KWA nia njema ya kutaka kueleweshwa uzuri, naomba nijibu hoja zinazodai kuwa Allah sio Yehova, kama alivyohitimisha Bw. Elia Batendi katika makala ya "Yehova na Allah: Muhibu bado hujajibu hoja", katika ukurasa wa 8 wa AN-NUUR ya Juni 11-17, 1999.
Bw. Muhibu na wenziwe walishajibu zamani hoja zote za Bw. Batendi na wenziwe kwa kuorodhesha majina na sifa (attributes) nyingi za Mungu zilizoandikwa katika Biblia na Qur'an, na kuzithibitisha kuwa zinafanana, na hata Batendi amekiri hivyo. Katika ANNUUR hiyo, akina Batendi wameleta majina zaidi ya Yehova katika Biblia ambayo wanadai hayamo katika Qur'an, na kwa sababu hiyo wanadai Allah sio Yehova. Zipo njia nyingi za kujibu.
Njia moja ni kuonyesha kuwa hata majina na sifa hizi mpya za Mungu katika Biblia nyingi zinafanana na zile katika Qur'an, ama moja kwa moja (directly) au kwa maana pana. Sababu ya hizo chache kutofanana sana ni kama ilivyotabiri Biblia (Yer. 8:8-9; 23:32; Lk. 1:1-4) na pia Qur'an 2:79) kuwa mikono ya waandishi wa Biblia imegeuzageuza sehemu nyingi za Biblia kiasi cha kuifanya Biblia isifanane zaidi na Qur'an na pia kuyafanya maneno kadhaa ya Biblia yasifanane na maneno mengine ya Biblia hiyo hiyo moja kama mifano ifuatayo ionyeshavyo. Katika majadiliano haya na yoyote mengine, mara ithibikapo kuwa maneno hata wawili ya hoja moja sio kweli, basi hoja nzima inavunjika. Tuvumiliane nikikosoa hoja zingine waziwazi mno.
Majina ya "Baba", "Bwana wa Majeshi" na "Mungu wa Waisraeli" hayamo katika Qur'an:
Dai hili sio la kweli. Qur'an haitaji jina la "Baba" moja kwa moja kwa kuwa Wakristo walilikufurisha jina hilo kwa kudai kuwa Mungu ndiye "Baba mzazi wa Yesu" na pia kuwa Yesu ni "Mwana mzaliwa pekee" wa Mungu (Zab. 2:7; Yon 3:16-17). Sisi watu na wanyama ndio tuna wana wazaliwa (eg. Ebr. 11:17), sio Mungu, kwa kuwa kuzaa ni tendo la kinyama na lahusiana na matendo dhalili ya kijinsia ya sie wanyama. Biblia imekemea sana hii kufuru ya kumfananisha Mungu na kiumbe chochote (Isa 40:18 na 25; Lk 13:18 na 20). Lakini Qur'an imelitaja jina la "Baba" kwa maana pana ya "Muumba" (2:29; 32:7), "Mhuishaji", "Chanzo cha vyote", "Mwenyezi Mungu", au "Mrembaji" (59:24; 2:117) wa watu wote (pamoja na Waisraeli, majeshi n.k.) na viumbe vyote vyote vya limwengu zote = Rabbil-Aalaminy-Cherisher and Sustainer of all Worlds (1:2). Haya yote kwenye "" ni majina au Sifa za Allah.
Hebu tuulizane: "Je, Yehova au Allah sio Mungu wa Wanyakyusa pia? Kama ndio, kwa nini hawadai kuwa "Mungu wa Wanyakyusa" sio Yehova kwa sababu tu Biblia haimtaji "Mungu wa Wanyakyusa" pia? Vipi basi akina Batendi wanang'ang'ania Qur'an pia imtaje "Mungu wa Waisraeli" na "Mungu wa Ibrahimu/Isaka/Yakobo", vinginevyo wanadai eti "Allah sio sawa na Yehova", au eti "inadhihirisha kuwa (Allah) ni Mungu wa ushirikina wa Uarabuni" (kwa kauli ya Prof. Kaisi katika Msemakweli la 27/6-3/7/1999 ukurasa wa 6?) Hata aya aliyonukuu Bw. Batendi yasema: " Yer. 3:19 Mtaniita , Baba yangu, wala hamtageuka". Hii yaonyesha kuwa Mungu akiitwa Baba kwa maana hii pana, basi huwa ni Baba Muumba wa wanadamu na viumbe wote, sio wa Yesu peke yake, kama alivyosititiza mwenyewe: "Yn 20:17 Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie sijapaaa kwenda kwa Baba yangu, naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu".
Hata kuzaliwa kwa Yesu bila baba sio sababu ya kumwita Yesu mwana pekee wa Mungu, kwani Adam (hana baba wala mama), wala Melkizedeki (hana baba, mama wala wazazi, hana mwanzo wala mwisho Ebr 7:1-3), hawaitwi wana pekee wa Mungu!
Ifuatayo ni mifano michache ya majina au sifa za Mungu kwa lugha mbalimbali, yote yakiwa yanafanana: Mungu aitwa "Allah, Khaaliq, Hayyu (Kiarabu). Au Elohim, Eloi, Eli, Adonai, Yehova YHWH (Kiebrania) au Kyala (Kinyakyusa) au God (Kiingereza) au Got (Kikaburu) na kadhalika. Biblia ya The New Scofield Reference Bible iliyataja majina: Elohim, El, Elah na Alah, kuwa ni majina ya Mungu, sasa yameshafutwa! Kwa hiyo Allah ndiye huyo huyo Yehova.
Qur'an imeitukuza Makka, wakati Biblia imeitukuza Yerusalem:
Dai hili pia sio kweli. Kwanza, Biblia inasema kuwa utukufu wa Yerusalemu ulikuja kuondoshwa kutoka Seiri (Yuda/Yerusalem) kwenda Parani (Mkaa, Arabia) (Yn 4:21-3; Mt 21:43, 23:37-9; Kum 33:1-2. Mwa 21:20-1; Gal 4:21-5) na kupewa Taifa lingine (Waarabu), "Maana Hajiri ni kama mlima wa Sinai ulioko Arabuni". Pili, Qur'an imeitukuza Yerusalem pia:
"17:1 Utukufu wa Wake Yeye (Allah) ambaye alimpeleka mja (Muhammad) Wake usiku mmoja tu (Miraji) kutoka Misikiti Mtukufu (wa Makka) mpaka Msikiti wa mbali (Palestina, uitwao Baytil-Muqaddas/Masjidil-Aqsa/Haram as-Shariff = Hifadhi tukufu) ambao Tumeubariki na Tumevibariki vilivyo pembezoni mwake...".
Tatu, umaarufu wa Yerusalem au kitu chochote wategemea sana maudhui, ikiwa waongelea pahala pa kuhiji au alipozaliwa Mtume (s.a.w.) au pa kuelekea wakati tunaposali, au paliposhukia aya nyingi za Qur'an (Makka na Madina), basi mji wa kutukuzwa ni Makka: "27:91 bila shaka nimeamrishwa nimwabudu Mola wa mji huu (Makka) ambao Kautukuza". Kwa hivyo miji yote miwili yatukuzwa na Qur'an na Biblia pia; hivyo hoja hii pia imekufa.
Yehova anawapenda Waisrali, na Allah anasema Mayahudi ni maadui kuliko wote:
Nayo hii sio kweli. Biblia inaripoti kuwa kuna nyakati Yehova aliwapenda na nyakati zingine aliwachukia mno Waisraeli kwa ufisadi wao, kama isemavyo Biblia:
"Kut 32:9 Tena BWANA (Mungu) akamwambia Musa, mimi nimewaona watu hawa, na tazama ni watu wenye shingo ngumu; 10: basi sasa niache ili hasira zingu ziwake juu yao, niwaangamize..." (Tazama pia: Kum 9:14; Hes 14:12) Qur'an pia imeongelea kupendwa kwa Waisraeli (2:47:-53), Kibri (2:54-59; 2:80; 96; 7:161), pamoja na makemeo na adhabu kwao 17:4-8). Kwa hiyo, kwa hoja hii pia Biblia na Qur'an zimefanana, na hivyo kuivunja hoja hii ya Bw. Batendi.
Uadui anaoutaja Bw. Batendi ni wa Mayahudi na Wapagani (na pia Wakristo) dhidi ya Waislamu; uadui ambao hauishi bado Waislamu wazifuate imani na mila zao potofu kama inavyosema Qur'an:
"5:82 Hakika utawakuta walio maadui zaidi kuliko watu wengine kwa Waislamu ni Mayahudi na wale mushurikina wasiokuwa na Kitabu...".
"2:120 Hawatakuwa radhi juu yako Mayahudi wala Wakristo mpaka ufuate mila zao".
"2:135 Na wakasema Mayahudi; ' kuweni Wakristo na mtaongoka', na wakasema Manasara, 'kuweni Wakristo na mtaongoka'...
Ambapo Uislamu unaamuru kutowalazimisha wasio Waislamu kusilimu:
"2:256 Hakuna kulazimishwa mtu kuingia katika dini.
Hili ndilo chimbuko la malumbano yote haya. Kadiri Waislamu wasivyokubali kwa wingi kubatizwa (juu ya umaskini wao na juu ya hongo nyingi wapewazo) na kadiri Wakristo wengi sana (tena wasomi na viongozi) wanavyosilimu hususan kwenye mihadhara, ndivyo chuki-pofu za Wakristo zinavyozidi kupamba moto.
|
|