Pamoja na vyombo vya dola kuwatisha baada ya matokeo:
Wananchi watembea vifua mbele
 

Na Mwandishi Wetu
 

USIKU wa Jumatatu kuamkia Jumanne ulikuwa wa aina yake kwa wakazi wa Manzese ambapo kwa masaa kadhaa wananchi kwa mamia walikuwa wametazamana na askari polisi wenye silaha, mbwa na wale wa FFU kama majogoo yanayopimana nguvu.

Polisi wakiwa wamejikusanya kwenye tuta katikati ya barabara walizungukwa na wananchi kwa pande zote za barabara. Baadhi ya wananchi walisimama wakiwa wametulia wakiwatizama polisi huku wengine wakipandishana mori kwa nyimbo na kuruka ruka mithili ya morani.

Mara kadhaa wananchi hao walioonekana kuwa wafuasi wa CUF walikimbia matiti kati ya Tawi la Kossovo na eneo la Urafiki na kurudi tena Kossovo.

Wanachi hao walikusanyika eneo hilo toka mchana wakisubiri kutangazwa kwa matokeo ya kura. Hadi kufikia saa kumi jioni wananchi wengi walikuwa wamefurika eneo hilo.

Wafuasi wachache wa CCM waliokuwa na magwanda ya CCM walijitokeza kutokea ofisi ya CCM Manzese Tip Top hata hivyo iliwawia vigumu kuonyesha shamra shamra yoyote na badala yake wakawa wanatoweka mmoja mmoja.

Ilionekana wazi wimbi la upinzani lilikuwa limeizidia CCM kwani kila aliyejaribu kujitokeza barabarani ama akiwa na bendera au nguo ya kijani wingi wa wananchi walio tofauti naye ulimtisha na kupotelea vichochoroni.

Kuchelewa kutolewa kwa matokeo kulizidi kuwavuta wananchi na wakati huo huo kujazana kwa askari wa kawaida na wale wa FFU.

Walirukaruka na kukimbia hapa na pale huku wakiimba vibwagizo kama: "Tumechoka kuonewa". "Hatuogopi Segerea", "Leo tutalipiza Mwembechai".

Ilikuwa ni hali iliyovuta taswira ya hali ilivyokuwa wakati Waafrika Afrika Kusini walivyokuwa wakiimba nyimbo za kuhamasishana kupambana na makaburu.

Hali hiyo ilidumu hadi pale Prof. Ibrahim Lipumba alipokuja kwenye majira ya saa 5 usiku na kuwasihi watawanyike waende nyumbani.

Kutwa ya Jumanne iliwashuhudia wanachama hao wa CUF wakikusanyika katika Tawi la Kossovo wakipongezana na kuweka mikakati ya kuendelea kufungua matawi.

Hadi tunakwenda mitamboni viongozi wa CUF bado walikuwa wakitafakari la kufanya baada ya kutokuridhika na matokeo ya uchaguzi.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook