Katika Kikao cha Bunge, Waziri wa Elimu na Utamaduni Profesa Juma Kapuya wakati wa kuwasilisha hotuba yake ya makadirio ya matumizi ya Wizara yake ya Elimu na Utamaduni ya mwaka 1999/2000 alitoa agizo kwa kila mwalimu mkuu na wakuu wa vyuo kuhakikisha wanafunzi wa madhehebu mbalimbali wanapewa nafasi ya kuabudu nyakati za sala kuu na waruhusiwe kuvaa mavazi yanayokubalika katika maadili yao.
Katika kuchangia hotuba ya Waziri kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari baadhi ya Wabunge walimtaka Mheshimiwa Waziri Profesa Juma Kapuya asiingize suala la udini mashuleni.
Inashangaza kuona Waheshimiwa Wabunge ambao wamechaguliwa na raia wa dini mbalimbali ili kutetea haki zao wakitoa shutuma kama hizo.
Kwa jinsi inavyofahamika, ni kwamba Waislamu kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamika kupata haki yao hii ya msingi. Agizo la Mheshimiwa Waziri lilikusudia kuondoa kadhia hii ili Waislamu nao wawe na uhuru wa kuabudu kama ilivyo kwa waumini wa dini nyingine. Picha inayojitokeza ni kuwa Waheshimiwa Wabunge ndio wenye udini kiasi cha kumshutumu Mheshimiwa Waziri Kapuya ambaye alikuwa anatekeleza Katiba ya nchi ili kuwapa waumini wa dini zote haki sawa.
Waheshimiwa Wabunge katika michango yao wamedai kuwa Waislamu kupewa haki sawa ya kuabudu kama dini nyingine kama vile ruhusa ya kwenda kusali na kuvaa mavazi kulingana na imani yao eti kutaleta kuvunjika amani na utulivu wa nchi hii. Nini tafsiri inayopatikana hapa. Hapa Waheshimiwa Wabunge wanamaanisha Waislamu kutekeleza imani maana yake nchi itaingia katika machafuko.
Katika hali isiyo ya kawaida baadhi ya Wabunge Waislamu hawakupewa nafasi kuchangia hoja hiyo.
MSAUD inalaani kitendo cha Wabunge hawa ambacho kimejaa udini ambao unalenga kuupiga vita Uislamu na Waislamu kwa kutoa shutuma zao dhidi ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Utamaduni anayetaka kuleta usawa kwa dini zote.
MSAUD pia inatoa tahadhari kwa raia wema kutozishabikia shutuma za namna hii za Waheshimiwa Wabunge ambazo ndizo zitakazosababisha kuvunjika kwa amani na utulivu wa nchi hii.
Ee Mungu. Wape viongozi wetu ujasiri wa kuwa waadilifu
Amiina
|
|