APRILI 26-30, 1999 ulifanyika
mkutano wa Kimataifa nchini Uingereza uliopewa anuwani Uingereza na Uislamu.
Kutoka Tanzania walihudhuria Mabwana Issa Mnenge na Ismail Abdullah. Fuatana
na Bwana ISMAIL ABDULLAH katika makala hii uelewe lengo na yatokanayo na
mkutano huo.
Lugha ya Kiingereza
HATA hivyo, lugha ya Kiingereza, imejionyesha kujipenyeza na kuchukua nafasi kubwa na pana katika elimu ya Kiislamu, kwa ushahidi uliokuwa wazi, katika maonyesho ya vitabu vya Kiislamu uliokuwa umeandaliwa hapo mkutanoni.
Na pia mtu yeyote alietembelea duka la vitabu au maktaba ya Msikiti Mkuu wa London ulioko "Park Rd" angeona kwa wingi vitabu vya Kiislamu vilivyo tafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza kuanzia Qur'an na si ile tulio zoea sana huku kwetu ya Yusuf Ali tu pia za hivi karibuni zilizotafsiriwa kwa Kiingereza na mabingwa kama Dr. Muhammad Taqi na Dr. Muhammad Muhsin Khan wa Chuo Kikuu cha Kiislamu Madina.
Huyu Dr. Muhammad Muhsin Khan wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Madina ndiye yule yule aliye tafsiri Sahih Al Bukhari Juzuu tisa kwa Kiingereza.
Na kitabu maarufu cha Fiqii cha Yusuf Al Qaradawi kutoka Islamic Culture ya Al-Azhar University.
Hii ni mifano michache ya waandishi wa nje ya Uingereza yenyewe. Ndani ya Uingereza vitabu ni vingi sana, tunaweza kuzungumzia maelfu, na ni fani malimbali, ambazo zimeandikwa au kutafsiriwa kwa Kiingereza na waandishi wa Kiislamu nchini Uingereza. Maduka makubwa ya vitabu vya Kiislamu ni mengi mno nchini Uingereza zaidi ya thelathini.
Wapo wachapishaji wa vitabu na magazeti ya Kiislamu kadhaa nchin Uingereza, kuna magazeti manne ya Kiarabu na ni ya kila siku. Kuna televisheni nne za Kiarabu mjini London tu.
Baada ya kuona jinsi lugha ya Kiingereza inavyojipenyeza na jinsi inavyozidi kuchukua nafasi kubwa kwenye Uislamu, sio kwenye vitabu tu, bali na hata kwenye mikutano mikuu ya kimataifa inayowakusanya Waislamu, kutoka nchi mbalimbali na bara mbalimbali, sasa tumalizie kwa kuitazama jamii ya Kiislamu inayoishi nchini Uingereza, ambayo kwa jina maarufu inajulikana kama "British Muslims".
Jamii ya Waislamu Waingereza
Nchini Uingereza ipo jamii ya Kiislamu yenye Waislamu wanaokaribia milioni mbili kwa idadi yao.
Miongoni mwao, asilimia thalathini na saba (37%) ni waliozaliwa humo humo nchini Uingereza, wazazi wao, wote wawili au mmojawapo akiwa ni muhamiaji.
Hawa ni mabalozi wa Waislamu waliotapakaa duniani kote na ndio kioo kinachoweza kutupa picha nzuri, ni upi mtizamo wa Waingereza kwa Waislamu na Uislamu.
Unapotembelea mjini London siku ya kwanza utakachogundua, uwe ndani ya treni, au basi au kwa miguu, ni mchanganyiko mkubwa wa watu wa mataifa yote, Mchina, Mhindi, Mwafrika na kadhalika watu wa rangi zote, nyeusi, nyeupe, mchanganyiko na kadhalika.
Ebu tujiulize ni sumaku gani ambayo imewavuta na kuwanasa watu wote hawa? Wallahi! Hata wewe na mimi tukienda hatutapenda kuondoka.
Sababu kuu, pamoja na sababu zingine, ni kwa sababu ya uhuru unaojisikia kuwa nao nchini Uingereza.
Na hii pia ndio sumaku iliyowavuta Waislamu wanaoishi Uingereza kuondoka nchi zao na kuhamia Uingereza, hususan kuanzia miaka ya 1950.
Lakini kwa upande mwingine, kwa Mwingereza kabla ya hapo Uislamu au Waislamu ulikuwa ni nadharia tu, ni watu waliokuwa kwenye makoloni yao tu, lakini leo Waislamu ni Waingereza.
Mfumo wa serikali ya Kiingereza na taratibu zao zililalia moja kwa moja kwenye Ukristo. Kwa sababu Waislamu hawakuwepo.
Ndugu msomaji kumbuka kuwa Uingereza iliingia katika Ukristo kwa sababu za kimsingi na hebu tuone kisa hiki kifupi.
Inasemekana kuwa Mfalme Edwin wa Uingereza zama za 627 AD aliwaita washauri wake wenye hekima, wamshauri iwapo aingize nchi katika dini mpya ya Kikristo.
Akasema mzee mwenye hekima kumshauri mfalme kuwa, maisha ya mwanadamu ni sawa sawa na ndege aliyeingia katika ukumbi wenye joto zuri na watu wamo ndani kwenye sherehe na huko alikotoka ni giza na baridi kali. Basi yule ndege akaruka ruka ndani ya ukumbi hapa na pale baadaye akaamua kutoka nje na kupotelea mbali pasipo julikana.
Na maisha ya mwanadamu ni vivyo hivyo. Mtu anakuja duniani na hatujui atokako na huondoka duniani hatujui aendako.
Basi ikiwa dini hii itatufundisha mafumbo hayo mawili ya; tulipotoka na tutakapokwenda, basi na tuipokee.
Mfalme Edwin akafurahi kwa ushauri wenye hekima, na Uingereza ikaupokea Ukristo. Kwa misingi hiyo. Na jamii ya Kikristo ikazaliwa na kukua mpaka leo, ambapo wanaanza kujiwa na wenzao Waislamu.
Kwa bahati nzuri haupingani na misingi hii na kwa uhakika Uislamu nayo pia, mafundisho yake yanatosheleza majibu ya mafumbo hayo mawili.
Kwa hiyo kimsingi hatuna utata, ila tofauti inatokana na jinsi ya kufikia malengo.
Lakini kwa vile Uislamu ni kitu kipya kwa wengi, na wengi wanaijua kwa sura mbaya na upotofu uliozuliwa ya ugaidi, basi lazima patakuwa na msuguano kwa kipindi hiki.
Katika hotuba maarufu ile ya Prince Charles alisema kwamba Waingereza kuhusu msuguano huu( 27th Oct. 1993)
"It was depressing that despite the advances in technology... mass travel the intermingling of races, the ever-growing reduction or so we believe-of the mysteries of our world, misunderstandings between Islam and the West continue. Indeed they may be growing. As far as the west is concerned, this cannot be because of ignorance.
There are one billion Muslims world wide. Manye millions of them live in contries of the commonwealth. Ten million or more live in the west, and around one million in Britain.
Our Islamic ocmmunity has been growing and flourishing for decades. There are nearly 500 Mosques in Britain, Popular interest in Islamic Culture in Britain is growing fast. Many of you will recall the wonderful festival of Islam which Her Majesty the Queen opened in 1976. Islam is all around us, and yet distrust, even fear persity"...
"In many ways it was odd that misunderstandings between Islam and the west should persist. For that wich binds our two worlds together is so much more powerful than that which divides us. Muslims, Christians and Jews are all "Peoples of the Book" Islam and Christinanity share a common monotheistic vision. A belief in one Divine God, in the transience of our earthly life, in our accontability for our actions, and in the assurance of life to come"...
Tafsiri
"Ilikuwa inasikitisha kuwa licha ya maendeleo ya teknolojia, usafiri, kuchanganyika kijamii mbalimbali, kutoelewana kati ya Uislamu na nchi za magharibi inazidi kukua. Ama kwa nchi za magharibi, sababu haiwezikuwa ni ujinga. Kuna Waislamu bilioni ulimwenguni. Milioni yao wanaishi nchi za Jumuiya ya Madola. Milioni kumi au zaidi wanaishi nchi za magharibi na wapatao milioni moja wanaishi Uingereza.
Jamii yetu ya Waislamu (nchini Uingereza) imeendelea kukua na inaendelea kuchanua kwa ..
Kuna karibu misikiti ipatayo 500 Uingereza, na hamu ya kujua utamaduni wa Kiislamu nchini Uingereza unazidi kukua tena kwa upesi.
Wengi wenu mtakumbuka tamasha zuri la kupendeza la Kiislamu lililofunguliwa na Malkia mwaka 1976. Uislamu upo pamoja nasi umetuzunguka. Hata hvyo kutoaminiana na hata kuogopana bado kupo. Kwa sababu nyingi sana inashangaza kuwa kutoelewana Waislamu na nchi za magharibi bado kupo. Kwani kinachounganisha nchi zetu mbili hizi kina nguvu zaidi kuliko kinachotutenganisha. Waislamu, Wakristo na Mayahudi wote ni watu wa kitabu. Uislamu na Ukristo wote wana uona wa Mungu mmoja, imani ya Mungu mmoja, imani katika maisha ya kupita, uwajibikaji wa vitendo vyote (kesho akhera) na uhakika wa maisha ya akhera"...
Ebu sasa tuitizame Uingereza nyumbani kwake, na wageni wake wa kudumu, yaani Waislamu wa Uingereza. Kuna misemo miwili ambayo katika nukta hii itabidi tuzitafakari, ya kwanza ni pale Muingereza anaposema "Charity begins at home". Tafsiri: "Wema huanzia nyumbani". Kwa hiyo dhamira ya Muingereza katika dhana ya mshikamano "Mutuality", kioo kizuri kama tulivyokwisha sema ni jinsi anavyoishi na Waislamu wa nyumbani kwake kwanza.
La pili, ni somo tunalopata sisi sote kutoka kwa Muingereza, kulingana na dunia ya sasa, kuwa dunia ni kijiji kimoja tu, chenye tamaduni mbalimbali, mila mbalimbali, dini mbalimbali. Kwa hiyo ikiwa dunia, hivyo ndivyo ilivyo, sasa ni kijiji tu, sembuse hiyo London au Uingereza kwa jumla.
Hapa ndio ule msemo wa hivi sasa "Devesify or you Die". Tafsiri inaweza kuwa: "Kubali mabadiliko au utakufilia mbali".
|
|