KAMA ulikuwepo utata au fujo katika uchaguzi mdogo wa Ubunge Temeke na Ubungo basi fujo hiyo ilikuwa ni kuchelewesha kutangazwa matokeo ya kura tena matangazo yenyewe yakasubiri watu washalala. Na watu wamekuwa wakihoji; je; kuchelewesha kutangaza matokeo ndio ilisababisha kujazwa polisi wa kawaida wenye mbwa na wale wa FFU? Na je hali hii si ingeipa nguvu dhana ya wale wanaohoji matokeo?
Bado wananchi wamekuwa wakiendelea kuhoji mantiki ya kujaza polisi vituoni wakati zoezi lenyewe lilikuwa shwari. Je, hawa polisi walikuja kuwazuia hao ambao hawakupiga kura? Na kama ndio hivyo hizo nyingi ambazo watu wengine walikuja kukataa kuzisaini zimetoka wapi?
Lakini pamoja na maswali hayo watu wanahoji mantiki ya baadhi ya viongozi wa CCM kudai kabla ya uchaguzi kwamba wembe uliotumika Zanzibar wakati wa uchaguzi Mkuu 1995 ndio ungetumika katika uchaguzi wa Temeke na Ubungo. Lakini mbinu au wembe uliotumika Zanzibar 1995 ulimleta Anyauko. Je; ilitakiwa aje tena Anyauko kwa uchaguzi huu wa Temeke na Ubungo?
Yapo mambo mengi waliyojifunza wananchi lakini yapo pia mambo mengi yaliyowatatiza na wakabaki bila ya maelezo wala majibu.
Kampeni ziliposhamiri mkuu wa wilaya ya Kinondoni ambaye pia ana nafasi maalum katika CCM aliibuka na kutoa shutuma kali dhidi ya baadhi ya vyama.
Kabla na baada ya kauli za Mkuu huyo wa wilaya wa wilaya; wananchi hawakupata kusikia kauli ya Tume ikionya juu ya kuwepo ukiukwaji wa taratibu za kampeni za uchaguzi.
Mkuuwa Mkoa naye alifuata nyayo za Mkuu wa Wilaya na Waziri Mkuu kulidaka akiwa Bungeni. Wote hawa wakiwa ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM walitumia majoho yao ya serikali kukemea shughuli za vyama vingine na kuamrisha vyombo vya dola viwashughulikie. Wakati wote huo Tume ya uchaguzi kimya utadhani imekasimu madaraka yake kwa serikali, polisi au CCM.
Wakati hayo yakiwashangaza wananchi, Katibu Mkuu wa CCM akaibuka na kuleta tuhuma nzito ya kosa la Jinai kwamba baadhi ya watu wanahongwa ili kuharibu taratibu za uchaguzi.
Tume ya Uchaguzi kimya wala haikuona haja ya kuhoji ushahidi wa tuhuma nzito kama hii. Wakati ikiendelea na kimya chake akaibuka kiongozi mwingine wa CCM na kudai kwamba kaagizwa na Chama chake autangazie uma kuwa wafurukutwa wa vyama vingine wacharazwe bakora na pasiwe na hofu katika kulitekeleza hilo kwani wao ndio wenye mamlaka na polisi.
Agizo hilo lilitolewa huku yakitolewa maelezo kuwa hiyo ilikuwa ishara ya kuanza kwa "sera za kihuni dhidi ya vyama vingine".
Tume iliendelea kupiga kimya na hivyo kuzidi kusitawisha dhana kwamba huenda Tume ya Uchaguzi imekasimu madaraka yake kwa CCM na serikali yake.
Yapo madai kuwa wakati wa zoezi la upigaji kura watu kadhaa walikamatwa ama wakiwa na shahada za wizi au waliodai kupewa fedha wakapige kura katika maeneo ambayo si yao na kwa shahada ambazo si zao. Mahali pengine wasimamizi walikataa kuhesabu kura katika vituo kwa visingizio kadhaa. Mahali pengine zilihesabiwa pale baadhi ya viongozi wa vyama walipofika na kuileta kashi kashi.
Matukio kama hayo yameelezwa kutokea maeneo ya Vituka, Mwembechai; Goba na Ubungo.
Katika madai hayo imeelezwa kuwa watu waliokamatwa waliripotiwa kwa wasimamizi wakuu wa vituo pamoja na polisi waliokuwepo. Lakini wahusika hawakuwekwa ndani. Wananchi wameshindwa kuelewa kwamba je haya ni matokeo ya ile kauli ya CCM kwamba wao ndio wenye serikali na polisi au vipi.
Hayo yote yamedaiwa kujiri wakati toka awali baadhi ya vyama vilishaiandikia Tume ya Uchaguzi vikilalamikia mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kupora mamlaka ya Tume na ishara za kuwepo wapiga kura wasio halali na mambo mengine ya kuvuruga haki katika uchaguzi huo.
Toka uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 chaguzi ndogo nyingi zimefanyika ambazo zimewagharimu walipa kodi mamia ya mamilioni ya shilingi. Na nyingi ya chaguzi hizo zimetokana na kutenguliwa matokeo ya uchaguzi kutokana na dosari katika uchaguzi wa awali. Pengine dosari hizo ni matokeo ya hali hii inayoashiria Tume kutokuwa makini katika majukumu yake.
Na hapana shaka dosari hiyo si ya kupuuzwa ikikumbukwa kwamba mwaka 1995 mita kadhaa tu kutoka zilipo ofisi za Tume Dar es Sala watu walikosa vifaa vya kupigia kura.
Lakufurahisha katika uchaguzi
huu ni kuwa pamoja na vitisho vyote vya serikali na vyombo vya dola wananchi
walijitokeza kwa wingi na kupiga kura zao. Hata hivyo wamebaki wakijiuliza
je, Tume hii ndiyo watakayoingia nayo kwenye uchaguzi wa 2000?
--
|
|