UCHAMBUZI WA HABARI
 
Hakuna atakaehimili mapambano ya Wananchi
 

Na Mwandishi Wetu

MNAMO Julai 4, 1776 vuguvugu la kujikomboa kwa Waamerika lilishika kasi ambapo mwanadiplomasia Thomas Jefferson alitoa andiko la uhuru lililonadi kujitoa kwa Amerika kutoka chini ya himaya ya kikoloni ya Mfalme wa kiingereza aliyeitwa George III.

Ilipofika 1783 Wananchi walichachamaa mno maandamano huku na kule utawala ukashinikizwa kukubali matakwa ya wengi. Waingereza walitii shinikizo wakiwa na uwezo mkubwa kijeshi mbali ya kuwa taifa kubwa wakati huo.

Kwanini Waamerika waliamua kujitoa muhanga huku wakijua wazi hatari ya jaribio lao? Ni vipi waliweza kujiamini kwamba walikuwa sahihi katika mgogoro wao na Uingereza? Ni kwa kiasi gani waliweza kuamini kuwa hali ya baada ya kujikomboa ingekuwa bora kuliko kuishi chini ya ukoloni? Haya ni maswali yanayoulizwa na kujibiwa na waandishi wengi wa masuala ya siasa zama hizi.

Msukumo mkubwa wa vuguvugu la kujikomboa ni imani waliyokuwa nayo waamerika zama hizo kwamba matatizo yao yangeweza kutatulika na kwamba wangeweza kupata utatuzi na namna nzuri ya kukabiliana nayo. Wangeweza kufanya hivyo kama pangelikuwepo na mawazo au nadharia za siasa na serikali zinazotoa uchambuzi na utatuzi wa matatizo sambamba na matarajio yao na hilo ndilo lililowafanya wajitoe muhanga..

La mwanzo waliloanza kama msingi wa yote katika kujiondoa na hali iliyokuwepo ni lile la kuweka muafaka wa kijamii (Katiba) ambao uliwahitaji Wanajamii wote kujifunga, na huo huo kuwa dira ya utendaji wa serikali zilizokuja kuongoza.

Katika mkataba huu serikali ilipewa nguvu fulani lakini ikitii na kufuata sheria na kanuni zilizowekwa na kutumia nguvu hizo kwa ajili ya maslahi ya raia wote. Na pale viongozi wanapozitumia nguvu hizo visivyo au kwenda kinyume na kanuni basi mkataba ule ungekoma mara moja. Raia walipewa uwezo kikatiba kuvunja mkataba na serikali iliyoko madarakani pale inapotenda kinyume na makubaliano. Hawakupaswa kuendelea kutii serikali inayofukia msingi wa kuwepo kwake.

Akifafanua mkataba huo Bwana Thomas Jefferson alisema: " Ni haki ya raia kuasi au kuiondoa serikali iliyo madarakani na kuweka mpya (muda wa kuwa imekwenda kinyume na kanuni zilizowekwa kikatiba)". Waamerika wamedumu na hali hiyo hadi hii leo wakiheshimu mambo muhimu matatu:

(a) Mamlaka na haki ya kuunda serikali yanatoka kwa wananchi (raia).

(b) Nguvu inazopewa serikali zina ukomo ambao ukikiukwa watu hawapaswi kuendelea kutii.

(c) Wananchi wanayo haki kuiasi na kuiangusha serikali isiyokidhi matakwa yao.

Kutokana na haya, leo hii Amerika haina upuuzi wa kiongozi kufanya atakavyo huku dola ikimpa ulinzi au vyombo vya habari kumjenga. Serikali ni ya watu na wao ndio wenye kibali cha kusema ndio au hapana na maamuzi yao kuheshimiwa kwa mujibu wa katiba. Kura na chaguo la wengi ndio leseni ya uongozi si vinginevyo jamii ya huko iko imara (strong civil society) kulipigania na kulisimamisha hilo.

Bahati mbaya mataifa 'machanga' hasa ya Kiafrika pamoja na kujaribu kuiga mfumo huo wa utawala bado zimeendelea na kasumba ya watu fulani kupewa uwezo na haki isiyowajibika kwa yeyote ambao huburuza wengine kwa kutumia mwanya wa kutodhibitiwa kikatiba.

Kasumba hizo zimekuwa na matukio ya migogoro ya mara kwa mara, mapambano na hatimaye mauaji. Mifano iko wazi kule Rwanda, Burundi, Angola, Algeria, Congo na kwingineko. Hivi sasa viongozi wa mataifa huru ya kiafrika wako nchini Algeria wakijadili hali hii lakini inastaajabisha mkutano huu kufanyika katika nchi ambayo serikali yake haikuundwa kwa matakwa ya wengi na kiranja wa ukiukaji wa misingi ya haki, amani na utulivu wa jamii!

Nchi yetu hivi sasa inapita katika mkondo ambao kama hawatapatikana watu wenye kujali na kutafakari mustakbali wa jamii, iko hatari kubwa mbeleni. Zipo dalili za wazi zinazoashiria mapigano mabaya ya wenyewe kwa wenyewe. Umaskini na ulafi huenda vikawa vyanzo vikuu. Ukaidi na kutowajibika zikawa chagizo. Chuki, upendeleo, ukandamizaji na dhulma kuwa pambio za mtafaruku huo wa kijamii.

Lakini msingi wa mapungufu hayo ni ukweli kwamba nchi yetu haijawa na muafaka makini wa kijamii. Na zimekuwepo jitihada za makusudi kudumisha hali hiyo! Suala la white paper ni ushahidi mmojawapo!

Kinyume na hali tuliyoileza mwanzo kule Amerika, hapa kwetu tokea taifa 'liundwe' wananchi hawajapata fursa ya kukutana kimakundi, kabila, dini na kadhalika kujadili namna watakavyoishi wakizingatia tofauti walizonazo huku wakisheshimiana kama raia wa nchi moja.

Aidha, katika usimamizi na uendeshaji wa yale yanayohusu maingiliano na mahitajiano hapajawa na fafanuzi, mahakikisho, ukomo na uwajibikaji kwa vyombo au watendaji. Na wala hapajaainishwa haki za wananchi kuurudi usimamizi au utendaji unaokiuka mipaka.

Hali hiyo imetoa fursa kwa watendaji hasa wa vyombo vikuu vinavyounda dola kuifikisha nchi hapa ilipofikia. Hatari kubwa inayonyemelea nchi yetu, ni kwamba wananchi wamechoka na hali hiyo.

Malalamiko yaliyozagaa mijini juu ya hali ngumu ya maisha inayotokana na vipato duni na serikali kushindwa kuboresha huduma mbali mbali, miundo mbinu mibovu, viongozi kuahidi na kusema uongo na kadhalika; rushwa na upendeleo katika vyombo vya sheria na Bunge kuwa mali ya vyama badala ya kujadili mambo ya wananchi, ni ushahidi kwamba jamii yetu, inakanyaga mahali penye mlipuko.

Ni hakika alivyosema kiongozi mmoja mstaafu wa jeshi kwamba duniani kote wananchi ni jeshi hatari linaloweza kuisambaratisha nchi iliyostawi. Ni jeshi baya kuliko lile lenye mafunzo maalum na vifaa bora kambini.

Kauli inaungwa mkono na hali ya machafuko inayoendelea nchini Somalia ambayo huko nyuma ilikuwa na nguvu kijeshi kuliko nchi kadhaa jirani zake lakini pale wananchi waliposema hapana matokeo ni haya ambapo nchi haina serikali, mapigano yanaendelea kwa miaka kadhaa sasa. Jitihada za kusuluhisha kidiplomasia zimekwama, mabavu pia yameshindwa.

Ni busara kubwa kama tungeanza kufikiria mkondo wa historia yetu. Tanzania isifikie mahali wananchi wakaamua kusema basi lolote na liwe, hapatakuwa na kiongozi, raia wa kawaida, mwanajeshi au polisi wa kuweza kuhimili mikiki yake! Nchi itasambaratika kufumba na kufumbua.

Tuache ubinafsi, tuharakishe kupata muafaka wa kweli wa kijamii unaoweza kuiokoa nchi yetu na janga la maafa siku, miezi au miaka michache ijayo.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook