MAKALA
 
Kukabana sisi kwa sisi, nao ni ukoloni!
 

IKIWA una sarafu ya shilingi mia moja mkononi, bila shaka utakubaliana nami kuwa sarafu hiyo ina pande mbili zinazotofautiana kisura. Kuwepo kwa sura mbili tofauti hakufanyi sarafu hiyo kuwa mbili au tatu. Itabaki kuwa sarafu ya shilingi mia moja ile ile; na kukiwa na mabadiliko basi uwezekano wa badiliko la kushuka thamani ndilo litakalochukua nafasi ya awali kuliko lile la kuongezeka thamani. Mikonzi wa Mikonzi anaelezea zaidi.

LIKITAJWA neno ukoloni, taswira inayojitokeza vichwani mwa watu wengi miongoni mwetu ni ile ya utawala wa Kizungu uliotoka Ulaya na kuja kuzipora haki za binadamu walioishi Afrika, kwa kupitia utangulizi wa wana dini wa Kikristo (Missionaries), wapelelezi wao na makampuni yao ya kibiashara. Ndiyo taswira ya haraka inayojidhihirisha.

Ningependa kukiri kuwa taswira hiyo inayojitokeza vichwani mwetu kuwa si ya uongo, isipokuwa inaoupungufu kutokana na ukweli kwamba sarafu ina pande mbili zinazokamilishana. Kutokana na usingizi huo bado nitakuwa nipo katika mstari nikisema kwamba ipo taswira nyingine inayouwakilisha upande mwingine wa ukoloni uliosimikwa na Wazungu.

Unaweza ukajenga hisia kuwa kalamu yangu imeamua kuuweka utata usiohitajika katika jambo ambalo ukweli wake uko dhahiri shahiri katika mtazamo wa kihistoria, kwamba ukiondoa ule ukoloni wa zamani, huu unaendelea sasa ni ule wa kimamboleo; bado huu ni upande mmoja wa sarafu ambayo ukiigeuza upande wa pili, macho yako yatatua katika sura ya ukoloni wa sisi kwa sisi.

Sidhani kama utashindwa kuniunga mkono kuwa laiti wale Wazungu waliovamia ardhi yetu wangelisimamisha utawala uliozingatia haki na uadilifu kwa kutowadhalilisha na kuwanyonya waliowakuta, neno ukoloni lisingelibeba maana ile inayoendelea kufundishwa mashuleni kupitia mitaala itumikayo, na wala uwepo wa utawala wa kikoloni usingesababisha kuibuka kwa harakati za ukombozi zilizoutingisha na kuung'oa.

Kama ingelikuwa hivyo, basi bila ya kinyongo wala pingamizi la aina yoyote ile utawala huo ungelikumbatiwa kwa kutumikiwa, ukashamiri na kustawi ili matunda yake yaliyomaruzi yapate kudumu na kurisishwa kizazi hadi kizazi nao waishi katika mfumo wa haki, usawa, upendo na kuhurumiana, amani na usalama vinavyopatikana ndani ya ukoloni.

Ni kweli kwamba ukoloni sio uzungu wala uzungu siyo ukoloni, bali ni utaratibu wa maisha uliojengwa katika misingi ya dhulma, unyonyaji, uonezi, ukandamizaji kutokana na sera na sheria za kibaguzi na kubaguana. Kutokana na ukweli huu yatupasa kutafakari kwa jicho la ndani ili tuweze kujenga jamii ya watu walioshibana katika misingi ya kutendewa haki na uadilifu ambapo kila mtu anaheshimu na kulinda haki.

Tutake tusitake ni lazima tukubali kuwa kiini cha mzizi wa fitna uliozua mtafaruku na kupelekea kuasisiwa kwa harakati za ukombozi zilizopinga na kuung'oa ukoloni si kingine bali ni ile dhulma na ukandamizaji, uonevu na unyanyasaji waliofanyiwa wananchi chini ya utawala wa kikoloni. Kwa makusudi kabisa wananchi walidhikishwa na kudhalilika ndani ya nchi yao na wakoloni waliona kuwa hiyo ndiyo stahiki ya wanaotawaliwa.

Mfumo wa elimu na mgawanyo wa madaraka ulijengwa katika umbile la mithili ya chupa ya soda, ambayo ni nyembamba kwa upande wa kichwani kuliko ile sehemu ya upande wa chini. Ili tuweze kwenda pamoja ningependa kila mmoja wetu azielekeze fikra zake kwenye chupa ya soda na ajaalie kuwa mikononi mwake ana chupa hiyo ikiwa haina kitu ndani yake.

Haya! Natuanze kwa kuisimamisha chupa yetu ikae kwa kutumia makalio yake. Mkao huu unatupa tafsiri gani kwa munasaba wa makala tunayokwenda nayo? Nakuna mahusiano yepi na ile sarafu yenye sura mbili kwa maana ya ukoloni ule na huu wa sisi kwa sisi?

Katika mkao huo, sehemu iliyonenepa ya chupa inawakilisha kundi kubwa la wananchi waliokuwa chini ya ukoloni ambao ulifaradhishwa kwao kuwa ni wajibu wao kulipa kodi zote walizowekewa katika hali yoyote iwayo, ima ya kujiweza au ya taabani hohehahe. Kodi ya kichwa, ya maendeleo, ya mazao, ya kibanda (land tax), mamilioni ya pesa yalikusanywa na kuingizwa kwenye hazina ya dola.

Aidha, sehemu hii iliyonenepa inawakilisha wananchi waliobanwa katika haki yao ya kielimu iliyo ya msingi kwa kila mwanadamu akiwa miongoni mwa wanajamii. Ni hakika isiyopingika kuwa utawala wa kikoloni uliona ni jambo la anasa lisilo na manufaa kwa upande wake ikiwa itachukua jitihada za makusudi za kutumia sehemu ya kodi katika kukipa kizazi cha wananchi elimu iliyowiana na ile iliyotolewa kwa kizazi cha wakoloni.

Kutokana na mfumo huo wa kibaguzi wananchi walinyongeshwa na kusukumwa kuwa vibarua waliotumikishwa kama vifaa vya uzalishaji na kulipwa ujira usiolingana na hali ya kimaisha pamoja na zile sulubu walizopewa. Umati huu wa wananchi haukuwa na nafasi nyingine zaidi ya kuwa vibarua wa bei poa (cheap labour) katika mashamba ya mikonge pamoja na kupokea vijisenti ambavyo kodi haikuvipitia mbali. Kwa kifupi walizungushiwa wigo wa seng'enge/senyenge ya umaskini na ukosefu wa elimu.

Tukiendelea kuitazama chupa yetu ikiwa katika mkao huo huo wa awali, ile sehemu ya juu iliyokondeana inawakilisha huduma za kimsingi za kijamii zilizotolewa na utawala wa kikoloni kwa wananchi. Wakati ukusanyaji wa kodi ukifanikishwa kwa kuwasaka watu nyumba hadi nyumba, ilikuwa ni lazima mgonjwa kupelekwa maili nyingi ili akapatiwe huduma kwenye hospitali ya Kanisa.

Ukusanyaji wa kodi haukuzingatia dini za wananchi lakini mazingira ya kupewa fursa katika masomo yalijengwa katika namna ambayo ni kijana wa mlipa kodi aingie "middle school" ilimlazimu kubadili dini au endelee kuwa mbumbumbu huku akiwa kwenye dini yake. Haya yote hayakutendeka kwa bahati nasibu ukizingatia kuwa wana dini wa Kikristo (Missionaries) ndio waliokuwa miongoni mwa wapambe waliopigia debe ujio wa ukoloni. Hivyo utawala wa kikoloni kwa upande wake 'haukufanya kosa' ulipojivua jukumu la kutoa elimu kwa wananchi bila ya ubaguzi.

Hebu na tujiulize kwa pamoja kuwa ni sababu zipi za kimsingi zilizowasukuma wenzetu waliotutangulia mpaka wakafikia kuanzisha harakati za ukombozi dhidi ya ukoloni. Je! Ni kwa kuwa wazungu walitoka makwao wakaja kwetu na kuweka utawala wao? Je! Ni kwa sababu ya tofauti za rangi baina yao na wananchi au tofauti ya kidini?

Naam! Ni vyema tukiigeuza chupa ili tupate tafsiri nyingine. Ipindue chupa yetu ya soda ikae chini juu, juu chini. Katika mkao huo sehemu ya chini iliyosinyaa inawakilisha wananchi wachache miongoni mwa maelfu ambao walipewa elimu ya kiwango cha chini sana ili waweze kuwa wasimamizi watukufu wa kuzitekeleza sera za kuuimarisha ukoloni.

Sambamba na hilo, taawili nyingine inayojidhihirisha kutoka kwenye mkao mpya wa chupa ni kwamba katika nafasi nyingi kubwa za madaraka ya juu muhimu yahusuyo maongozi ya nchi, wananchi walipewa nafasi finyu na ya chini ambayo jukumu lao ni kuinamisha vichwa kila walipopewa amri kwao wao ni ksuema "sawa bwana mkubwa". Kwa maneno mengine hakukua na mtu miongoni mwa hao wachache waliokuwa na nafasi pamoja na ubavu wa kuwasemea wananchi haki zao mbele ya ukoloni na kupewa ufumbuzi stahiki.

Ukiangalia hiyo chupa kwa makini na kuutafakari huo mkao wake, utagundua kuwa unafafanua jambo moja la kweli kuhusiana na utaratibu wa kibaguzi katika ukoloni. Ni kwamba kijisehemu kidogo cha chini kisichonenepa kinawakilisha wakoloni na kizazi chao wakati ambapo sehemu iliyonenepa inawakilisha fursa pamoja na huduma mbalimbali walizojipendelea. Uwiano baina ya sehemu hizo mbili unaonyesha ni kwa kiango gani jamii ya watawala walivyojipa ubinadamu zaidi ya wale wanaowatawala.

Nasema tena kuwa kama wazungu waliovamia ardhi yetu wangelisimamisha utawala wa haki na uadilifu usiokuwa wa kujipa upendeleo wa wao kujiona ni binadamu zaidi kuliko wananchi, basi ukoloni usingelikuwa wenye kuchukiwa wala haja ya kuanzishwa kwa harakati dhidi yake isingelikuwa na maana. Dhulma ndiyo tatizo lililotengeneza madukuduku na mafundo mioyoni mwa wananchi wakakereketwa kikweli kweli na kuyahamisha madukuduku yao kwenye matendo

Itaendelea toleo lijalo
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook