Lipumba awataka wananchi wawe tayari kwa mabadiliko
 

Na Mwandishi Wetu
 

WATANZANIA wametakiwa kuwa tayari kukabiliana na misukukosuko ya Chama tawala iwapo wamedhamiria kuleta mabadiliko ya kweli nchini.

Akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule ya Uhuru Jijini Jumamosi iliyopita, Profesa Lipumba alisema Chama kilichotawala miaka 40 hakitakuwa tayari kuachia madaraka kwa njia ya kidemokrasia.

Profesa Lipumba aliuambia umati huo wa watu kuwa CCM itafanya njama na kila hila ili iendelee kubakia madarakani.

Alisema matokeo ya uchaguzi mdogo wa Temeke na Ubungo ni ushahidi mmojawapo unaoashiria kuwa wanaotaka mabadiliko wana safari ndefu yenye vitisho na misukosuko mingi ambayo itawahitaji kuwa wavumilivu, walio tayari na msimamo madhubuti.

"Vijana wetu wa Temeke hivi sasa wako ndani kwa kesi za kupakaziwa, hata dhamana wananyimwa kwa kuwa wameonyesha upinzani kwa Chama tawala", alisema Profesa huyo katika hotuba iliyoonyesha kuvuta hisia za wengi.

Huku akiuuliza umati uliokuwa ukimsikiliza; "Ni nani walio tayari na msimamo wa kukabiliana na hayo", alionya Profesa Lipumba kuwa demokrasia ya kukabidhiana madaraka kwa njia ya kura haitakubalika hapa nchini kama wananchi hawatasimama imara.

Alisema mabadiliko ya kweli yanahitaji maguvu ya wananchi kupambana na watawala wakaidi wasioona haya kudhulumu.

Alisisitiza kuwa wananchi hawana budi kujiimarisha kuanzia sasa ili waweze kuleta mabadiliko ya kimsingi ambayo hayatotoa mwanya wa wakiritimba kupenyeza mirija yao.

Akizungumzia kutumika kwa vyombo vya dola kukisaidia chama tawala, alisema inasikitisha kuona Idara ya Usalama na Polisi vikipokea maelekezo ya CCM kuwaonea wananchi.

Profesa Lipumba alisema Idara ya Usalama na Polisi imeuwa ikikiuka kanuni zake ili kuisaidia CCM.

Kuhusu vyombo vya habari Lipumba alionyesha kushangazwa na baadhi ya magazeti kushindwa kuripoti habari katika usahihi wake.

Alidai propaganda za CCM kama ile ya jeneza iliripotiwa na vyombo vya habari katika namna iliyolenga kuishutumu CUF. Aliviomba vyombo hivyo kufanya uadilifu wa kitaaluma.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook