TUITION
 
Elimu ya Dini ya Kiislamu shule za Sekondari
Somo la Fiqh Form IV:
Upeo mpana wa Uadilifu wa kiislamu
 

Kutokana na mafundisho ya Uislamu kuwa matokeo ya mitihani na majaribio tunayopewa na Mwenyezi Mungu hayatajulikana katika ulimwengu huu bali yatajulikana huko Akhera na kwamba mafanikio au hasara ya kweli ni ile atakayoipata mtu huko Akhera, ni dhahiri kuwa mtazamo wa mtu juu ya maisha haya na mambo yake hubadilika kabisa.

Kwa sababu ya imani hii Muislamu hayahesabu matokeo yanayojidhihirisha katika ulimwengu huu kama ndio kipimo cha kweli na cha mwisho cha wema na uovu, zuri na baya, kweli na uwongo, kufanikiwa na kufeli, na hivyo basi kuzitii kwake kanuni za uadilifu hakutegemei matokeo yanayojidhirisha hapa duniani.

Mtu mwenye msimamo huu ataendelea kusimama imara katika kuzitii sheria za uadilifu bila kujali kama kufanya hivyo kutaletea furaha au majonzi, au kama atapata manufaa ya kidunia au la. Hii haina maana kuwa atakuwa hazingatii matokeo ya vitendo vyake katika dunia hii, la. Bali matokeo haya katu hayatakuwa kipimo cha kurekibishia mwenendo wake wa tabia, yaani uchaguzi wake na mwenendo wa kuufuata hautategemea manufaa au hasara atakayopata hapa duniani. Kwa mfano tuseme daktari ameajiriwa kutibu watu. Kama daktari huyo atakuwa anashikamana na mafundisho ya Uislamu juu ya uadilifu katu hatakuwa tayari kuiba au kwenda kuuza nje dawa alizokabidhiwa kutibia wagonjwa wala hatawadai wagonjwa rushwa ya aina yoyote hata kama anaweza kufanya hayo na asikamatwe. Hatafanya hayo hata kama hali yake ya maisha ni duni sana. Hatafanya hayo hata kama anajua kuwa wanaofanya hivyo wanapata pesa nyingi sana zinazowawezesha kujenga majumba kwa muda mfupi, wanakula vizuri na kustarehe. Hatafanya hayo kwa sababu kutajirika hapa duniani siyo kipimo chake cha kweli na cha mwisho cha kufuzu au kufeli. Kwa sababu hiyo uadilifu katika Uislamu si kitu kinachobadilika kila uchao

Jukumu la Binaadamu

Matokeo ya mafundisho ya Uislamu juu ya ukhalifa wa binadamu ni kwamba, binaadamu anatakiwa kutumia vipawa vyake vyote na rasilimali zote alizopewa kwa mujibu wa maamrisho na mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Hii ina maana kuwa binaadamu atakuwa anaukana ukhalifa wake iwapo hatakuwa tayari kutumia raslimali zote hizo kama alivyoagiza Mwenyezi Mungu. Si hivyo tu bali pia atakuwa anaukana ukhalifa huo iwapo ataacha kuvitumia vipawa na raslimali hizo, na hivyo kuupuuza wajibu wake kama khalifa. Aidha kwa mujibu wa mafundisho haya maisha ya jamii yanaendeshwa kwa namna ambayo binadamu wote, yaani makhalifa wote wa Mwenyezi Mungu wanashirikiana katika kutekeleza majukumu yao, na isiwezekane kabisa chini ya utaratibu huo kwa mtu mmoja au kikundi cha watu kuwanyang'anya wengine ukhalifa wao. Yaani makhalifa wote wa Mwenyezi Mungu wanashirikiana katika kutekeleza majukumu yao, na isiwezekane kabisa chini ya utaratibu huo kwa mtu mmoja au kikundi cha watu kuwanyang'anya wengine ukhalifa wao.

Kwa kuwa hadhi na nafasi ya binadamu ni ile ya ukhalifa basi lengo la maisha yake halina budi kuwa ni kusimamisha Ufalme wa Mwenyezi Mungu hapa duniani na hivyo shabaha ya jitihada zake zote za uadilifu iwe ni: kusimamisha sheria ya Mwenyezi Mungu katika lile eneo ambalo dhamana ya uendeshaji wake amekabidhiwa yeye na Mwenyezi Mungu; kujenga na kudumisha mazingira ambayo amani, haki na ihsani vitastawi; kuzuia na kuondosha uovu na ufisadi katika sura zake zote; na kujenga ule mwenendo ambao Mwenyezi Mungu anapenda kuuona ukistawi miongoni mwa waja wake.


Mgawanyo wa mali katika Uislamu
 

UISLAMU unasisitiza kuwa zaidi ya kuchuma, kumiliki na kusambaza mali, mgawanyo pia uwe wa haki katika jamii ili kujenga udugu, amani na utulivu wa kweli. Na katika kuhakikisha hilo mfumo wa uchumi wa Kiislamu (Iqtisad) unatumia njia zifuatazo:

1. Zaka

(i)Kilugha, neno zaka lina maana mbili (a) Utakaso na (b) ustawi. Hivyo Zaka ni Ibada inayochangia sana katika kuleta uadilifu na ustawi wa jamii kiuchumi na hata kisiasa.

(ii) Zaka katika Uislamu ni taasisi maalumu na imesisitizwa katika Qur'an. Aya zipatazo 80 zimeitaja Zaka pamoja na Swala. Zaka ina upeo mpana sana na ina husisha vipengele vingi kama vile:

(a) Kijamii - Zaka ni kama bima ya jamii inayowahakikishia wakazi hifadhi ya kiuchumi endapo watapata matatizo kama ya umasikini au maafa. Zaka pia huondosha chuki na migogoro ya kitabaka na kujenga hisia za kujihisi kitu kimoja.

(b) Kisaikolojia, Zaka inawalea watu katika moyo wa kuhurumiana na kusaidiana.

(c) Kiuchumi - Zaka ni njia mojawapo ya kupambana na tatizo la umaskini. Tatizo hili linazikabili nchi zote na Uislamu unalenga katika kuondoa umaskini pasi na jitihada za watu binafsi. Uislamu haupiganii usawa badia wa kuwa kipato cha kila mtu kiwe sawa na mwingine wala Uislamu hauinyamazii hali ya wengine watumie na kusaza wakati wengine wanaendelea kutaabika kwa kushindwa kujipatia mahitaji muhimu. Tofauti za kimapato, vipaji na uwezo zitakuwepo katika jamii, lakini pengo la tofauti hiyo lisiwe kubwa sana.

(d) Kwa maumbile yake, Zaka huwahimiza watu kuweka vitega uchumi na kuzalisha mali na kupiga vita tabia ya kuhodhi mali. Hii ni kwa sababu Zaka hutozwa kwa kipato kilichokaa mwaka mzima bila kutumika.

2. Sadaka

Hisia za kuhurumiana na moyo wa kusaidiana kama ndugu zinazomsukuma mtu kutoa zaka kwa kutaraji kupata radhi za Allah ndizo hizo hizo zinazomsukuma mtu kutoa sadaka. Hivyo tofauti kati ya zaka na sadaka haipo katika lengo la kutoa bali katika wajibu wa kutoa. Zaka ni wajibu kutoa na sadaka ni amali iliyokokotezwa sana japo haikuwekewa kiwango na muda wa kutoa. Hutolewa kulingana na haja Misingi ya kutoa sadaka ni ile ile ya kuhurumiana na kusaidiana kama Allah alivyoagiza katika Qur'an:

"Na saidianeni katika wema na ucha-Mungu, wala msisaidiane katika dhambi na uadui" (5:2).

"Mfano wa wale wanaotoa mali zao katika njia ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa punje moja iliyotoa mashuke saba; ikawa katika kila shuke pana punje mia., Na Mwenyezi Mungu humzidishia amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni mwenye wasaa mkubwa na Mwenye kujua." (2:261).

Aidha, Mtume (s.a.w.) amesisitiza katika hadithi nyingi sana umuhimu wa kutoa sadaka. Katika hadithi iliyosimuliwa na Bukhari, Muslim, Ahmad na At-Tirmidh, Mtume (s.a.w.) amesema mtu asiyewahurumia watu hatahurumiwa na Allah. Na katika hadithi iliyosimuliwa na Attabarani na Baihaqi, Mtume (s.a.w.) amesema: Naapa kwa Allah si muumini yule anayelala akiwa kashiba na ilhali jirani yake kalala na njaa. Na katika hadithi iliyosimuliwa na Al-Hakim, Mtume (s.a.w.) amesema ikiwa wakazi wa eneo fulani (kama vile mtaa) wakiamka asubuhi na ilhali mmoja wao ana njaa basi Allah hujitenga nao.

Matukio maalum yanayohitaji kutolewa kwa sadaka Baada ya kumaliza mfungo wa Ramadhani kutoa Zakatul Fitr ni lazima. Zakatul Fitr kiwango chake ni kilo 21/2 za chakula aghlabu katika mji huo kama vile mchele au ngano. Na mtu hutoa kiasi hicho kwa ajili yake mwenyewe na hutoa tena kiasi hicho hicho kwa kila mtu anayemhusu kumlisha katika familia yake. Hivyo atamtolea pia mkewe, na wanawe wote na wazazi wake iwapo anakaa nao na hawana uwezo.

Tukio la pili ni siku ya kuvuna mazao shambani, Mwenyezi Mungu ameagiza siku hiyo mtu atoe baadhi ya mazao yake na awape maskini, jamaa na majirani zake aliposema katika Qur'an:

"Naye (Allah) ndiye aliyeumba miti inayoegemezwa (katika chanja katika kuota kwake na isiyoegemezwa na (akaumba) mitende na mimea ya matunda mbali mbali, na (akaumba) mizaituni na mikomamanga inayofanana na isiyofanana. Kuleni matunda yake inapotoa matunda; na toeni haki yake siku ya kuvunjwa kwake (kwa kuwapa maskini na jamaa na majirani na wengineo) Wala msitumie kwa fujo, hakika Yeye (Allah hawapendi watumiyao kwa fujo." (6:141).

Tukio la tatu ni wakati wa ndoa, Kuoana ni jambo lililohimizwa sana katika Uislamu. Hivyo Uislamu unasisitiza kuwa watu wasaidiane sana katika jambo hili. Wanazuoni wengi wanasema kuwa iwapo mtu anao uwezo wa kuoa lakini hapa mwanzo anakabiliwa na matatizo ya kifedha Hazina ya serikali ya Kiislamu (Baitul Maal) itumike kumsaidia. Wakati wa Ukhalifa wa Umar vijana kama hao walikuwa wakisaidiwa. Katika kuonyesha ubora wa ndoa Allah amesema:

"Na waozeni wajane miongoni mwenu (waungwana) na walio wema katika watumwa wenu (wanaume) na wajakazi wenu, kama watakuwa mafakiri Allah atawatajirisha katika fadhila zake; na Allah ni Mwenye ni Mwenye wasaa" (24:32).

Tukio la nne ni iwapo mtu atapata wageni. Uislamu unamtaka mtu awakarimu wageni wake. Katika Hadithi iliyosimuliwa na Bukhari na Muslim, Mtume (s.a.w.) amesema: Yule anayemwamini Allah na siku ya mwisho awe mkarimu kwa wageni wake. Kwa mchana mmoja na usiku afanye takrima maalum. Kwa siku tatu zinazofuata afanye takrima ya kawaida na zaidi ya hapo ni sadaka ya hiari.

Tukio la tano ni wakati wa kugawa urithi, iwapo watakuwawepo watu mafakari wakati huo wa kugawa basi wapewe chochote, kwani Allah anasema:

"Na wakati wa kugawanya wakihudhuria jamaa na mayatima na maskini, wapeni kitu katika hayo (mali ya urithi) na waambieni kauli njema." (4:8).

Tukio la sita ni agizo la Allah na kusaidiana kwa hali mbali mbali hasa majirani.

Tukio la saba ni wakati wa uzazi. Kama ambavyo Uislamu unahimiza ndoa ndivyo pia unavyothamini malezi ya watoto. Kihistoria ni Uislamu ndio ulioanzisha utaratibu wa kutoa malipo fulani maalum kwa familia zenye watoto wachanga.

Mfumo wa kutoa ruzuku kwa familia

Hivi leo ziko baadhi ya serikali duniani ambazo hutoa msaada wa pesa kwa familia zenye watoto wachanga. Huko Kanada kwa mfano upo utaratibu wa kutoa msaada wa pesa kwa kila mtoto aliyezaliwa na kama watoto wakifikia umri wa miaka 18 na bado wanasoma kiwango cha pesa wanachopewa huongezwa.

Utaratibu huu ulianza katika karne ya 7 wakati wa ukhalifa wa umar. Umar alianzisha mfumo wa kutoa dirham 100 kwa kila mtoto aliyezaliwa na kiwango hicho kiliongezwa kadiri mtoto alivyokua.

Hivyo mfumo wa kutoa ruzuku kwa familia ni moja ya sadaqa zitolewazo katika mfumo wa uchumi wa Kiislamu.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook