CHAKULA NA LISHE
 
Serikali ilipe madeni yake ili kunusuru maisha ya wananchi
 

Na Mujahid Mwinyimvua
 

AWALI ya yote napenda kuwaweka sawa wasomaji wa makala hii ya chakula la lishe, wanaoweza kuhoji mbona makala inaingilia siasa. Ni kweli usiopingika kuwa juhudi za lishe bora kwa wananchi haziwezi kufanikiwa endapo viongozi wa siasa (serikali) watatumia vibaya rasilimali za nchi au msaada unaotoka kwa wahisani. Ni kwa kulijua hili, lishe lazima ichanganywe na siasa.

Katika dhana nzima ya chakula na lishe, maji hasa ya kunywa yana nafasi ya pekee. Taaluma ya sayansi inatujulisha kuwa, binadamu anaweza kupitisha muda fulani bila ya chakula lakini muda huo huo hawezi kuupitisha bila ya maji mwilini mwake.

Katika nchi zenye serikali makini, swala la upatikanaji wa maji safi na salama huwa ni miongoni mwa agenda zao za awali kabisa. Na Rais wa nchi huwa hapati usingizi (hana raha) kama serikali yake inashindwa kuwapatia wananchi walioridhia awe Rais maji safi na salama.

Hii ni kwa sababu, ukosefu wa maji ya kutosha, na yaliyo safi na salama ni chanzo kikubwa cha maradhi ya tumbo katika nchi masikini kama Tanzania. Magonjwa kama vile kipindupindu (Cholera), homa ya matumbo (typhoid fever), kuharisha na kuumwa na tumbo huwa ndiyo mtindo wa maisha. Yaani magonja yanawakabili wananchi kila mwaka.

Si hivyo tu bali, magonjwa hayo huwa ni chanzo kikubwa cha vifo vya wananchi hasa wale wa daraja la chini. Ninasema wananchi, wa daraja la chini kwa sababu wale wa daraja la kwanza na lile la kati huwa wanamudu gharama za matibabu, na wengine (viongozi wa serikali) hupelekwa hasa Ulaya kwa matibabu. Kwa hiyo, idadi ya vifo (kwa sababu ya kipindupindu) kwa makundi hayo mawili huwa ni mdogo au haipo kabisa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, kuanzia Januari mpaka Agosti, 1998, watu elfu moja (1000) walifariki nchini kutokana na ugonjwa wa kipindupindu. Hatujuwi waliokufa kuanzia Septemba, 1998 mpaka leo Alhamis (wakati gazeti hili linakwenda mitamboni. Ni vyema tuwaombe Wabunge waliulize hilo na sisi tuweze kupata takwimu hizo ili tuweke rekodi kwa ajili ya kizazi cha kesho na manufaa mengine kwa ujumla.

Wataalam wa afya wanatuambia kuwa, ugonjwa wa kipindupindu unasababishwa zaidi na ukosefu wa maji ya kutosha na yale yaliyo safi na salama.

Katika kero zinazowakabili Watanzania wakati dunia inakaribia kuingia karne mpya ya 21, ya sayansi na teknolojia, ni ukosefu wa maji ya kutosha na yaliyo safi na salama. Bila ya kwenda mbali (vijijini), hali ya maji katika Jiji la Dar es Salaam ambapo Ikulu ipo ni ya kusikitisha. Kuna maeneo watu hawapati kabisa maji ya bomba. Miji mingine kama Mwanza, Morogoro n.k., ukipewa maji ya kunywa hayawezi kupita kinywani hasa kwa wale wanaotazamwa afya zao Ulaya na Marekani.

Licha ya hali hiyo ya kutisha, serikali haionyeshi nia ya kuondoa kero hiyo katika siku za hivi karibuni. Ninasema hivi kwa sababu, matumizi ya serikali kuu katika mambo yaliyo nje na huduma za jamii yanatisha. Na huku serikali hiyo hiyo inadaiwa mamilioni ya shilingi na mamlaka mbalimbali za maji taka na safi.

Kwa mfano, serikali imetenga kutumia shilingi bilioni 3 kwa ajili ya kuikarabati Ikulu, na shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya nyumba ya Waziri Mkuu. Wakati fedha hizo zimeanza kutumika, Mwalimu Nyerere amependekeza ofisi nyeti zikiwemo ya Rais (Ikulu) na Waziri Mkuu zianze kuhamia Dodoma. Na sote tunajua nafasi ya Rais Mstaafu, Mwalimu Nyerere, katika siasa ya Tanzania.

Lakini hayo yote afadhali ukilinganisha na utumiaji huo wa fedha za umma na serikali, wakati serikali hiyo inamadeni kama nilivyokwisha kusema. Mwezi Juni, mwaka huu, vyombo vya habari vilimripoti Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Taka na Safi wa Mkoa wa Mwanza akisema kuwa Mamlaka yake inazidai taasisi na serikali, shilingi milioni 580 na kwamba hadi kufikia Aprili, mwaka huu, serikali imeweza kulipa sh. milioni 50 kati ya sh. milioni 280 inazodaiwa.

Mkurugenzi huyo, Bwana Zephania Mihayo alikaririwa akisema kuwa, maji kiasi cha asilimia 50 kinapotea kila siku na kusababisha hasara ya shilingi milioni 1.5, na hivyo huduma ya maji kwa wateja inazorota na Mamlaka iko katika hali ngumu. Uchafu wa mabomba ni moja ya sababu zinazochangia upotevu huo wa maji kwa asilimia 50 kila siku.

Kama serikali ingelipa deni lake lililobaki, shilingi milioni 230 mamlaka ya maji taka na safi ingeweza kununua mabomba mapya kadhaa na kuweza kuboresha huduma hiyo ya maji, na hatimaye wangeweza kuokoa maradhi, vifo na usumbufu kwa wananchi wa Mwanza. Lakini wapi!

Serikali yetu ya awamu ya tatu inajisifu kwa kukusanya kodi na haina 'simile' na watu wasiotaka au wanaochelewa kulipa kodi. Sasa asietaka kulipa deni kwa huduma aliyofanyiwa huyu nae nini hukumu yake? Serikali ilipe madeni yake ili kunusuru maisha ya wananchi.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook