Uchambuzi/hoja binafsi
 
 
Yehova kaamuru panapofanyiwa ushirikina pavunjwe
 

Na Abu Tarik

Hii pia sio kweli; na huenda akina Batendi hawazielewi aya za Uislamu vizuri. Sai ni ibada ya Hijja ya kutembea haraka baina ya vilima Safa na Marwa huko Makka, hiyo ikiwa ni kumbukumbu ya vile ambavyo Mama Hajira (r.a.) mke wa Nabiy Ibrahim (a.s.) alivyoishiwa maji kule jangwani Makka na akawa anatapatapa akitembea baina ya vilima hivyo viwili mara nyingi, ili aone mbali, akitafuta maji amnyweshe mwanae mchanga Ismail (r.a.) aliyekaribia kufa kwa kiu.

Hatimaye Mwenyezi Mungu (s.w) akajaalia hapo jirani kuibuka kisima cha Zamzam, akakata kiu zao, na hadi leo maji ya kisima hicho yapo mengi. Iwapo akina Batendi wanaongelea jinsi makafiri wa Makka walivyokuja kuweka pale kisimani masanamu mawili (kama walivyoweka masanamu zaidi ya 300 mle kwenye Kaaba, Makka) wakayaabudu basi yote hayo yalishaondoshwa na kuteketezwa zamani, na muhala mle sasa mwafanyiwa ibada za kumwabudu Mungu, hakuna masanamu ya kuabudiwa. Ndio maana aya ya Qur'an 2:158 aliyonukuu Ndugu Batendi imewatoa shaka watu kuwa pahala panapochafuliwa kwa sanamu au najisi yoyote, pakiondolewa hizo najisi na kutwahirishwa basi panakuwa sio haramu wala sio shirk kuswalia hapo.

"2:158 Hakika Safa na Marwa (vilima viwili kule Makka kunakofanyiwa ibada ya kusai wakati wa Hijja) ni katika alama za kuadhimisha dini ya Mwenyezi Mungu. Basi anayehiji kwenye nyumba hiyo (Al-Kaaba) au kufanya Umra (Hijja ndogo), sio kosa (sio ushirikina) kwake kuvizunguka vilima hivyo viwili..."

HII ndio maana Waprotestanti waingiapo kusali Kanisa la pamoja (kama lile la Muhimbili) huondosha tu masanamu yote yaliyowekwa na wenzao kisha nao husalia humo bila hata ya kuyavunja! Uislamu uko mbele sana kuepusha dhambi isiyosameheka ya kumshirikisha Mungu inayokemewa mno na Biblia: Mt. 4:10; Yn 17:3; 7-8, 20:17; Law 24:16 na Qur'an 4:48, 36, 116.

Mathalan; Uislamu unakataza kusali wakati wa machweo au mawio ya jua, ili kujitofautisha na waabudu jua, lakini Wakristo fulani kila Pasaka huenda pwani na kusali sala ya mchomozo wa jua (Easter sunrise sermon), kama waabudu-jua. Mitindo mingi ya ujenzi, mavazi, ibada na kadhalika katika Ukristo mwingine nas asasa vimetokana na ule upagani wa kale uliopenyeza kule Roma ukaigwa duniani kote; kwa mfano; aina, maana, na matumzii ya misalaba, minara (obelisks, and towers), sikukuu kama za Krismass na Pasaka na shrehe zake, kuabudu "Mama na Mwana (kama walivyokiabudiwa Semiramis na Tammuz wa Babiloni, au Devaki na Krishna wa India, au Isis na Horus wa Misri au Cybele na Deoius wa Asia). Hata jina la siku tuliyoshurutishwa sote iwe ya mapumziko (Sunday) (Jumapili) ni "Siku ya Jua" yaani siku ya kusali watu wanaoabudu jua.

Yehova alifanya maagano kwa Damu, lakini Allah hakuagana kwa damu:

Dai hili nalo sio sahihi, na wadai wamejikanganya. Kwanza aya aliyonukuu Ndugu Batendi, Kut. 15:7-10 haiongelei agano la Ibrahim, bali zimeongelea aya Mwa. 15:5-14 au 15:18-21, au 17:2. Sijui ana maana gani kudai kuwa Yehova hufanza maagano yote kwa damu na kuchinja, kwani hakuna matukio ya damu kwenye maagano na Ibrahim (Kum. 15:18-21 na 17:2) na Nuhu (Mwa. 6:18 na 9:8), wala na Isaka, na Ishmaeli, na Yakobo, Daudi, na Waisraeli, na Finehasi.

Isitoshe, Mungu wala Yesu hawapendi sadaka (Hos 6:6, Mt 9:13) bali wanataka atiiwe Mungu kwa kuahidi kutimiza maagano yake kwa kumsujudia na kuyafanyia kazi:

"Kum 17:2 Nami nitafanya agano langu kati ya mimi na wewe, nami nitakuzidisha sana sana 3: Abramu akaanguka kifudifudi (akasujudu), Mungu akamwambia akasema, Mimi agano langu nimefanya nawe, nawe utakuwa baba wa mataifa mengi...".

Lakini Qur'an imeagiza utoaji wa sadaka na kuweka maagizo na maana yake wazi:

"22:34 Kila umma tumewafanyia mahali pa kuchinjia mihanga ya ibada ili kulitaja jina la Allah juu ya vile Alivyowaruzuku katika wanyama wenye miguu minne... 37: Nyama wala damu zao (hao wanyama wanaochinjwa) hazimfikii Allah, lakini inayomfikia Allah ni taa (utii) yenu".

Yehova anasema Yesu alikuwa radhi auawe ili damu yake iwe Dhabihu ya dhambi:

Usemi huu na aya ya Isa 53:10 sio sahihi. Mtume Paulo ndie alieupigilia wokovu wote msalabani na akahalalisha itikadi hii kwa kuzusha itikadi nyingine kadhaa (contoversial). Akionyesha jinsi itikadi hii ya Yesu kufa ili damu yake iondoe dhambi, Paulo alisema:

"1 Kor 15:14 Tena kama Kristo (hakufa na) hakufufuka basi kuhubiri kwetu ni bure, na imani yetu ni bure".

Itikadi hii ya Ukristo ("Paulline Christianity") yasema ni rahisi sana kuingia peponi. Wewe sadiki tu kuwa Yesu alikufa msalabani na kufufuka baada ya siku 3, basi utaondolewa dhambi zako zote ulizokwisha zitenda na utakazokuja kuzitenda, pamoja na adhabu zake! Lakini itikadi hii pamoja na itikadi zenzie za "Dhambi ya asili (Original sin)" na pia za "Upatanisho (Atonement)", zinapingana na aya nyingi za Biblia. Kwa mfano aya zifuatazo zapinga sadaka za kawaida, seuze kafara ya mwanadamu tena mwana "mzaliwa pekee" na mpendwa wa Mungu:

"Hos 6:6 Maana nataka fadhila wala si sadaka, na kumjua Mungu kuliko sadaka.

Naye Yesu, kama alijua akina Batendi watajaribu kuupotosha ukweli huu, alisisitiza hivi: "Mat 9:13 ... Mkajifunze maana ya maneno haya. Nataka rehema (mercy) sio sadaka." Kama alivyokuwa Yohana Mbatizaji, Yesu alihubiri toba, sio kujitoa muhanga. Pia itikadi hiyo inapinga aya zingine nyingi zinazoonyesha kuwa Yesu hata hakujua wala hakupenda kufa, hususan kile kifo cha laana cha msalabani, kama isemavyo Qur'an aya ya 4:57, na kama mifano ifuatayo inavyoodhihirisha:

Yesu hakufurahia kufa kwa ajili ya Mungu, na alifanya kila hali ili aokolewe: Kwa vile Yesu alikuwa mcha Mungu sana, lazima angefurahia kuuliwa kama alivyopangiwa na Mungu na kwa ajili ya lengo adhimu hilo la ondoleo la dhambi za watu wote. Yesu angeridhia na kutoa ushirikiano wote wa wauaji wake, kama alivyoridhia Nabii Ibrahim (a.s.) kuchinjwa na kutoshwa motoni (na Mungu akajamuokoa) au Nabii Ismail (a.s.) alivyoridhia kuchinjwa na babake Ibrahim (a.s.) (na Mungu akamuokoa), Lakini kinyume cha hivyo, Yesu alifanza kila namna ili aepuke kifo kile. Kwa hivyo Yesu akamwita Yuda "msaliti" kwa kumletea wauwaji wake (Lk 22:21, 48) badala ya kumsifu kwa kufanikisha ondoleo la dhambi zote. Aliwaagiza wafuasi wake walete silaha na mmoja amkate sikio mtumishi wa Kuhani (Lk 22:50). Yesu alisali na akalia mno asiuliwe, na kwa kuwa alikuwa mcha - Mungu dua zake zilikubaliwa (Mt. 26:37, 39 na 27:46; Lk 22:42-4; Yn 12:27); na akafarijiwa na akaokolewa (alisikilizwa:

"Lk 22:43 Malaika kutoka mbinguni alimtokea akamtia nguvu". "Ebr 5:7 Yeye siku za mwili wake alimtolea yule awezae kumwokoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana machozi, akasikilizwa, kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu".

"Mt 15:29 Bwana yu mbali na wasio haki, bali husikia sala ya mwenye haki". "Yk 5:16 ... Kuomba kwake kwa mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii". Pia ucha Mungu hurefusha maisha ya mtu, bali uovu hufupisha (Mt 10:27). Ushahidi huu waonyesha Yesu aliokolewa kama alivyoomba, na hakuuawa.

Itaendelea toleo lijalo.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook