MAKALA YA KIMATAIFA
 
Waislamu waajiriwa Uingereza wanaswali kwa wakati
 
 

APRILI 26-30, 1999 ulifanyika mkutano wa Kimataifa nchini Uingereza uliopewa anuwani Uingereza na Uislamu. Kutoka Tanzania walihudhuria Mabwana Issa Mnenge na Ismail Abdullah. Fuatana na Bwana ISMAIL ABDULLAH katika sehemu ya tanu ya makala hii uelewe lengo na yatokanayo na mkutano huo.
 

EBU sasa tuitizame Uingereza nyumbani kwake, na wageni wake wa kudumu, yaani Waislamu wa Uingereza. Kuna misemo miwili ambayo katika nukta hii itabidi tuzitafakari, ya kwanza ni pale Muingereza anaposema "Charity begins at home". Tafsiri: "Wema huanzia nyumbani". Kwa hiyo dhamira ya Muingereza katika dhana ya mshikamano "Mutuality", kioo kizuri kama tulivyokwisha sema ni jinsi anavyoishi na Waislamu wa nyumbani kwake kwanza.

La pili, ni somo tunalopata sisi sote kutoka kwa Muingereza, kulingana na dunia ya sasa, kuwa dunia ni kijiji kimoja tu, chenye tamaduni mbalimbali, mila mbalimbali, dini mbalimbali. Kwa hiyo ikiwa dunia, hivyo ndivyo ilivyo, sasa ni kijiji tu, sembuse hiyo London au Uingereza kwa jumla.

Hapa ndio ule msemo wa hivi sasa "Devesify or you Die". Tafsiri inaweza kuwa: "Kubali mabadiliko au utakufilia mbali".

Jitihada za Uingereza kubadilisha kanuni na taratibu zake, tena kwa nia njema, zinaonekana wazi unapofuatilia mafanikio ya Baraza la Waislamu wa Uingereza (Union of Muslim Organisation of UK & EIRE", katika mijadala iliyofanya na serikali yake. Hapa chini ni mifano michache kama tunavyoipata kutoka UMO news review vol. 1 No. 3 of 18 January 1999.

1996 ilikuwa imefanikiwa kupata vibali 18 vya kujenga Misikiti, sehemu mbalimbali nchini Uingereza, na hivi sasa walikuwa wamefanikiwa kupata vibali zaidi ya 1000.

Wamefanikiwa kupata kibali cha kuwa na mabucha yenye kuuza "halali" iliyochinjwa Kiislamu. Nazo ni nyingi na zimetapakaa sehemu mbalimbali nchini Uingereza.

Wamefanikiwa kupata kibali kinachowaruhusu waajiriwa kuswali swala zao kwa wakati makazini kwao.

Kupatikana kwa muhubiri wa Kiislamu kwa ajili ya wafungwa magerezani.

Serikali inagharamia shule mbili za Kiislamu, huu ni mwanzo mzuri kwani Waislamu wana shule zao za msingi, sekondari na vyuo vikuu vyote kwa jumla zapata sitini.

Haya si mabadiliko madogo bali ni mabadiliko makubwa na inaelekea kuwa ni mwanzo wa mabadiliko mbalimbali mazuri katika mfumo kongwe wa jamii ya Kiingereza ili kuipa nafasi nzuri jamii mpya ya Kiislamu, wageni wahamiaji kujisikia kuwa nao ni raia huru.

Namalizia kwa kusema kuwa kitu muhimu ambacho mkutano uligundua kuwa kinaweza kuwa, mara nyingi, ndio sababu kuu ya kutoliwana ni Ignorance. Tafsiri: Nadhani tafsiri ni ujinga lakini nzuri ingekuwa kutojua.

Waislamu na Wakristo licha ya kuwa wanaishi pamoja enzi na enzi lakini huenda Waislamu hawawajui Wakristo na Wakristo hawawajui Waislamu licha ya kuwa wanaoleana, kufanya kazi pamoja na kadhalika.

Kabla ya kumalizia turudie swali letu lile la awali:

Kwa nini Uingereza inaipa umuhimu mkubwa suala la "Mutuality"? Na tuache Waingereza wajibu wenyewe.

Tunajibu kwa kurudi tena kwenye ile hotuba ya mtoto wa Malkia Prince Charles (Oktoba 27, 1993):

"Waislamu Waingereza ni Kito. Wenye kutoa mchango wao kwenye nyanja zote za uchumi wetu: Viwanda, huduma za jamii, utaalam na sekta binafsi. Wao ni waalim, madaktari, wahandisi na wanasayansi.

Paliposhindikana maelewano kuhusu mshikamano basi pana haja ya maelewano zaidi miongoni mwa wananchi wetu. Navutiwa na wale wanaume na wanawake wanaojitahidi bila kuchoka kukuza uhusiano mzuri katika jamii.

Uislamu na Magharibi lazima wajitahidi kwa bidii kuelewana. Na kuondoa sumu yoyote baina yetu. Na kumuondoa jinamizi la kutoaminiana na kuogopana. Umbali tutakaosafiri katika mwelekeo huo, ndio dunia bora ambayo tutajenga kwa ajili ya watoto wetu na vizazi vijavyo".

Somo:

Somo tunalojifunza toka kwa Waingereza ni kuwa Waislamu wapo, watakuwepo na hawapaswi kupuuzwa. Hazina kuu aliyonayo na anayoringia Mwingereza ni utamaduni wa "Dialogue" Mjadala.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook