Maoni yetu
 
 
Serikali kuitema hoja yake Bungeni; inatuambia nini?
 

HOTUBA ya Wizara yoyote haiendi Bungeni kama hoja ya Waziri husika. Haiangalii sura, kabila wala dini ya Waziri. Bali huenda kama hoja ya serikali ikizingatia maslahi na matarajio ya serikali na nchi.

Ikishaandaliwa na Katibu Mkuu, hotuba huwasilishwa kwa Kamati ya Makatibu Wakuu wa Wizara zote. Mwenyekiti wa Kamati hiyo ni Katibu Mkuu ofisi ya Rais.

Hapo hujadiliwa na kuwekwa sawa kabla ya kupelekwa kwenye Baraza la Mawaziri ambapo Mwenyekiti wake ni Rais mwenyewe. Ikitoka hapo ndipo huenda Bungeni ikiwa ni hoja ya serikali isiyoangalia dini, sura wala kabila la Waziri, bali sera, mwelekeo na ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala. Ndio maana mara kadhaa Waziri Mkuu kama kiongozi wa shughuli za serikali Bungeni hulazimika kusimama kutetea hoja za Mawaziri kwani zile si hoja zao bali ni za serikali.

Hatuna wasiwasi na ukweli kwamba hotuba ya Mhe. Kapuya ilifuata mlolongo huo na kwamba alichokuwa anazungumza Bungeni alikuwa anaiwakilisha serikali. Wasiwasi wetu na linalotushangaza ni huu msimamo wa serikali kupata kigugumizi na kukiuka ada yake. Vipi lile jukumu la Waziri Mkuu kutetea hoja za serikali Bungeni liote mbawa na kuyeyuka ghafla!

Je; serikali ilifanya makusudi ili itoe fursa kwa Wabunge kumsulubu Waziri Prof. Kapuya au ilikuwa ni mpango wa serikali kutumia Bunge kuhalalisha msimamo wake juu ya swala la Ijumaa kwa wanafunzi!

Hotuba ya Waziri Kapuya ilizingatia mambo kadhaa ya msingi. Kwanza ni kutekeleza Katiba kwamba watu wana uhuru wa kuabudu (Kf. 19(1). Pili, serikali haiwaingilii watu katika dini zao (Kf. 19(2).. Tatu, ambayo ni katika kuitekeleza Katiba hiyo hiyo watu wasibaguliwe kwa kabila zao, rangi zao, dini zao, jinsia au mahali watokapo (Kf. 13(2) (3) (4) (5) ).

Na hoja nyingine ni kwamba kama wapo Watanzania waliopewa siku mbili kamili (masaa 48) katika wiki kufanya 'sala' zao kuu, Watanzania wengine nao wana haki ya kupata masaa mawili kuhudhuria swala yao kuu kwa wiki kwa mujibu wa dini yao.

Kuwapa baadhi ya wananchi masaa 48 waabudu, wenye kuhitaji masaa mawili ukawanyima ni unyanyasaji, ubaguzi, kutotenda haki na kuwafanya baadhi ya raia kuwa si kitu bali daraja la kupuuzwa lisilostahili kusikilizwa wala kupewa stahiki yake. Na hili ndilo alilolipigia kelele Mhe. Rais Mkapa kwamba yeye binafsi asingependa kuona baadhi ya watu wananyanyaswa na kujihisi daraja la pili katika Tanzania hii.

Je, kimya cha Mhe. Waziri Mkuu Bw. Frederick Sumaye Bungeni wakati Wabunge wakiushambulia Uislamu na kupiga makofi ni salamu toka kwa Mhe. Rais kuwa msimamo wake umebadilika! Au ni kielelezo kuwa msimamo wa Mkuu wa shughuli za serikali bungeni ni tofauti na ule wa serikali yenyewe!

Hatudhani kwamba wapo Wabunge ambao hawajui kuwa katiba ya nchi haiwazuii watu kufuata dini zao. Wala hatudhani kuwa wapo Wabunge ambao hawajui kuwa Katiba ya nchi hairuhusu watu kunyanyaswa au kubaguliwa kutokana na dini zao.

Lakini tujaalie kuwa wapo ambao wanayaangalia kwa upofu na uziwi maelekezo ya Katiba pale linapokuja suala la Waislamu. Hawa ndio wale walioleta kejeli na kushangilia bungeni, hali inayopandikiza chuki na kustawisha ufa baina ya wananchi. Vipi hata hapo Waziri Mkuu asione umuhimu wa kuingilia kati; au kwa vile waliokuwa wanakejeliwa ni Waislamu! Hawa wanaokejeliwa na kuambiwa kuswali Ijumaa ni udini si ndio wale wale mnaohudhuria hafla zao na hata Maulid yao na kudai kwamba hamna chuki nao!

Waislamu walipouliwa pale Mwembechai baadhi ya Wabunge walimuomba Mhe. Spika kwamba Kamati ya Bunge ya Mambo ya Katiba na Sheria ilitazame suala hili. Mhe. Spika alikataa kwa madai kuwa hakuna fedha. Sasa inatujia hata kama fedha zingekuwepo kwa Wabunge hawa kusingefanyika chochote. Je; wananchi hawa waendelee kulitegemea Bunge!

Wananchi wamefanywa waamini kuwa Wakuu wa serikali hawaongozi nchi kwa kuongozwa na imani ya dini zao wala kutokana na maelekezo ya Wachungaji na Watakatifu wao. Ni serikali ya 'kisekula' na Bunge la 'Kisekula'.

'Usekula' uko wapi wakati watu wana chuki kiasi hicho dhidi ya Waislamu! Au 'Usekula' inapokuwa jambo la Wakristo. Serikali haiingilii kwa sababu 'Sekula', lakini la Waislamu inakuja juu; "Udini"! Serikali inakuwa ya Kikristo!

Jumuiya na taasisi zote za Kikristo nchini hapa ziko huru, kwa sababu katiba ya nchi inasema kuwa serikali kitakuwa mbali kabisa (na wala haitakuwa sehemu ya shughuli zake) na uendeshaji wa taasisi za dini (Kf. 19(2). Lakini serikali imeshiriki kuunda BAKWATA. Mwaka 1993 ikasimamia kwa hali na mali kupitishwa kwa Katiba ya kidikteta ya BAKWATA.

Viko Vyuo Vikuu kadhaa vya kidini vishafunguliwa nchini hapa kama kile cha Tumaini Iringa na Nyegezi. Hatukuwahi kusikia hata mara moja serikali kuwa mstari wa mbele katika kuunda kamati za uanzishwaji wa vyuo hivyo.

Sasa hicho cha Waislamu inayoanza kwa kuundiwa kamati za watu wa serikali itakuwa cha Waislamu au cha serikali. Na serikali yenyewe ipi! Iliyochukua ahadi ya kutenga nafasi maalum kwenye vyuo vyake vya ualimu kwa ajili ya watu wa Makanisa! Je; ni hii iliyojipa jukumu la kuyatafutia Makanisa fedha kutoka kwa nchi za nje ili kuendesha shughuli zake!

Yote haya yanayoashiria serikali kufanywa kama taasisi ya Kanisa (Memorandum of Understanding...) Waheshimiwa Wabunge hawayaoni. Hakuna udini wala Ukristo, ila pale Waislamu watakapotaka kuswali Ijumaa wakiwa shuleni hucharuka na kuwa wakali kama mbogo aliyejeruhiwa!

Pengine ipo dhana miongoni mwao kwamba waweza kuukandamiza Uislamu na kuwadhibiti Waislamu kwa kutegemea kauli kali za Bungeni na makofi mengi pamoja na hotuba za vitisho. Dhana hiyo ni sawa na yule aliyetaka kuzima glopu ya taa (bulb) kwa kuipuliza kama anavyozima kikoroboi. Katu haitozimika.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook