BAADHI ya vyombo vya habari jana viliripoti kuwa Wabunge kadhaa walimcharukia Waziri wa Elimu na Utamaduni Profesa Juma Athumani Kapuya wakimtuhumu kuleta udini katika mfumo wa elimu. Udini unaodaiwa ni pale katika hotuba ya makadirio ya matumizi ya Wizara yake, Prof. Kapuya alipoeleza kwamba kila Mwalimu Mkuu na Wakuu wa Vyuo watawajibika kuhakikisha kwamba wanafunzi madhehebu ya dini mbalimbali wanapewa fursa ya kuabudu nyakazi za sala kuu na pia waruhusiwe kuvaa mavazi yanayokubalika katika maadili yao.
Ni dhahiri wanaotakiwa kupewa fursa ya kuabudu sala kuu sio Wakatoliki wala Wasabato kwani tangu hapo Jumapili na Jumamosi ni siku za mapumziko. Ni wazi pia sio Wakatoliki au Waprotestant wanaoombewa ruhusa ya kuvaa kwa mujibu wa dini zao kwani hata Makanisani huenda na "sketi" na "blaus" au magauni ya urefu na mshono sawa tu na ule wa sare za shule.
Aidha, kwa upande wa watawa Wakatoliki wamekuwa wakivaa sare zao wala hapana aliyewahi kuwabughudhi; si shuleni, chuoni au kazini.
Nidhahiri basi waliomcharukia Waziri Kapuya walikuwa wanapinga wanafunzi Waislamu kupewa fursa ya swala ya Ijumaa na kuvaa hijab. Na hii ndio tafsiri yao ya udini.
Wabunge waliotajwa kwa majina kumtaka Prof. Kapuya kuondoa kipengele hicho katika hotuba yake ni Mhe. Thomas Nyimbo (CCM), Mhe. Ndimara Tegambwage (NCCR), Mhe. Wilbroad Slaa (CHADEMA), Mhe. Mufwalamagoa Kibaasa (NCCR) na Richard Ndasa (CCM).
Wabunge hao walisimama katika hoja ya uzalendo kwamba wanapigania umoja, kuendeleza amani na utulivu na kuzuia migawanyiko.
Kama ipo ihsani ambayo Wabunge hawa walishawahi kuwafanyia wananchi basi ni hii ya kuwatangazia kwamba wao huingia Bungeni na dini zao pamoja na ukereketwa wao. Laiti wangekuwa na chembe ya uzalendo tungewasikia wakihoji vipi nchi hii iwe mwanachama wa Jumuiya ya Madola wakati kiongozi mkuu ni Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Anglikana duniani. Tungewasikia pia wakihoji nafasi ya Balozi wa Vatican nchini hapa wakati nchi hii si ya Kikatoliki. Aidha, tungewasikia wakicharuka kwanini Kadinali Pengo apewe itifaki ya hadhi ya Rais wa nchi.
Ungekuwepo uzalendo, tungewasikia wakihoji vipi siku ya Jumamosi ikafanywa siku ya mapumziko baada ya wanafunzi Wasabato kukataa kusoma siku ya Jumamosi. Wangekuwa wanapigania umoja tungewasikia kauli zao wanafunzi Waislamu wanapolalamika kulazimishwa ama kuwahudumia nguruwe au nguruwe hao kunajisi mazingira ya shule. Wangekuwa agenda yao ni amani na utulivu wa nchi hii tungewasikia wakihoji kwanini Waislamu waliuliwa pale Mwembechai, aidha tungewasikia wakiichagiza serikali kwanini haijawafikisha mahakamani wale waliowaua wananchi kwa risasi za moto. Tungewasikia wakihoji taratibu na sheria zilizotumika kuwaruhusu polisi kuvamia Msikiti kuwadhalilisha wanawake na kuishia kuamrishana "piga yule", "piga shaba". Bila kujali kuwa hao wanaowaua ni binadamu na sio vicheche.
Wabunge hawa wasidhani kwamba wanamshambulia Waziri Kapuya. Wanawashambulia wananchi waliopo mitaani. Wananchi ambao dini yao inawaelekeza waondoe ovu kwa mikono yao na kama ni wanyonge sana basi ndio waseme tu na kuchukia. Udhaifu na unyonge huu unakuwepo tu pale wanapokuwa hawajatambua mazingira na hisia za watu kama Wabunge wao. Watakapowajua kwa rangi na sura zao halisi na huo utakuwa ndio mwisho wa mchezo. Watu watagawana mitaa na kwa mchezo huu wa Wabunge wetu, ilani ikiambazani.
Dk. John Sivalon alishaeleza kuwa toka miaka ya 1970 walikuwa wanajigamba kwa asilimia yao kubwa Bungeni. Na haya wanayoyasema leo ni kielelezo cha kujiamini walichofikia na jinsi wanavyotumia fursa mbalimbali kuendeleza ubabe dhidi ya wengine. Lakini yote hii ni kheri, kufichua kwao hisia zao kunaimarisha zaidi umoja wa Waislamu.
Lakini Wabunge hawa na wengine wanapaswa wajue kuwa maelekezo haya ya Wizara ya Elimu ni ihsani ya serikali kwa wakereketwa wa dini zao ambao hawaoni raha bila ya kuwabughudhi Waislamu wakienda kuswali Ijumaa au wakivaa hijabu.
Muislamu hahitaji ihsani
hii kwani hahitaji kibali cha Bunge kuwa Muislamu. Yeye huangalia amri
ya yule anayemtaka aipiganie dini yake kwa mali yake na nafsi yake. Na
hata kama anaonekana mnyonge leo basi ni udhaifu wa kutokujua hisia na
ukereketwa wa Waheshimiwa Wabunge huko Bungeni wanakoingia na dini zao.
Na kwa mwendo huu ipo tamaa, punde tu udhaifu huu utaondoka.
--
|
|