika Kusini wakati ambapo wengine zaidi wanazidi kuja kwa madhumuni ya kuandika habari za wimbi la mapambano nchini Afrika Kusini.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook