Na Dkt. Abdallah J. Saffari
Katika makosa karibuni yote ya jinai, mtu atatiwa hatiani tu kwa kosa ambalo amelitenda kwa kudhamiria. Hivyo kutokuwa na dhamiri ya kutenda kosa linalodaiwa ni utetezi madhubuti wa makosa yote ya jinai isipokuwa yale tu ambayo hutendeka hata bila kuwa na dhamiri ya kuyatenda (F. 10, Kanuni ya Adhabu, i.h.j.). Kwa hiyo ajali ni aina moja ya utetezi chini ya fungu hili.
Makosa ya kweli
Tumeona punde tu kuwa imani ya kweli juu ya itibari ya mali au kitu fulani ni utetezi dhidi ya makosa ya wizi. Kwa upande mwingine, makosa ya kweli yanayotokana na imani ya mshitakiwa ni utetezi pia dhidi ya makosa ya jinai (F.11, Kanuni ya Adhabu, i.h.j). Utetezi huu ni mpana zaidi kwa vile unajumuisha aina zote za makosa ya jinai. Mathalan mtu hawezi kuwa na hatia kwa kumwua mtu aliyeamini ni nguruwe anayeharibu mazao yake shambani. Masharti ya utetezi huu ni lazima kwanza imani juu ya makosa yanayohusika iwe ya kweli na kuyakinika. Kwa mfano sio yakini kudhania mtu kuwa tembo.
Hata hivyo nyakati nyingine makosa ya kweli yanaweza yasiwe utetezi. Mfano mzuri ni makosa dhidi ya usalama barabarani. Dereva anayesababisha ajali kwa kuamini tu kuwa breki zake ni nzima kumbe sio nzima anaweza kupatikana na hatia. Anaweza tu kujitetea iwapo breki zake hizo zilikuwa nzima alipoanza safari zikaharibika katikati ya safari kabla au wakati wa ajali bila ya yeye kufahamu mapema. Ama sivyo utetezi huu ungetumiwa kama kisingizio na kuwaponya watu wengi wenye silka ya uzembe.
Wazimu au Kichaa
Mtu hatakuwa na hatia kwa kufanya au kutofanya kitendo iwapo wakati wa kufanya au kutokufanya kitendo hicho, kutokana na ugonjwa wa akili, ameshindwa kuelewa analolitenda au kujua kwamba ilikuwa ni vibaya na hakustahili kufanya au kutokufanya kitendo kinachosababisha (F.13, Kanuni ya Adhabu, i.h.j).
Hivyo utetezi una masharti matatu kuukamilisha. Kwanza ni kuwepo kwa maradhi ya akili yaani wazimu au kichaa. Pili athari ya ugonjwa huo wa akili imnyime uwezo wa kuelewa kitendo anachokifanya au kutokifanya. Au, tatu, ugonjwa huo wa akili umnyime uwezo wake wa kujua kuwa hatakiwi au kustahili kufanya au kutokufanya kitendo hicho. Sharti hili linahusiana na kutofahamu ubaya wa kitendo kinachohusika.
Ni dhahiri basi kuwa sio kila aina ya wazimu au kichaa kinaweza kuwa utetezi dhidi ya kosa linalodaiwa. Ugonjwa huo wa akili, uwe kichaa au wazimu, sharti usababishe athari katika ufahamu wa mshtakiwa na kumfanya asitambue analolitenda au hata kama analitambua, asielewe ubaya wa kitendo hicho.
Katika shauri maarufu la R. v Said Mwamwindi (1972 H.C.D.n.) mshitakiwa akikabiliwa na shitaka la kumwua Wilbert Kleruu, aliyekuwa Mkuu wa Moa wa Iringa kwa wakati huo. Mshitakiwa alijitetea kuwa alipokuwa anamwua marehemu Kleruu alirukwa na akili akapotewa na fahamu ya kuweza kuelewa kile alichokuwa anakitenda. Jaji Onyiuke alikataa hoja hiyo kwa kutilia maanani kwamba baada ya mshitakiwa kughadhibishwa ndipo alipokwenda ndani kuchukua bunduki ambayo aliitumia kumwua marehemu. Ushahidi huo ulidhihirisha haja na hivyo fahamu timamu ya lile alilokuwa analitenda. R. v. Doris Liundi (1980 I.R.T. n. 107) ni shauri jingine maarufu ambapo mahakama yalikataa dai la mshitakiwa kuwa alikuwa hajui analolitenda wakati alipowanywesha sumu na kuwaua watoto wake watatu. Ushahidi wa kununua na kutayarisha sumu yenyewe pamoja na kumkataza mtumishi kuwapa watoto hao maziwa ambayo yangepunguza athari ya sumu, vilitosha kuthibitisha fahamu timamu za mshitakiwa juu ya kitendo chake. Na barua aliyoandika kwamba mumewe asipewe bughudha wala kusumbuliwa kutokana na vifo hivyo ilidhihirisha zaidi kwamba alielewa ubaya wa kitendo hicho chake. Kwa sababu hizo hizo mahakama ya Rufani ya Tanzania yaliitupilia mbali rufaa ya mshitakiwa (R.v. Agnes Doris Liundi, 1980 I.R.T. 107).
Kwa upande mwingine kuna msururu wa mashauri ambapo washitakiwa wameachiliwa huru kutokana na utetezi wa ugonjwa wa akili (Kwa mjadala wa utetezi huu soma Saidi Mwamwindi v. R. i.h.j na R.v. Agnes Liundi i.h.j).
Utetezi huu ni dhidi ya makosa yote ya jinai ingawa aghalabu hudaiwa na kutumika kwenye mashauri ya mauaji.
Tofauti na aina nyingine za utetezi ambazo mahakama inaweza kuzitilia maanani bila ya kudaiwa na mshitakiwa, ni lazima mshitakiwa mwenyewe adai kuwa mpungufu wa akili. Haja hii inatokana na dhana kwamba kila mtu ana akili timamu mpaka athibitishwe vinginevyo (F. 12, Kanuni ya Adhabu, i.h.j). Wajibu huu wa kuthibitisha upungufu huo wa akili umo mikononi mwa mshitakiwa mwenyewe. Hata hivyo, kutokana na matatizo yanayoambatana na asili ya ugonjwa wa akili tumeona katika sura ya pili kwamba kuna utaratibu unaoyapa mahakama na hata upande wa mashitaka uwezo wa kuchunguza iwapo mshitakiwa ana akili timamu mara tu wanapoona dalili au kutilia mashaka akili ya mshitakiwa.
Kwa jumla utetezi huu umesababisha, na bado unasababisha matatizo kadhaa wa kadhaa. Tatizo kubwa kupita yote ni; iwapo mshitakiwa ni kichaa kwa mujibu wa sheria.
Watu wengi ambao wanaonekana kuzurura mitaani nusu uchi wanaweza kabisa kuelewa wanayoyatenda na pengine hata ubaya na uzuri wake. Hivyo wakati ambapo madaktari wa akili wanaweza kuwaona watu hao ni vichaa mahakama yanaweza kuwahukumu kuwa ni wenye ufahamu wa yale wayatendayo kiasi cha kuwajibika nayo.
Kwa upande mwingine, pengine kwa mastaajabu ya wengi, watu ambao huonekana wana akili timamu huachiwa kwa matendo waliyoyafanya kwa kuonekana hawaelewi wayatendayo. Aghalabu washitakiwa hao ni wale wanaorukwa na akili kwa vipindi vifupi vifupi.
Ili kupata ushahidi thabiti kuhusiana na akili ya mshitakiwa maoni ya wataalam ya maradhi ya akili hupewa hadhi kubwa. Lakini maoni hayo, japo yawe ya kuheshimika kiasi gani, sio lazima yakubaliwe na kufuatwa na mahakama. Na hivyo basi katika mashauri mengi tatizo ambalo limejitokeza ni mgongano wa maoni ya madaktari kwa upande mmoja na wanasheria kwa upande mwingine katika kubainisha iwapo, kwa mujibu wa sheria, mshitakiwa ni kichaa au la. Mathalan katika shauri la R. v. Agness Doris Liundi ( R.v. Agnes Doris Liundi, i.h.j) mahakama yaliona muhali kuyaafiki maoni ya Daktari wa vichaa, Dakta Hauli, licha ya kwamba yeye alikuwa ni bingwa wa vipeo vya juu katika fani hiyo (K.h.j).
Shauri la The Ripper (Katika shauri hilo Mwingereza mmoja aliua idadi kubwa ya wanawake akidai alikuwa akitekeleza amri ya Mungu kuondoa wanawake malaya. Wakati wa kesi iliposikilizwa alidai kuwa wakati wa mauji hayo alikuwa mgonjwa wa akili) ni mfano mwingine mzuri wa mgongano wa maoni baina ya wanasheria na madaktari. Mshitakiwa katika shauri hilo kwa kukusudia, alishitakiwa kuwaua, kwa namna inayofanana, wanawake zaidi ya kumi na tatu. Akitoa utetezi wake alidai alikuwa sio timamu wa akili kwa vile wakati huo wote aliamini kwamba wanawake hao aliowaua, wengi wao akiwa alifanya nao mapenzi, ni malaya.
Na kwamba Mungu alimtuma
kuwaua wanawake hao ili kuisafisha dunia na uchafu wao. Upande wa utetezi
uliita madaktari wengi wastahiki waliobobea katika fani ya maradhi ya akili
(wengine maprofesa wa vyuo vikuu) kuthibitisha kauli yaani utetezi wa mashitakiwa.
Upande wa mashitaka nao uliita madaktari wake kupinga nadharia hiyo ya
utetezi. Hivyo vikazuka vita baina ya fani za sayansi ya maradhi ya akili
- mja ikimwona mshitakiwa punguani na nyingine, kwa ushahidi wa kisayansi
vile vile, ikamwona mshitakiwa timamu. Lakini, kama ilivyosemwa, mahakama
ndiyo mwamuzi wa mwisho. Hata hivyo sio vigumu kuona namna ambayo, katika
mazingira kama hayo ya mgongano wa ushahidi wa kisayansi, inavyoweza kuwa
vigumu kuelewa kwa usahihi iwapo mshitakiwa, kwa mujbu wa sheria, ni kichaa
au la. Wakati mwingine mahakama huweza kukanganyika zaidi (kutokana na
ushahidi wa kitaalamu) badala ya kurahisisha uamuzi wake juu ya suala hilo.
--
|
|