Na Muhibu Said
MADRASAT Samaawiyya ni chuo pekee cha Kiislamu na cha siku nyingi kilichopo katika kijiji cha Mitengwe, tarafa ya Mzenga, wilaya ya Kisarawe, mkoa wa Pwani.
Madrasa hiyo ilianzishwa sambamba na Masjid Samaawiyya na Imamu wa Msikiti huo, Sheikh Maulid Jokolo, mnamo mwaka wa 1985 kijijini hapo.
Tangu kuanzishwa kwake mpaka sasa, Mwalimu pekee wa madrasa hiyo ni Sheikh Jokolo ambaye pia ndiye Imamu pekee wa Msikiti huo.
Madrasa hiyo ambayo inaungana kimajengo na nyumba anayoishi Sheikh Jokolo ina jumla ya wanafunzi wavulana na wasichana 150. Pia ina programu ya kuendesha darsa la akina mama watu wazima wa Kiislamu wanaofikia 12.
Masomo yafundishwayo na madrasat Samaawiyya ni pamoja na kujifunza kusoma Qur'an takatifu na mambo mengine mbalimbali ya Kiislamu.
Kwa muda wote wa uhai wake mpaka sasa, madrasa hiyo imeweza kutoa vijana kadhaa wanaoweza kuwafundisha wenzao Uislamu na wanaoweza kuendesha ibada tukufu ya swala msikitini hapo.
Madrasa hiyo ambayo imejengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi inakabiliwa na matatizo mbalimbali ya kimsingi, ikiwemo ufinyu wa nafasi inayoshindwa kuhifadhi idadi kubwa ya wanafunzi waliopo na watarajiwao.
Matatizo mengine makubwa na sugu mno ni kulazimika kusimama kwa madrasa hasa katika vipindi vya mvua, kutokana na nyasi zilizoezekwa juu yake kuruhusu kuingia maji kwa wingi, hali inayosababisha kuzuka kwa gharika lisilokuwa rasmi!
Hali hio pia huchangiwa na ukosefu wa uwezo wa kuliendeleza jengo la Msikiti na madrasa lililo ubavuni mwa Masjid hiyo ambalo uendelezaji wake umekwama tangu lisimamishwe mnamo mwaka 1997.
Juzuu, masahafu, vitabu vya kusomeshea, vikalio (mikeka au majamvi, madawati) na kadhalika navyo pia ni katika orodha ya matatizo sugu yanayoikabili madrasa hiyo.
Mbali na matatizo hayo, mtihani mkubwa unaotishia uhai wa Msikiti na madrasa hiyo ni hali mbaya ya kiafya inayomkabili Imamu na mwalimu pekee wa madrasa hiyo, Sheikh Jokolo.
Sheikh Jokolo anakabiliwa na maradhi ya maumivu makali ya miguu kwamuda sasa takribani miaka 17.
Anasema hali hiyo iliyomzukia ghafla miaka hiyo iliyopita, hupata unafuu kwa muda wa siku chache lakini humpa maumivu makali ikiwa ni pamoja na kuvimba miguu kwa muda mrefu.
Hali hiyo ya maumivu ya miguu anasema wakati mwingine humchukua kiasi cha muda wa miaka miwili mfululizo, hali ambayo anasema hufanya ashindwe kabisa kutembea kwenda kwenye hafla mbalimabli za Kiislamu na kwenda kujitafutia riziki.
Kutokana na kukabiliwa na mtihani huo, Sheikh Jokolo amelazimika kuwakabili ndugu zake Waislamu kuwaomba wamsaidie kwa hali na mali ama matibabu ya maradhi yake hayo au kumnunulia angalau kijibaiskeli cha walemavu cha miguu mitatu aweze kumudu vyema shughuli zake za Da'awah kijijini hapo. Na hiyo ni kwa kuzingatia kuwa yeye ndiye Imamu na mwalimu pekee wa Kiislamu anayetegemewa mpaka sasa kijijini hapo.
Sambamba na msaada huo, pia Sheikh Jokolo anawaomba makarimu wa Kiislamu wenye uchungu na dini yao wamsaidie vile vile kumlipa madeni yake yote ya fedha alizokopa kwa watu mbalimbali kijijini hapo tangu maradhi hayo yaliposhamiri na hivyo kushindwa kutembea kuhangaika kutatua matatizo yake ya kimaisha na kifamilia kwa ujumla. Fedha anazodaiwa zinakadiriwa kufika kiasi cha shilingi 25,000.
Ili uweze kumfikia salama
na kirahisi, msaada huo anaomba upelekwe katika ofisi za gazeti hili zilizoko
mtaa wa Mahiwa na Livingstone, karibu na Msikiti wa Kwa Mtoro, Kariakoo,
S.L.P. 55105, Simu Na. 181365, Dar es Salaam.
--
|
|