MASHAIRI
 

Kigwanda cha kijani!

Hasira zimenipanda, chini sitaki kukaa,
Nachana changu kigwanda, sikitaki kitambaa,
Moyoni nishakiponda, kibaya kimefubaa,
“Chaa”, “chaa”, nakichana chaa, kigwanda cha kijani.

Kimeukuwa cha kihuni, walevi washinda baa,
Watu walo majununi, watendao yasofaa,
Natupa sikitamani, Kiko mwana wa Ulamaa,
“Chaa”, “chaa”, nakichana chaa, kigwanda cha kijani.

Hamu kimeshanishinda, sinacho tena tamaa,
Chanuka kama kidonda, che funza wanozagaa,
No mana mwenye nakonda, kimenijaza balaa,
“Chaa”, “chaa”, nakichana chaa, kigwanda cha kijani.

Chake rihi ya Rwanda, damu kimetapakaa,
Japo kimetoka Ndanda, nchini sitakivaa,
Ndani ya changu kibanda, sikipi tena wasaa,
“Chaa”, “chaa”, nakichana chaa, kigwanda cha kijani.

Nikichome na motoni, kwa mafuta yake taa,
Kitoke pangu machoni, kiwe jivu la mkaa,
Linitoke la moyoni, dukuduku lilojaa,
“Chaa”, “chaa”, nakichana chaa, kigwanda cha kijani.

Nangoja hapo mwakani, rizuke Jiji la Daa,
Nitafute madukani, chenye rangi ya kung’aa,
Cheupe si cha kijani, kile ninokikataa,
“Chaa”, “chaa”, nakichana chaa, kigwanda cha kijani.

Mwisho mbele sitokwenda, nakichana chana chanaa,
Bado niko njia panda, safari naiandaa,
Wenzangu mnokipenda, oneni yangu fatwaa,
“Chaa”, “chaa”, nakichana chaa, kigwanda cha kijani.

Idd S. Kikong’ona,
Morogoro.



Hata zawadi hapewi

Mtu anayeropoka, hata zawadi hapewi,
Umaarufu utang’oka, watu hawakuelewi,
Na moto unaukoka, kuwaka hauchelewi,
Hata zawadi hapewi, mtu anayeropoka.

Matope anajipaka, amejenga usodawi,
Tabia yake vilaka, ubora haujengewi,
Halekebiki miaka, kwa ukweli hauelewi,
Hata zawadi hapewi, mtu anayeropoka.

Akili yake kichaka, ujinga umesitawi,
Anazidi kujipaka, husikia haelewi,
Amezoea kudaka, na kwa watu haridhiwi,
Hata zawadi hapewi, mtu anayeropoka.

Mwenye ameridhika, hajijui hatakiwi,
Asemayo si hakika, hawezi kufanikiwi,
Hapo alipo pashika, ukweli haafikiwi,
Hata zawadi hapewi, mtu anayeropoka.

Semanae ukacheka, kama mnyama haliwi,
Ubaya umteka, na wala hajaribiwi,
Na pia kazoeleka, umwambia aambiwi,
Hata zawadi hapewi, mtu anayeropoka.

Wajuzi wanagutuka, haramu hairudiwi,
Mipaka imeivuka, kila sehemu ni tawi,
Ni vema ukaepuka, hasikikii ni kiziwi,
Hata zawadi hapewi, mtu anayeropoka.

Kaditama nimefika, yabidi apigwe kiwi,
Amezidi kujipika, ajulikanavyo ziwi,
Hawezi kuaminika, kwa umma agombaniwi,
Hata zawadi hapewi, mtu anayeropoka.

(Jua la usiku)
Ramadhani M. Nyembe (Siri ya Nyumba),
S.L.P. 943,
Dodoma.


Ewe dada Islamu
 

Bismillahir naanza, kwa jina lake Rabuka,
Tena kanipa uweza, kusoma na kuandika,
Nia ni kuwaeleza, wasia wangu hakika,
Acha kujidhalilisha, ewe dada Islamu.

Islamu wa kisasa, kwa kweli wanishangaza,
Waichukua mikasa, nakupita itangaza,
Waicheza kwasa kwasa, njiani bila kuwaza,
Acha kujidhalilisha, ewe dada Islamu.

Amekuwa hayawani, hujuwi kikudhurucho,
Kila onacho njiani, wakitaka uwe nacho,
Yakushinde miwani, yakaapo kwenye jicho,
Acha kujidhalilisha, ewe dada Islamu.

Yarabi katuumbia, sura za kila namna,
Sie twajiharibia, twajiweka kwa namna,
Ngoziye kuikoboa, nazo nyuso kuzichuna,
Acha kujidhalilisha, ewe dada Islamu.

Hivi huna hata haya, kukataa bara lako,
Vipi wale wa Ulaya, wakitaka kuja kwako,
Wakimbilia Ulaya, na nywele kama ukoko,
Acha kujidhalilisha, ewe dada Islamu.

Mashindano uremboni, ndiyo hayo mwayaweza,
Utakuta gazetini, uchi mmejilegeza,
Hata huko mashuleni, nao pia wajikaza,
Acha kujidhalilisha, ewe dada Islamu.

Acheni mfananisho, kati yako na kondoo,
Yaja siku ya kitisho, ukate ndugu na koo,
Kikutoke na kijasho, hiyo siku ya kitisho,
Acha kujidhalilisha, ewe dada Islamu.

Nane beti namaliza, kalamu naweka chini,
Namshukuru muweza, kuniweka akilini,
Kanijalia uweza, unifae maishani,
Acha kujifananisha, kati yako na wanyama.

Asha Juma,
Msamala Muslim Seminary Sec. Sch.,
S.L.P. 985,
Songea.

--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook