Na Bisura Nyello
KIPINDI cha WDTV Jounal kinachotayarishwa na TRANSTEL kilichorushwa hewani siku ya Juni 11, 1999, Ijumaa, kati ya saa 12.30 na saa 1.00 jioni na ITV2 kimewavunjia heshima kinamama kwa kiwango cha juu sana. Kimedhalilisha utu katika kikomo cha udhalilifu!
Kipindi hiki kilikuwa na maudhui nzuri tu ya kuelimisha ulimwengu juu ya matatizo na majanga ya uzazi yanayowakumba wanawake wa nchi zinazoendelea. Yaani Afrika, Asia na Latin Amerika.
Ijumaa ya Juni 11, mwaka huu, kipindi hiki maalum kilizungumzia matatizo ya wanawake wa Kiafrika wanaoishi vijijini. Na dira yao ilikuwa wanawake wa Zimbabwe vijijini.
Jambo la kuhuzunisha na linalochoma moyo ni picha zilizokuwa zikirushwa za mwanamke mzazi wa Kiafrika. Mwanamke huyo ameoneshwa tangu alipoanza kushikwa na uchungu mpaka alipomaliza kujifungua kitoto.
Picha zilipigwa katika pembe zote mpaka kwenye njia ya uzazi na namna mtoto anavyotolewa na wakunga wa jadi kutoka tumbo la uzazi la mama yake. Hakukuwa na stara yoyote wala pazia! Ilikuwa ni mandhari ya kutisha sana na isiyotegemewa!
Nikiwa kama mwanamke na mzazi kwa kweli nilijisikia vibaya sana. Huwezi kumdhalilisha mwanamke zaidi ya kuonesha aibu zake za kike kwenye vioo vya 'Televisheni' kwa ajili ya hadhira za kimataifa. Mambo ya uzazi yana adabu zake na namna yake ya kuyafikisha kwa jamii. Si adabu hata kidogo kuonesha mambo mazito kama haya kwenye TV kirahisi tu kama mechi za Manchester na Arsenal!
Tatizo haliko katika mafundisho ya kipindi bali picha zilizoambatana na mafundisho ya kipindi hazikubaliki kwa jamii yetu. Jamii ya Kitanzania haiko tayari kushuhudia tendo la mwanamke kujifungua kuwekwa bayana kabisa! Hiyo ni moja ya siri nzito katika jamii.
Pamoja na nia njema ya kipindi hiki, lakini ni lazima kwa utawala wa ITV na wafanyakazi wao wazingatie walengwa hasa wa elimu hizo na muda wa kuzirusha kama lazima wazirushe. Kipindi chenye picha za kutisha namna hiyo kurushwa saa 1.30 jioni nini maana yake? Kama siri nzito kama hizi zinawekwa wazi kwenye TV kwa ajili ya umma, tutakuwa na siri gani tena za kuhifadhi?
ITV lazima ielewe kwamba masuala mengine kwa ajili ya umma. Ni kwa ajili ya watu maalum tu. Aidha, madaktari, wakunga, manesi na wanawake wenyewe. Siri ya mtungi ajuaye kata! Sasa kila mtu akiwa kata hata huo mtungi wenyewe si utavunjika?
Nawaomba ITV wawe walinzi wazuri wa siri za kinamama wanawake tunastushwa sana na masuala ya uzazi yanapowekwa hadharani bila ya kificho. Mnatusaliti na kutuvunjia heshima. Hadhi yetu iko wapi katika jamii? Kinamama wana siri zao zinazoambatana na maumbile yao. Ni mwiko na dhambi kubwa kabisa kuzidhalilisha kwa watu wasiohusika.
Jambo jingine linalokera ni kwamba kipindi hiki kilirudiwa tena siku ya Ijumaa ya Julai 9, 1999 saa 12.30 hali ya kuwa kimehaririwa vizuri kabisa. Heka heka zote zile za mwanzo hazikuwepo. Kumbe wahariri wa ITV walikuwa na uwezo wa kutuletea picha zinazoendana na mila, desturi na hadhi ya wanawake wa kwetu. Ila tu walitufanyia kusudi ili hata watoto wadogo watuone. Jamani! Hii adabu gani?
Nafasi ya mwanamke katika jamii za Kiafrika ni ya kipekee. Siyo viumbe wa kufanyiwa mchezo, kudhalilishwa na kuabishwa mbele ya watoto waliowazaa wenyewe!
Siku chache tu nyuma mlituletea kipindi cha malumbano ya hoja kilichorekodiwa Nkrumah Hall, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kikilumbana juu ya mada kama TV inaelimisha au inapotosha. Ingawa mada ilikuwa ni nzuri na 'debatable' lakini ilitungwa kijanja kijanja ili kukwepa hoja ya msingi.
TV kama chombo cha mawasiliano au habari ndiyo inaweza kuelimisha au kupotosha. Na anayeelimisha na kupotosha siyo TV bali vipindi vinavyorushwa kupitia TV. Kwa hiyo mada ile ya malumbano ya hoja ingekuwa na maana na inayokidhi haja kama ingekuwa hivi: "Vipindi vinavyowekwa kwenye TV vinaelimisha au vinapotosha jamii? Kusudi wachangiaji wachangie vipindi vya TV moja kwa moja. Kwa maana hii tungeweza kuvijuwa vipindi vinavyofaa na visivyofaa ili tuweze kuvirekebisha.
Ningemalizia tu kwa kuwaomba
ITV wawe wangalifu sana wanapoweka vipindi vinavyozungumzia mambo ya siri,
hususan ya kinamama. Heshima ya wanawake kama wazazi katika jamii inategemea
sana utunzaji wa siri zinazowahusu. Hakuna maana yoyote kuwaumbua kwanza
halafu ndiyo mjirekebishe.
--
|
|