Ikabeni koo serikali ifuate Katiba - Lipumba
 

Na Mwandishi Wetu
 

PROFESA Ibrahimu Lipumba amewahimiza wananchi wawe madhubuti na washinikize kufuatwa kwa Katiba kwani bila kufanya hivyo hali itaendelea ya kutokuwa na Tume huru ya uchaguzi.

Lipumba amesema kuwa bila ya wananchi kuzijua haki zao na kujitoa muhanga hawataweza kuziwajibisha taasisi muhimu zenye kusimamia haki zao muhimu. Kwa kukosekana kwa hilo Prof. Lipumba amesema kuwa uchaguzi mdogo wa Wabunge katika majimbo ya Ubungo na Temeke ulikuwa wa hila, njama na vitisho hivyo kuwezesha wagombea wa CCM kupata ushindi.

Akizungumza na ANNUUR jana Mshauri Mkuu wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba alisema matokeo yaliyotangazwa na Tume hayakuwa halali na yameitundika demokrasia kitanzini.

Profesa Lipumba alisema chama chake kimeorodhesha matukio kadhaa kama ushahidi wa kukosekana haki katika uchaguzi huo.

Alitoa mfano wa eneo la Goba ambalo linaonyesha asilimia 150 ya wapiga kura zaidi ya matarajio kulinganisha na maeneo mengine.

"Wengi waliopiga kura sio wa maeneo hayo", alisema Profesa Lipumba.

Walikamatwa watu kadhaa ambao walikuwa na shahada za uongo hata hivyo walipowafikisha polisi waliachiliwa.

"Tulikutana na Incharge wa CID wa Kinondoni kuulizia hatua zilizochukuliwa juu ya watu hao, akatuambia walipewa dhamana na akatuomba kama kuna watu wa kwetu waliokamatwa na hali hiyo twende tukawawekee dhamana", alieleza kwa mshangao Lipumba.

Alisema walishangazwa na hali hiyo kwa sababu polisi mara kadhaa wamekuwa wakiwakatalia dhamana wafuasi wa CUF kwa madai kwamba kesi zinazohusiana na uchaguzi ni serious kwa hivyo watuhumiwa wasingeweza kuachiwa haraka.

"Limetokea upande wa CCM dhamana inakuwa wazi haraka kiasi hicho, huu ndio utendaji wa vyombo vya dola", aliongea kwa masikitiko Profesa Lipumba.

Kuhusu utendaji wa Tume ya uchaguzi Lipumba alisema umeegemea kwa chama tawala hivyo hauna uwezo wa kusimamia haki wala kutoa matokeo halali.

"Ni Tume inayopokea maelekezo ya CCM na kuyafanyia kazi, imekuwa ikiipendelea CCM", alisema.

Profesa Lipumba pia aliviliamu vyombo vya habari kwa kuonyesha upendeleo wa wazi kwa chama tawala.

Alisema polisi imekuwa ikiwakamata wapinzani kwa maelekezo ya CCM.

"Wafuasi wa CUF wamekuwa wakipigwa na kukamatwa na polisi kwa madai ya kufanya fujo wakati CCM ndiyo yenye kufanya vitendo hivyo na kuwasingizia wapinzani", alisema Prof. Lipumba na kuongeza kwamba polisi imekuwa chombo cha dhulma badala ya kusimamia usalama.

Matukio kadhaa alisema Prof. Lipumba ambayo yamekuwa yakiripotiwa na CUF kuhusiana na vurugu zinazofanywa na CCM polisi imeshindwa kuyachukulia hatua.

Gazeti hili liliwasilana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam Alfred Gewe kuhusu taarifa hizo za CUF alikiri kuwepo kwa matukio hayo lakini hakuweza kusema ni hatua zipi ilizozichukua jeshi la polisi dhidi ya wafuasi hao wa CCM.

Kituo kimoja cha televisheni juzi kilionyesha wana CCM wakimpiga kijana mmoja wa Temeke kwa madai kuwa ni mfuasi wa CUF.

Kitendo hicho cha uonevu kilionyeshwa sambamba na maelezo ya Mkuu wa Mkoa yanayowataka wafuasi wa CUF wajiepushe na vurugu.

Hadi sasa polisi imewakamata wafuasi 17 wa chama cha CUF inaodai kuwa wamehusika na vurugu zilizosababisha hasara za mamilioni ya shilingi.

Wananchi wengi walioongea na gazeti hili kufuatia hatua za uonevu ambazo zimekuwa zikichukuliwa na polisi kabla na baada ya uchaguzi wamekitaka chombo hicho cha dola kuacha upendeleo na dhulma kwa wananchi.

Wakati huo huo, Chama cha CUF kimesema kitaendelea jitihada za kupigania katiba mpya katika kipindi chote kilichobaki kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwakani.

Akizungumza na mwandishi wa ANNUUR jana Mkurugenzi wa Habari wa CUF Bw. Ramadhani Mzee alisema matatizo yanayojitokeza katika uchaguzi na maeneo mengine ya uendeshaji wa nchi kimsingi yanatokana na udhaifu uliomo kwenye katiba ya nchi.

Bwana Mzee alisema CUF itashirikiana na taasisi ya KAMAKA kudai katiba mpya itakayokidhi haja na matakwa ya wananchi.

"Nchi yetu haijawa na Katiba inayotokana na ridhaa ya wananchi wenyewe tangu tupate uhuru mwaka 1961", alisema Mzee.

Naye Profesa Lipumba akizungumzia suala la Katiba alisema tatizo la nchi yetu kutokuwepo kwa katiba ya muafaka na taasisi makini za uendeshaji wa nchi.

"Tunaweza kuwa na katiba nzuri lakini taasisi za usimamizi na uendeshaji zikawa hizi zinazokwenda kinyume na Katiba", alisema.

Aidha alionya kuwa pasipokuwepo Strong civil society kushinikiza kufuatwa kwa Katiba hali itaendelea kuwa hii ya serikali kutotenda haki, mahakama kutokuwa huru na kukosekana Tume huru ya Uchaguzi hata kama katiba itakuwa nzuri.

Alionyesha haja kwa Watanzania ya kuzijua haki zao na kuamua kujitoa muhanga kuzisimamia kwa kufanya hivyo wataweza kuziwajibisha taasisi husika.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook