Jalada la kesi ya Sheikh Bashir halijafika mahakamani
 

Na Muhibu Said
 

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini imesema kwamba inashindwa kumfutia shitaka la "uchochezi" aliyekuwa Imamu wa Msikiti wa Mwmbechai, Sheikh Omari Bashiri kwa madai kwamba jalada la kesi hiyo bado halijafikishwa mahakamani hapo hadi sasa.

Akiahirisha shauri hilo mahakamani hapo Jumatatu ya Julai 19, mwaka huu, Hakimu wa mahakama hiyo ambaye kesi hiyo iko mbele yake, Bw. G. Lwakibalila, alisema kuwa mahakama yake ingeweza kumfutia mtuhumiwa shitaka hilo kisheria endapo jalada hilo lingekuwepo mahakamani hapo.

Hakimu Lwakibalila aliyasema hayo kufuatia ombi lililowakilishwa mbele yake na Wakili wa kujitegemea anayemtetea mtuhumiwa, Bw. Twaha Taslima la kuiomba mahakama hiyo imfutie mteja wake shitaka hilo.

Wakili Taslima aliiomba mahakama hiyo imwondolee mteja wake shauri hilo kwa hoja kwamba shauri hilo limekwishashughulikiwa zaidi ya mwaka mmoja mahakamani hapo bila kusikilizwa.

Bw. Taslima aliiambaia mahakama hiyo kuwa mteja wake anayo haki ya kufutiwa kesi hiyo kulingana na kifungu cha 225(5) cha sheria ya kanuni za mwenendo wa jinai ya mwaka 1984 kinachoruhusu mshitakiwa kufutiwa kesi hiyo husika iwapo itafikisha siku sitini (60) mahakamani bila kusikilizwa na pia mwendesha mashitaka wa serikali (PP) au mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai wa mkoa (RCO) kushindwa kutoa sababu za msingi kuendelea kuwepo kwa kesi hiyo mahakamani bila kusikilizwa.

Amesema kuendelea kuwepo kwa shauri hilo mahakamani dhidi ya mteja wake bila kusikilizwa ni sawa na kumtwika mteja wake mzigo mzito begani na kuuacha uzidi kumtesa kwa kumwelema bila sababu zozote za msingi.

Hata hivyo, Hakimu Lwakibalila alisisitiza kuwa mahakama yake inasita kufuta kesi hiyo kwa madai kwamba inachelea mtuhumiwa kukamatwa na kurudishwa tena mahakamani kwa kuwa jalada la shauri bado halijafikishwa mahakamani hadi sasa.

Awali, mwendesha mashitaka wa polisi, Bw. Kisusura akiomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo, alidai mahakamani hapo kuwa jadala la kesi hiyo bado hajalipokea na kwamba mpaka sasa bado liko kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DPP).

Kesi hiyo itatajwa tena Agosti 3, mwaka huu.

Kesi hiyo yenye namba 1621 ilifunguliwa na serikali mahakamani hapo mwaka jana.

Wakati huo huo, kesi mbili za tuhuma ya kufanya ghasia, kujeruhi na kuharibu mali maeneo ya Mwembechai zinazowakabili Waislamu 22, zimeahirishwa mahakama ya Kisutu katika tarehe tofauti.

Kati ya kesi hizo namba 192/98 inatarajiwa kuendelea kusikilizwa mahakamani hapo Agosti 3 ambapo kesi namba 184/98 imepangwa kuendelea kusikilizwa hapo Agosti 25, mwaka huu.


Waalimu wa dini ya Kiislamu Mwanza waomba msaada wa vifaa
 

Na Ibun Thadeo, Mwanza
 

WAALIMU wa dini ya Kiislamu mashuleni mjini Mwanza wametoa wito maalum wa kupatiwa misaada ya vifaa vya kufundishia kutoka kwa wazazi na Waislamu kwa ujumla ili waweze kufikisha ujumbe wao kwa walengwa.

Kwa mujibu wa waraka wao, vijana hao ambao hasa hushughulika na elimu ya dini ya Kiislamu shule za msingi, wamesema kuwa pamoja na ahadi zilizotolewa na Waislamu mbalimbali wakati wa mahafali ya kuwaaga wanafunzi wa kidato cha nne mwaka jana katika shule ya sekondari Mwanza hakuna ahadi hata moja iliyotekelezwa.

Waliahidiwa baiskeli ili kuwahi mashuleni hasa shule za mbali, pia waliadiwa vitabu vya kiada (rejea), makaratasi kwa ajali ya kuchapa mitihani na hata posho kidogo kwa ajili ya kujikimu mchana.

Kuna taasisi ambayo iliahidi kuwaweka chini ya "programu" yao ya elimu mashuleni, lakini bila maelezo yoyote hadi sasa hakuna mawasiliano yoyote ambayo tayari yamefanywa.

Wakielezea wasiwasi wao kuhusu mitihani ya mwezi wa Agosti mwaka huu, wamesema kuwa kama hawajitokeza Waislamu kuwalipia gharama za kuandaa na kuchapisha mitihani hiyo, huenda isifanyike kabisa mwaka huu.

Vijana hao ambao kwa kifupi wanaitwa "JUVIKKU" wameonyesha kuleta mafanikio na hamasa kwa wanafunzi hasa wa kike kuweza kuvaa mavazi ya Kiislamu kwa kufuata rangi ya sare ya shule husika, sulaa la wanafunzi wa Kiislamu wa shule za msingi kuvaa hjabu ilikuwa ni suala "nyeti" kwa mujibu wa maelezo ya baadhi ya walimu waliozungumza na ANNUUR kwa sharti la kutotajwa majina yao.

"... Vijana wanastahili sifa, na hasa uvumilivu wao na maneno ya kukatishwa tamaa toka kwa walimu wenzetu hsa wakuu wa shule hizi za msingi". Walisema sasa hivi tatizo ni wazazi wenyewe kushindwa kuwashonea watoto wao hijabu, walitoa ombi maalum kwa wazazi wa Kiislamu kufanya mawasialino na walimu hawa ili kuhakikisha hakuna mtoto Muislamu wa kike asiyevaa hijab shuleni, ruhusa ipo tangu shule za msingi hadi vyuoni kwa nchi nzima.

JUVIKKU sasa hivi imepata ofisi mtaa wa Unguja baada ya kuhangaika sana kutokana na kuvunjwa kwa nyumba ya wakfu ya Msikiti wa Ijumaa iliyokuwapo pia ofisi ya Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania mtaa wa Mtakuja.

Kwa mujibu wa waraka huo wa WAJUVIKKU hivi sasa wanafanya maandalizi ya mkutano wa pamoja utakaojumuisha wanafunzi wa Kiislamu wa shule za msingi za mjini Mwanza.


Sherehe za TAMTA DAY zafana
 

Na Faki A. Faki, Tanga
 

WAISLAMU wa madhehebu mbalimbali wametakiwa kujifunza elimu ya dini ya Kiislamu ili waweze kuuelewa na kuutetea Uislamu.

Wito huo umetolewa na Masheikh wa Madrasat Shamsiya inayomilikiwa na Jumuiya ya TAMTA ya mjini Tanga, Sheikh Abdallah Ayub na Sheikh Muhammad Abubakar Al-Burhan.

Masheikh hao wametoa wito huo wakati wa kufunga sherehe za kuadhimisha siku ya kuasisiwa kwa Jumuiya ya TAMTA zijulikanazo kwa jina la TAMTA DAY zilizomalizika hivi karibuni mjini hapa.

Sherehe hizo zilizohudhuriwa na mamia ya Waislamu wa Manispaa ya Tanga na vitongoji vyake zilifanyika kwenye Makao Makuu ya Jumuiya hiyo eneo la Gatundu mjini hapa.

Katika nasaha zao mara tu baada ya kusomwa kwa Maulid yaliyohitimisha sherehe hizo, Masheikh hao waliosimama mmoja baada ya mwingine walisisitiza umuhimu wa elimu ya dini na kutoa hadithi mbalimbali za Mtume (s.a.w.) pamoja na aya za Qur'an kuonyesha fadhila za elimu.

Sheikh Abibakar ambaye alikuwa wa kwanza kuwahutubia Waislamu katika sherehe hizo alinukuu aya ya Qur'an na kusema kuwa Mwenyezi Mungu hakuwaumba majini na watu ila ni kutaka wamuabudu na kusisitiza kuwa mtu hawezi kumuabudu Muumba wake ipasavyo bila kuwa na elimu.

Sheikh Abibakar ambaye ndiye Mudir wa Madrasa hiyo aliongeza kusema kuwa ibada ya mtu mwenye elimu inapendeza zaidi kwa Mwenyezi Mungu kama vile mwanadamu anavyopendezwa na maji safi.

Naye kwa upande wake, Sheikh Ayub alitumia hadithi ya Mtume (s.a.w.) inayomtaja mtu anayekwenda kutafuta elimu kuwa ni sawa na mtu anayekwenda kwenye jihad.

"Ukifa katika kutafuta elimu unahisabiwa kama uliyekufa kwenye jihadi", alibainisha.

Akizungumzia kuwasaidia wanafunzi wa madrasa za kidini, Sheikh Ayub aliwataka Waislamu wenye uwezo kupeleka zaka zao katika madrasa mbalimbali ili kuboresha elimu kwa kuwasaidia wanafunzi hao kujikimu.

Alisema kuwa Waislamu wengi wanaopaswa kutoa zaka hutoa zaka zao kwa watu binafsi tu lakini hawafahamu kuwa inajuzu pia kutoa zaka zao katika madrsa za kidini kwa vile wengi wa wanafunzi wanaosoma ni maskini.

Sherehe hizo ambazo zilianza mwanzoni mwa wiki iliyopita kwa kisomo cha Tawasul na kupandisha bendera kwenye lango la jumuiya hiyo zilitawaliwa na shamra shamra mbalimbali za kusisimua.

Miongoni mwa shamra shamra hizo ni zafa iliyoanzia Msikiti wa Madina hadi yalipo Makao ya Jumuiya, misafara ya magari, pikipiki na baiskeli kwenda kuwarehemu Masheikh maarufu wa mjini Tanga waliofariki dunia na maonyesho ya wanafunzi pamoja na Maulidi. Jumuiya ya TAMTA inatimiza miaka 42 tangu ilipoanzishwa.


Sahihisho
 

KATIKA toleo lililopita iliandikwa kimakosa kwamba moja ya msaada unaohitajika kwa Imamu na Mwalimu pekee wa Msikiti na Madrasat Samaawiyya Mitende ya Kijiji cha Mitengwe, Kisarawe, Sheikh Kondo Maulid Jokolo kuwa ni pamoja na Baiskeli ya walemavu ya magurudumu matatu.

Usahihi ni kwamba ni baiskeli hasa inayohitajika kwa Sheikh Jokolo ni ya magurudumu mawili itakayomwezesha kubebwa na nduguze Waislamu kwenda sehemu mbalimbali kuhudhuria shughuli za Kiislamu na kuikodisha aweze kupata riziki. 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook