Uchaguzi Ubungo, Temeke:
Tume yaundwa kuchunguza matokeo
 

Na Bakari Mwakangwale
 

WAKATI baadhi ya wananchi wa majimbo ya Temeke na Ubungo wakilalamikia matokeo ya chaguzi ndogo za viti vya Ubunge zilizofanyika Jijini hivi karibuni, TCCR imeunda Tume ya uchunguzi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyofika katika ofisi za ANNUUR inaeleza kuwa kwa kuwa Tume ya Uchaguzi ya Serikali imeshindwa kufuata misingi ya haki katika Uchaguzi Mkuu 1995 pia chaguzi ndogo ndogo zinazofanywa katika majimbo ya Wabunge.

"Tume hii imedhihirisha kuwa imekisaidia Chama tawala tu, pia Chama tawala ndio kilicho chagua Tume", imeeleza taarifa hiyo.

Imeendelea kusema taarifa kuwa, kesi nyingi sana za Wabunge zilizobatilishwa na mahakama kuu hapa nchini na pia kesi zilizofunguliwa baada ya Uchaguzi Mkuu ni nusu ya majimbo ya uchaguzi kwa nchi nzima na wengine kukosa fedha za kufungulia kesi zao.

"Tunajua kuwa uchaguzi pia wa Rais haukuwa wazi na haki (free and fair) ila tu sheria inatukataa kuziuliza kura zake, huo ni udikteta. Hivyo TCCR imeamua kutangaza Tume ya Uchaguzi itakayoshirikiana na Tume ya Uchaguzi ya Serikali ili zifanye kazi pamoja katika chaguzi zinazoendelea na Uchaguzi Mkuu mwaka 2000 na kuendelea", imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo yenye vipengele zaidi ya vitano na iliyotiwa saini na Mwenyekit wake, Chifu Masanja imeendelea kusema kuwa, Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 tunaziomba jumuia za Madola kusimamia Uchaguzi huo. Matokeo ya kura za Rais hata kama yatatangazwa lakini asiapishwe hadi siku 90 zipite bila malalamiko yoyote; basi mahakama haina budi kusikiliza kwa uangalifu malalamiko hayo.

"Tumejifunza kuwa malalamiko ya aina hiyo ndiyo chanzo cha vurugu katika nchi zetu hususan Afrika", imesema taarifa ya TCCR.

Aidha imeeleza kuwa, kama serikali haitaikubali basi muda wake utakapoisha Oktoba, 2000 basi watataka serikali ikadhibiwe kwa Jaji Mkuu ili aongoze serikali hadi Jaji Mkuu atakapoitisha kongamano la Katiba kuelekea uchaguzi chini ya katiba mpya.

"TCCR haitakubali kuendelea na utawala huu tena", imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeorodhesha majina ya waliomo kwenye tume hiyo kuwa ni Alhaj Jaji Musa Kwikwima - Mwenyekiti, Mwalimu Boaz Kapaya, Ramadhani Mwandu, James Boas, Said Msabila Mdachi pamjo ana Ally Elias.

Ikielezea suala la ruzuku katika vyama vya upinzani imeeleza kuwa, serikali imetoa tamko rasmi kukataa kuitoa ruzuku katika uchaguzi mkuu hivyo wameomba wahisani wasiufadhili uchaguzi mkuu na serikali ikabidhiwe kwa Jaji Mkuu ili uitishwe uchaguzi mkuu wa katiba.

"Kwa kuwa CCM inaendeleza udikteta ili kuwanyima raia haki ya demokrasia basi tunaziomba nchi wahisani na mashirika ya kimataifa yasiisaidie tena serikali ya Tanzania hadi muafaka wa katiba uwepo maana misaada haifiki kwa awalengwa", imemaliza taarifa hiyo ya TCCR.


Kesi ya Mwembechai yaahirishwa tena
 

Na Muhibu Said
 

KESI mojawapo kati ya tatu za tuhuma za kufanya vurugu maeneo ya Mwembechai inayowakabili Waislamu kumi, imeahirishwa hadi Agosti 18, mwaka huu, kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa katika mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Jijini Dar es Salaam.

Kuahirishwa kwa kesi hiyo kumetokana na Hakimu anayeisikiliza Bw. Gabriel Mirumbe, kutokuwepo mahakamani Jumanne ya Julai 13, mwaka huu, siku ambayo kesi hiyo ilitarajiwa kuendelea kusikilizwa mahakamani hapo. Ilielezwa Hakimu huyo yuko likizo.

Kesi hiyo yenye namba 407, awali ilifunguliwa na serikali katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini hapo mwaka jana. Baadae ilihamishiwa katika Mahakama ya Kivukoni Jijini kabla ya siku chache kuhamishiwa katika mahakama ya wilaya ya Kinondoni ambako ndiko inakoendelea kusikilizwa hadi sasa.

Kesi hiyo imekwishasikilizwa mara mbili ambapo mashahidi wa upande wa serikali wamekuwa wakitoa ushahidi wao.

Mashahidi ambao wamekwishajitokeza kutoa ushahidi wao upande wa mashitaka ni pamoja na askari polisi wa kituo cha Magomeni, Bw. Moses na Ofisa wa zimamoto Jijini, Bw. Mohamed Mlawa.

Kesi nyingine kama hiyo inatarajiwa kuendelea kusikilizwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu Jijini hapo Julai 20, mwaka huu. Mashahidi wa upande wa serikali wanatarajia kuendelea kutoa ushahidi wao.

Kesi hiyo yenye namba 184/98, imekwishasikilizwa mahakamani hapo zaidi ya mara tano ambapo mashahidi wa upande wa serikali wamekuwa wakitoa ushahidi wao. Kesi hiyo inawakabili Waislamu 11.

Kesi nyingine ya tuhuma ya uchochezi inayomkabili aliyekuwa Imamu wa Msikiti wa Mwembechai, Sheikh Omar Bashir itatajwa tena hapo Julai 19, mwaka huu.

Kesi hiyo yenye namba 1621 ilifunguliwa na serikali mwaka jana katika mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu na iko mbele ya Hakimu wa mahakama hiyo Bw. Lwakibadila.

Kesi hiyo ilitajwa tena mahakamani hapo Jumanne ya Juni 22, mwaka huu na kuahirishwa hadi Julai 19, mwaka huu, kwa madai kwamba jalada la kesi hiyo liko kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DPP).

Tangu kufunguliwa kwake mwaka jana, kesi hiyo imekuwa ikitajwa mahakamani hapo na kuahirishwa kwa madai kwamba jalada lake bado halijafikishwa mahakamani.

Aidha, imebainika kuwa Sheikh Bashir amekuwa akitajwa pia katika kesi namba 184/98 inayowakabili Waislamu 11 wanaodaiwa kufanya vurugu maeneo ya Mwembechai mwaka jana.

Sheikh Bashir amekuwa akitajwa kama mtuhumiwa wa kesi hiyo, Waislamu hao walipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza hapo mwaka jana na kusomewa shitaka hilo.


Waalimu waazimia kufundisha elimu ya Kiislamu mashuleni Mtwara
 

Na Fatma Musa, Mtwara
 

SEMINA ya waalimu Waislamu iliyomalizika Julai 12, mwaka huu mjini Mtwara imeazimia kuanza rasmi kufundisha somo la elimu ya dini katika mashule mbalimbali mkoani hapa.

Washiriki 70 wa semina hiyo iliyowajumuisha waalimu wa shule za msingi, sekondari na madrasa kutoka mjini Mtwara na mkoa wa jirani wa Lindi waliahidi kuanza kuyatekeleza yale waliyojifunza kwa kuanza na kuwavisha watoto wao mavazi ya Kiislamu.

Mada tatu zilichokozwa na kujadiliwa kwa kina na washiriki wote wakiongozwa na wahadhiri maarufu kutoka Lindi na Mtwara.

Akizungumza katika semina hiyo, Bwana Musa Mdidi kutoka Lindi alionyesha uadui uliowazunguka Waislamu hapa nchini ambao umekuwa ukikwaza jitihada zao mbalimbali.

Bwana Mdidi aliwataka waalimu hao kuujua uadui huo na kuchukua hatua za kupambana nao kwa kuanza ma malezi ya wanafunzi mashuleni.

Wadhahiri wengine katika semina hiyo iliyoanza Julai 6, walikuwa Bwana Said Bawazir, Kombo Ali Fundi na Mohamed Saleh kutoka Kenya.


Waislamu tujifunze toka Kosovo - Amir Lulu
 

Na Idd Katimba, Mwanza
 

WAISLAMU wote wametakiwa kutumia kila mtu alichonacho kwa manufaa ya Uislamu.

Akizungumza na Waislamu katika Msikiti wa Raudhwa mtaa wa Lumumba mara baada ya kisomo kwa ajili ya kumrehemu Sheikh Khamis Khalfani aliyefariki Julai 3, mwaka huu aliwataka Waislamu wajifunze yanayowapata Waislamu wa Kosovo, wanauawa bila ya kuulizwa wao ni Waislamu wa aina gani, maadam ni Muislamu basi hukumu ni moja tu kuuawa, alisema ni bora mwenye elimu au utaalamu wa aina fulani autumie vile vile kwa manufaa ya Uislamu na jamii nzima.

Akisisitiza umuhimu huo, alitoa mfano wa timu ya mpira ambapo wachezaji huwa ni kumi na moja, kila mchezaji anacheza nafasi yake kwa lengo moja tu ambalo ni ushindi, hivyo ikiwa kila Muislamu atafahamu na kutekeleza wajibu wake kwa malengo na Uislamu ukiwa mbele, bila shaka tutafaulu kwani hiyo ni ahadi ya Allah (s.w.) kwetu.

Akigusia "wimbo" wa sasa wa karne ya ishirini na moja ya "sayansi na teknolojia" alisema kwa Muislamu msomi aliyesoma kwa ajili ya Allah (s.w.) mambo ya sayansi yamejaa ndani ya Qur'an. Alitoa mfano wa suratul Hadidi inayoelezea jinsi chuma kilivyo na faida na madhara kama kitatumika vibaya.

Aliwaasa Waislamu juu ya kushndwa kwao kuutangaza Uislamu hadharani, alisema Waislamu wametishika na propaganda za makafiri za kuitwa siasa kali, mujahidina, magaidi na majina mengineyo mabaya mabaya hadi sasa Muislamu kama ni Abdallah Ally Makaranga basi mara zote atajiita A.A. Makaranga, sasa tutajuana vipi kwa kujifichaficha kiasi hiki?

Alisisitza kuwa kila mtu atumie utaalamu wake kwa kushirikiana na wataalamu wa nyanja isiyo yake ili mradi lengo ni Uislamu kuwa juu. Aliwashauri Masheikh na Maulamaa ambao wamebobea katika mambo ya elimu ya dini tu kutokudharau wataalamu ambao hawakusoma upande wa utaalamu wa dini, washirikiane na kuheshimiana.

Alisema, marehemu Sheikh Khamis Khalfan alishirikiana na wote ndio maana amekuwa na msimamo wa kutokuwa na kundi au taasisi maalum aliyoiongoza.

Alimalizia kwa kuwaomba Waislamu kuufuata Uislamu kwanza kwa Tawheed ya kweli na pili Qur'an yenyewe na Sunna za Mtume wetu Muhammad (s.a.w.) ambao ndio usia mkuu aliotuachia mashuhuri katika khutba yake ya kuaga siku alipowahutubia Waislamu kwenye Hijja yake ya mwisho.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook