Na Mwandishi Wetu
KIKAO cha Maimamu kilichofanyika juzi (Jumatano) alasiri katika Msikiti wa Taqwa kimeamua kufanyika maandamano ya Waislamu wote Ijumaa ijayo kupinga kauli za Wabunge kuhusiana na vazi la hijab na swala ya Ijumaa kwa wanafunzi Waislamu.
Maimamu hao wamesema kwa kuwa Bunge limevunja katiba ya nchi kwa kuruhusu maamrisho ya dini kujadiliwa na Wabunge hawaoni sababu kwa Waislamu kuendelea kulalamika badala yake wasimame kuitetea dini yao.
Kikao hicho cha Maimamu kilichoitishwa kufuatia azimio la Waislamu waliokusanyika Msikiti wa Mtambani Jumapili iliyopita, kilitoa tamko la kupinga mwenendo wa taasisi za dola likiwemo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa kushambulia Uislamu na Waislamu.
Tamko hilo ambalo lilitarajiwa kuwasilishwa kwa Spika wa Bunge jana, limekemea vikali kauli za Wabunge na kutamka kutokuwa na imani na Bunge mpaka pale litakaporekebisha msimamo lililouita hasi ambao Wabunge hao wanakuwa nao wanapojadili mambo yanayohusiana na Watanzania Waislamu.
Tamko hilo limeorodhesha matukio kadhaa ambayo limedai yanaashiria chuki waliyonayo Wabunge dhidi ya waumini wa dini ya Kiislamu.
"Tunadhani Wabunge hawawaangalii Waislamu kwa mtazamo sawa na raia wengine wala kujali hisia zao, imesema sehemu ya tamko hilo lililotiwa saini na Amiri wa Waislamu Sheikh Juma Mbukuzi.
Aidha, Maimamu hao wamekemea hatua ya Wabunge kujadili maamrisho ya dini bila ya kuwahusisha wahusika.
"Pamengekuwepo na uwakilishi wa kidini Bungeni kama ilivyo kwenye masuala ya sheria ambapo Mwanasheria Mkuu uiwakilisha serikali", limesema tamko hilo ambalo ANNUUR ina nakala yake.
Aidha, limemtaka Spika wa Bunge kutoa kauli ya kufuta madai ya Wabunge kuwa wanafunzi Waislamu kuvaa nguo za stara na kuhudhuria swala ya Ijumaa ni udini unaoweza kuvuruga amani nchini.
Limewataka watendaji wakuu wa taasisi za dola kuzingatia kwa makini malalamiko ya Waislamu ili wachukue hatua za haraka kuiepusha nchi na mgogoro mkubwa wa kijamii unaoweza kusababisha maafa.
"Sote tupiganie amani na
utulivu unaotokana na kutendeana haki na uadilifu", limemaliza tamko hilo.
--
|
|