'Kutozungumza siasa Misikitini ni pumbao la kisiasa'
 

Na Mwandishi Wetu
 

MWANAHARAKATI maarufu na muasisi wa vuguvugu la wanafunzi na vijana wa Kiislamu nchini, Mwalimu Mtengwa Burhani amewahadharisha Waislamu na pumbao kuwa siasa isizungumzwe Misikitini.

Mwalimu Mtengwa alitoa hadharisho hilo katika mkesha wa Maulid yaliyofanyika Jumamosi iliyopita katika Msikiti wa Mtambani.

Alisema nadharia ya kuitenganisha dini na siasa iliasisiwa na Karl Marx baada ya Kanisa lililokuwa likitawala nchi za Ulaya kujihusisha na harakati kandamizi dhidi ya makabwela waliotumikishwa kinyama na mabwanyenye kwa ujira mdogo.

Alisema kutokana na ukandamizaji huo wa mabwanyenye uliopewa baraka zote na Kanisa ndipo Marx alipoibuka na mfumo wa Kijamaa ambao nadharia zake zinaitenga dini na masuala ya siasa kwa hoja kwamba ni kasumba iliyotumika kuwalaza watu waendelee kunyonywa na kukandamizwa.

Mwalimu Mtengwa ambaye ni msomi wa Historia alieleza umati uliofurika Msikitini hapo kuwa mawazo ya Marx yalikuja kuwekewa matendoni na Lenin wakati wa kilichoitwa mapinduzi makubwa ya Urusi ya mwaka 1917 ambapo dini zilipigwa marufuku na majengo ya ibada kuwa majumba ya makumbusho na vilabu vya starehe.

Katika hotuba fupi iliyosikilizwa kwa utulivu mkubwa, Mwalimu Mtengwa alisema hapa nchini nadharia hizo ziliingizwa rasmi wakati wa Azimio la Arusha ambalo liliitangaza Tanzania kuwa nchi inayofuata itikadi ya "Ujamaa na Kujitegemea".

"Kuanzia wakati huo propaganda ya kutochanganya dini na siasa, serikali haina dini, zikaanza kuenezwa na bahati mbaya sana Waislamu ndio waliopumbazwa na pumbao hilo", alisema Ustaadh Mtengwa.

Aliwakumbusha wale wanaowataka Waislamu wasizungumze siasa Misikitini kuwa ni Misikiti na madrasa ndizo zilizotumika kama vituo vya harakati za kudai uhuru wa nchi hii.

"Muislamu wa mwaka '61 ni tofauti na huyu wa sasa aliyekolewa na pumbao la kisiasa la kuiweka mbali Misikiti na harakati za kisiasa", aliasa Ustaadh huyo.

Katika siku za hivi karibuni kumejitokeza madai kwamba Waislamu wanaitumia Misikiti kuzungumza siasa badala ya kuendesha "mambo ya dini". Madai hayo yalipewa uzito mkubwa wakati wa kampeni za uchaguzi za Ubunge katika majimbo ya Temeke na Ubungo.

Katibu Mkuu wa CCM Bwana Philip Mangula aliwashutumu Waislamu kwa kile alichokiita kutumia Misikiti kuendesha kampeni za chama kimoja cha siasa.

Hata hivyo Bwana Mangula hakuweza kueleza chochote juu ya harakati zinazoendeshwa na serikali ya chama tawala za "kupora" hafla za Kiislamu kugeuza majukwaa ya mashambulizi dhidi ya Waislamu.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook