Na Modi Mngumi, Muheza
WANAWAKE wa Kiislamu wametakiwa kuanzisha miradi ya uzalishaji mali ambayo ni halali ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza kwenye baraza la wanawake wa Kiislamu lililofanyika mwishoni mwa wiki katika tarafa ya Maramba wilayani hapa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (UMMU SALAMA) mkoa wa Tanga Bibi Batuli Jabba alisema ni lazima wanawake wafanye kazi ili kuongeza kipato chao katika familia zao.
Bibi Jabba pia aliwataka wanawake wa Kiislamu kuzidai haki zao ambazo zimo ndani ya Qur'an na siyo kudai usawa kwa mtazamo wa kikafiri.
Akizungumzia kuhusu malezi Bibi Jabba alisema lazima wazazi hasa akina mama kuwalea watoto wao katika maadili ya kidini ili kupunguza maovu yanayoongezeka kila siku katika jamii.
Alisema mbali ya kuwa maadili
ya dini ya Kiislamu yanamfundisha mtu adabu nzuri pia yanalinda afya ya
binadamu kwani yanakataza kutumia vitu vinavyoweza kumdhuru mtu kama vile
utumiaji wa madawa ya kulevya na pombe.
Na Mwandishi Wetu
MAMIA ya Waislamu walikusanyika Msikiti wa Mtambani Jumapili iliyopita kujadili kauli ya Wabunge juu ya mavazi ya stara na uhudhuriaji wa swala kuu kwa wanafunzi Waislamu.
Waislamu hao walionyesha kushtushwa na mwenendo waliouelezea kuwa ni wa hatari unaoendelea kuzoeleka Bungeni kwa Wabunge kujadili masuala ya imani hasa ya Kiislamu bila ya kujali hisia za wahusika.
Akizungumza kwa niaba ya Maimamu, Amir Sheikh Juma Mbukuzi alielezea kwa kirefu madhila wanayoyapata Waislamu kutoka taasisi za dola.
Huku akikariri kauli ya Wabunge kama ilivyoripotiwa na gazeti moja binafsi la kila siku, Sheikh Mbukuzi alisema madhila hayo yamefikia kiwango cha Mbunge kusimama na kutoa kauli ya kuzuia Waislamu kutekeleza dini yao.
Alionya kuwa kama Waislamu watakaa kimya mwenendo huo ipo hatari ya kufutwa Uislamu kidogo kidogo hapa nchini.
"Leo wamezuia wanafunzi wasivae hijab na kuswali Ijumaa, kesho watatuzuia adhana na hafla za Waislamu", alisema Amir huyo wa Waislamu jijini.
Akitoa mfano wa hatari ya ukimya wa Waislamu, alisema leo hii jiji la Dar es Salaam limeenezwa mabucha ya nguruwe, vilabu vya usiku na magrosari yanayouza pombe usiku na mchana.
Alisema miaka ya nyuma jiji halikuwa na mambo hayo hasa maeneo ya Kariakoo, lakini kutokana na mikakati aliyoiita ya kidogo kidogo leo hii hali ni mbaya ambapo imefikia nyumba za Waislamu kugeuzwa baa na Misikiti kuzungukwa na stoo za pombe.
Wengi wa watu waliopata fursa ya kuchangia katika mkutano huo walionyesha kuchoshwa na mfululizo wa matukio dhidi ya Waislamu, hivyo walipendekeza kufanyika kwa tukio linaloweza kutoa picha ya hasira waliyonayo Waislamu.
Wachunguzi wa mambo ya jamii wameielezea hatua ya Wabunge kuzuia utekelezaji wa maamrisho ya dini kwa baadhi ya wananchi huenda ukasababisha kuvurugika kwa amani ambayo nchi yetu imekuwa ikijivunia.
Akizungumza na gazeti hili wiki hii mtaalamu mmoja wa masuala ya jamii wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema matamshi ya Wabunge yanaipalia makaa Tanzania.
Alisema kwa uzoefu wake kinyume
na walivyozungumza Wabunge ndio kudumisha amani nchini kamba watu wapewe
fursa kufuata maamrisho ya dini zao hasa kwa waumini wa dini kuu.
Na Mwandishi Wetu, Tanga
WAISLAMU mjini Tanga wamefadhaishwa na kauli zilizotolewa na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wakati wakijadili mawasilisho ya Bajeti ya Wizara ya Elimu na Utamaduni wiki iliyopita.
Jumuiya za Shamsiya, Zaharau, Maawa na Jamaat Kheir zimekubaliana kuwapa maelekezo waumini wa mjini Tanga juu ya nini kifanyike kukabiliana na njama za kuwakufurisha Waislamu zinazoandaliwa na taasisi za dola.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Tanga wiki hii, wasemaji wa Jumuiya hizo wameonyesha nia ya kutaka kufanya maandamano kupinga njama hizo ambazo wamesema zinaweza kuliingiza Taifa katika machafuko ya kidini.
Maeneo mbalimbali ya Tanga mjini yamebandikwa matangazo kuwataka Waislamu kuhudhuria Maulid ya Sharif Nnuur ambayo ratiba yake inaonyesha kutakuwa na ujumbe maalum utakaotolewa kwa Waislamu siku hiyo kuhusiana na yaliyojitokeza Bungeni.
Wiki iliyopita Wabunge wa CCM, NCCR na CHADEMA walimshinikiza Waziri wa Elimu Profesa Juma Kapuya kuondoa hoja ya wanafunzi waumini wa baadhi ya dini waruhusiwe kuvaa sare za shule zenye kuzingatia mipaka ya dini zao na kuhudhuria swala kuu.
Wabunge hao walidai kuruhusu wanafunzi hao kutekeleza imani zao ni udini unaoweza kuhatarisha amani ya Taifa.
Hata hivyo Wabunge hao hawakuona
hatari ya udini kwa wanafunzi Wakristo kupewa fursa ya mapumziko siku za
Jumamosi na Jumapili kuhudhuria ibada zao na sare za shule kuzingatia maelekezo
ya dini zao.
Na Mwandishi Wetu
JUMUIYA ya Ansaar Sunnah ya mjini Tanga iko hatarini kufutwa na Msajili wa Vyama kama haitaeleza kwa nini isifutwe katika muda wa siku 21 kuanzia Julai 14, mwaka huu.
Barua ya Msajili wa Vyama kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani imedai Jumuiya hiyo imeshindwa kukamilisha masharti ya kuwepo kwake mpaka kufikia mwishoni mwa mwezi uliopita.
Barua hiyo yenye Kumb. Na. SO.No. 836/20 ya Julai 14, 1999 iliyosainiwa na B. Shomari ambayo ilipokelewa na Jumuiya hiyo wiki hii imedai kwa mujibu sect 12 ya sheria ya vyama (Society Ordinance) Msajili wa Vyama anapaswa kuifuta Jumuiya hiyo ya kidini baada ya siku 21 tangu tarehe ya barua hiyo.
Jumuiya ya Ansaar ilianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 80 ikiwa na maengo ya kuwaelimisha vijana wa Kiislamu na kuwapa maadili ya dini yao.
Tangu wakati huo imekuwa ikishughulisha na ujenzi wa shule za watoto, Misikiti na kulea mayatima.
Imetoa mchango mkubwa katika kubadili mienendo ya vijana wa mjini Tanga ambao hivi sasa wamekuwa wakereketwa wa masuala ya dini.
|
|