CHAKULA NA LISHE
 
Kumnusuru mtoto na tatizo la utapiamlo
 

Na Mujahid Mwinyimvua
 

KATIKA makala hii neno utapiamlo linamaanisha ile hali ambayo mwili haupati virutubisho vya kutosha na vilivyosahihi kutoka kwenye vyakula anavyokula mtu. Vile vile, mwili ukiwa unapata virutubisho (nutrients) vingi kuliko mahitaji kutoka kwenye vyakula, hali hiyo nayo hujulikana kama utapiamlo.

Katika nchi maskini kama Tanzania, utapiamlo unaosumbua zaidi ni ule wa mwili kutopata virutubisho vya kutosha na vilivyosahihi. Kwa mfano, watu wengi hawapati vyakula vya kutosha vinavyoupa mwili nishati (nguvu), protini, vitamini, nyuzi nyuzi, na kadhalika.

Nchini Tanzania tatizo la utapiamlo wa upungufu wa virutubisho mwilini ni kubwa zaidi kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Na kundi hilo la watoto ndilo linaloongoza kwa idadi kubwa ya vifo vinavyosababishwa na tatizo la utapiamlo.

Makala hii inaelezea hatua za msingi za kuchukuliwa ili kupunguza kama si kuondoa kabisa tatizo la utapiamlo na hatimaye kupunguza idadi ya vifo kwa kutumia elimu hii aliyotupa Mungu Muumba.

Kwanza, mtoto mwenye umri wa siku moja hadi miezi minne anyonyeshwe maziwa ya mama pekee. Ndiyo kusema watoto wenye umri huo, wasipewe vyakula zaidi ya maziwa ya mama. Kama mama aliyejifungua matiti yake hayatoi maziwa na hakuna mama mwingine atakayeweza kumnyonyesha mtoto huyo mchanga maziwa ya mama, hiyo ni dharura.

Katika hali kama hiyo, mtoto lazima anyonyeshwe maziwa ya kopo na wala siyo yale ya wanyama anayokamua mtu kwa mnyama wake. Hii ni kwa sababu, maziwa ya kopo ya watoto, yameandaliwa kwa watoto lakini yale yasiyotengenezwa kiwandani yanavirutubisho ambavyo siyo saizi ya afya ya mtoto mwenye umri chini ya miezi minne.

Hata hivyo, wananchi hasa wazazi wasijewaelewa kuwa makala hii inawahimiza wao kuwanyonyesha watoto maziwa ya kopo. Tunachosema ni kuwa, kama hakuna uwezekano wa kupata maziwa ya mama, afadhali mtoto anyonyeshwe maziwa ya kopo licha ya ukweli kuwa mtoto huyo anaweza kupata matatizo ya kiafya, kuliko kutonyonyeshwa kabisa. Bila kunyonyeshwa kabisa mtoto huyo anaweza kufariki dunia.

Pili, mtoto mwenye umri wa zaidi ya miezi minne au sita, apewe vyakula zaidi vyenye protini. Vyakula hivyo ni kama vile nyama, maharage, samaki, maziwa ya wanyama na kadhalika.

Tatu, mlishe mtoto wa miezi minne au zaidi chakula chenye nishati (energy) kwa wingi kwa kuongeza kwenye chakula cha mtoto, kiasi cha kijiko kimoja cha vyakula kama mafuta, karanga, sukari, asali, ufuta au unga wa kimea.

Nne, mtoto lazima apewe mboga za majani na matunda mchanganyiko kila siku. Hakuna tunda lenye aina zote za virutubisho, kwa hiyo ni vema mtoto apewe matunda mchanganyiko ili aweze kupata virutubisho vyote muhimu vinavyopatikana katika matunda.

Kwa mfano, asubuhi unampa chungwa, mchana unampa papai, jioni unampa ndizi na usiku unampa embe. Kesho yake unampa matunda mengine. Kama hakuna aina nyingine usiache kumpa aina ile uliyompa jana yake. Zaidi ya hayo, mtoto lazima apewe chakula safi na maji safi yaliyochemshwa.

Pia mazingira ya nyumba, vyombo na nguo lazima yawe safi. Na mtoto aogeshwe mara kwa mara.

La mwisho, mtoto lazima apelekwe kliniki kwa ratiba iliyopendekezwa na wataalamu wa afya.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook