MZALENDO, Jumapili,
Novemba 3, 1985.
RAIS Nyerere amewaomba wazee nchini kumsaidia Rais mteule, Ndugu Ali Hassan Mwinyi kama ambavyo walivyomsaidia yeye wakati wa kudai uhuru na baada ya uhuru.
Mwalimu akizungumza na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam katika sherehe za kuagana nao zilizofanyika jana kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, mjini Dar es Salaam alisema mambo makubwa ya nchi ya kimaendeleo yanayoanzishwa hayawezi kufanikiwa kama hayana baraka za wazee.
"Kama mlivyonisaidia mimi, msaidieni na mwenzangu. Anaihtaji sana msaada wenu", alisema Mwalimu ambaye anastaafu Urais kesho kutwa wakati Ndugu Mwinyi atakapoapishwa kuwa Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano.
Mwalimu ambaye katika hotuba yake alizungumzia kwa kirefu misaada mbalimbali aliyopewa na wazee nchini wakati wa kudai uhuru, alieleza kuwa pamoja na kuwa misingi mizuri imejengwa nchini, matazamio ya wananchi ni makubwa jambo ambalo alisema linamfanya Ndugu Mwinyi awe na kazi kubwa mbele yake.
Aliwashukuru kwa msaada, imani na kuelewa kwao mambo na ushirikiano mzuri waliompa katika miaka 24 ya uhuru wa taifa na pia katika harakati za kuutafuta. "Kila nilipotembea nchini wakati wa kudai uhuru watu wa kwanza walionielewa walikuwa wazee", alisema.
Mwalimu aliwataka vijana nchini kuiga mfano wa wazee hao na pia kufanya kazi za kujitolea ili kuliwezesha taifa kufikia hatua kubwa zaidi ya kimaendeleo.
Akigusia mchango uliotolewa na vijana enzi za kudai uhuru ambao wengi wao hivi sasa ni wazee, Mwalimu alisema Tanzania haiwezi kufanya maendeleo makubwa bila vijana kufanya kazi za kujitolea.
Alisema vijana ndio wengi nchini ni wasomi na wana nguvu na kwamba bila wao kutumiwa kwa kufanya kazi za kujitolea, maendeleo makubwa hayawezi kufikiwa.
Mwalimu aliwakumbusha baadhi ya michango ya vijana wa zamani ya kujitolewa iliyosaidia kupatikana kwa uhuru. "Kazi za vijana wa zamani ilikuwa kufanya kazi za hiari kwa ajili ya TANU na kuimba, alisema.
Aliwataka vijana kuchagua kazi ambazo wanaweza kuzifanya kwa kujitolea ili kusaidia taifa kufikia maendeleo makubwa zaidi.
Katika risala yao kwa Mwalimu, wazee hao walimpongeza Mwalimu kwa uamuzi wake wa kustaafu na kumtaka wakati akiwa Mwenyekiti wa Chama kufanya kila analoweza kukiimarisha Chama. "Chama ndicho kilichotukomboa ... Chama ndicho kilichotukomboa... Chama ni baba na mama", walisema wazee hao.
Miongoni mwa zawadi walizompa Mwalimu katika sherehe hizo ni baiskeli, jembe, panga, kiti na mkongojo.
Leo Mwalimu atapokea maandamano makubwa ya walimu wa mkoa wa Dar es Salaam yatakayoanzia Arnautoglu hadi Ikulu ambako ataagana nao.
Mapema jana Rais Nyerere alikabidhiwa rasmi "nishani ya Mkuu wa nchi" kutoka Chama cha Kimataifa cha Klabu ya Misaada za Lions kutokana na chama hicho kutambua mchango wa Mwalimu katika kuwasaidia binadamu.
Katika sherehe iliyofanyika nyumbani kwake Msasani, mjini Dar es Salaam asubuhi, Mwalimu pia alikabidhiwa shilingi laki moja atakazozitumia kwa ajili ya mradi wowote wa maendeleo jinsi atakavyoona yeye katika eneo lolote nchini.
Mwafrika, Alhamisi
Juni 22, 1961
BWANA Lifa Chipaka alisema jana kwamba bado anaendelea na cheo chake cha Mwenyekiti wa African National Congress. Ripoti iliyotolewa na chama hicho juzi kusema Chipaka hatakiwi kwahiyo ajiuzulu aliita kuwa ni ya uongo mtupu, wala haitambui.
Bwana Chipaka alidai kuwa hiyo Districk Committee iliyosemwa kuwa imemfukuza kazi yeye haifahamu, wala hata kama iko yeye anafikiri kuwa haiwezi kumtoa kazi Mwenyekiti wa chama cha Tanganyika nzima.
Akafyatuka, "Mtemvu lazima atoke yeye katika Congress maana ameharibu jina la chama, alipokuwa akisafiri huko na huko ulimwenguni. Alipokuwa China Mtemvu alijiita Waziri Mkuu wa Tanganyika", alisema Bwana Chipaka. Hapo hapo akatoa bahasha ya barua kutoka China aliyoletewa Mtemvu kwa cheo cha Waziri Mkuu wa Tanganyika.
Aliendelea, "Mimi nilikubaliana na Bwana Mtemvu kuwa niende Unguja, mwenyewe akanipa barua nikampelekea Bwana Ali Muhsin. Nilifanikiwa sana, ndiyo maana sasa Mtemvu ananionea gele.
"Nilipokuwa Unguja nilikuwa kama Mfalme, na sasa Mtemvu hapandezwi na kufanikiwa kwangu huko na Mtemvu anashirikiana na Marijani ili kuniangusha. Wala sipendelei Marijani awe Katibu wa Mtemvu.
Chipaka aliongeza, " Mtemvu alipokwenda nchi za Mashariki, hakufanikiwa kama vile nilivyofanikiwa mimi Unguja. Alipewa vitu vingi lakini aliporudi huku alijifanya kwamba vilikuwa zawadi alizopewa yeye mwenyewe wala hazikutolewa kwa Congress.
Halmshauri Kuu ya chama ilikuwa ikikutana tangu Jumamosi ikimfikiria Bwana Mtemvu, alisema Bwana Chipaka.
Akazidi kueleza, "Nilipokwenda Unguja nilimweleza Bwana Muhsin kuwa sikuwa na kitu, akanipa senti fulani, lakini sasa wakina Mtemvu na Omido wanavitaka hata visenti nilivyopewa Unguja nivitoe kwenye chama. Lakini Mtemvu mwenyewe hakurudi na hata senti moja kutoka nchi za Mashariki.
"Hawawezi kunitoa katika Congress kwa sababu wanachama wote wako upande wangu nami nina kila ushahidi wa haya ninayosema. Hafai
Aliendelea, "Mtemvu hafai kwa uongozi, ndio maana Sanga aliacha chama cha Congress. Katika barua yake ya kuacha kazi Sanga mwenyewe alisema wazi kwamba yeye hawezi kuwa Katibu na Mtemvu kuwa Rais wa Congress, aliona kwamba hawawezi kufanya kazi pamoja".
Naye Bwana Omido Katibu Mwenezi
wa Congress alisema kwamba mashitaka ya Bwana Chipaka hayana msingi wowote.
Alisema kwamba jana usiku habari ya Bwana Chipaka ilikuwa ikifikiriwa na
Halmashauri Kuu ya Congress.
--
|
|