MAKALA MAALUM
 
Tamko la Maimamu dhidi ya matamshi na msimamo wa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kuhusu wanafunzi Waislamu kutekeleza imani yao wakiwa mashuleni
 

1.Uzoefu unaonyesha kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano limekuwa na msimamo hasi linapojadili masuala yanayohusu Uislamu na Waislamu:

Ni Bunge hili lililoanzisha zogo iliposemekana Zanzibar imejiunga na OIC.

Ni Bunge hili ambapo alisimama aliyekuwa Waziri Mkuu wa serikali ya awamu ya pili Bwana John Malecela kupiga marufuku mahubiri ya Waislamu.

Ni Bunge hili lililodhamiria kufuta sheria ya Mirathi ya Kiislamu badala yake kutumika sheria moja ya Mirathi kwa Watanzania wote, hatua yenye mwelekeo wa kuwakufurisha Waislamu.

Ni Bunge hili lililoshangilia kuuliwa Waislamu Msikiti wa Mwembechai.

Ni Bunge hili lililozuia kujadiliwa hoja ya kuuawa Waislamu na kuundwa Tume ya Wabunge kuchunguza huzuni hiyo kinyume na ilivyokwisha fanya katika masuala mengine.

Kwa uzoefu huu, tunadhani kwamba Bunge na Wabunge hawawaangalii Waislamu kwa mtazamo sawa na raia wengine wala kujali hisia zao kwa sababu:

Ni Bunge hili lililojadili na kupitisha kwa kauli moja Jumamosi kuwa siku ya mapumziko ili kuyapa baadhi ya madhehebu ya Kikristo fursa ya kushiriki ibada zao hali kadhalika 'Boxing Day (Desemba 26) na Mwaka Mpya ni fursa nyingine kwa Wakristo kusherehekea. Ni Bunge hili ambalo huanza kwa maombi ya Kikristo.

Hivyo, sisi Maimamu wa Misikiti ya Dar es Salaam tukiongoza waumini tunalaani mwenendo huo wa Bunge na kutamka wazi kutokuwa na imani nalo mpaka pale litakapoonesha kuwajibika kinchi bila ya chuki dhidi ya, wala upendeleo kwa, dini, madhehebu au makundi fulani ya wananchi.

2. Ni dharau na kejeli kubwa Wabunge kujadili imani za watu na kuthubutu kuzuia au kuelekeza namna ya kuzitekeleza; kwa ajili hiyo:

(a)Sisi Maimamu tunapinga vikali kupelekwa Bungeni hoja ya swala na mavazi kwa wanafunzi Waislamu. Alichopaswa Waziri kutekeleza ni kushinikiza utekelezaji wa Circular iliyokwisha tolewa kwa waalimu wakuu ambao baadhi yao hivi sasa wamechukua msimamo wa kupinga suala hilo wakiegemea dini zao.

(b)Kama hapana budi kujadiliwa basi pawepo na uwakilishi wa kidini Bungeni kama ilivyo kwenye masuala ya sheria ambapo Mwanasheria Mkuu huiwakilisha serikali Bungeni. Haiyumkini Wabunge wanaowakilisha vyama visivyo na dini kujadili imani au maamrisho ya kidini Bungeni.

(c) Spika wa Bunge awahadharishe Wabunge kuwa mwenendo wao wa chuki dhidi ya madhehebu fulani utaiingiza nchi katika machafuko na umwagaji wa damu.

Sambamba na hayo, kabla ya kikao cha Bunge kuakhirishwa tunamtaka Spika atoe kauli ya kufuta madai kwamba wanafunzi Waislamu kuvaa nguo za stara na kuhudhuria swala ya Ijumaa Msikiti ni udini na kuvuruga umoja na amani ya nchi. Hatudhani na wala si kweli kwamba umoja wa nchi unaweza kuvunjika kwa Muislamu kuvaa Hijab au kuhudhuria swala.

3. Tuna wasiwasi mkubwa juu ya utendaji wa taasisi kuu za dola; serikali, Bunge na Mahakama zinaposhughulikia masuala au mashauri yanayohusu Waislamu na imani yao. Tungeomba wahusika wa ngazi za juu (Rais, Spika na Jaji Mkuu) wa vyombo hivyo wafuatilie kwa karibu mwenendo huu unaoweza kuwafikisha raia Waislamu kuamua vinginevyo.

Pamoja na hayo tumeazimia kufanya maandamano ya amani ili kushinikiza madai yetu Ijumaa ijayo tarehe 30/7/1999.

Sote tupiganie amani na utulivu unaotokana na kutendeana haki na uadilifu.
 

Wabillah Tawfiq

Sheikh J. Mbukuzi

AMIR
SHURA YA MAIMAMU

 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook