Na Habiba Swedi
JUNI 16, mwaka huu wananchi pote nchini walizishuhudia sherehe za maadhimisho ya "Siku ya Mtoto wa Afrika". Maadhimisho haya ni ya kuhistoria, kukumbuka kupinga elimu ya kibaguzi kulikopelekea Juni 16 mwaka 1976, madhalimu wa kikaburu kuwadungua risasi za moto na kutoa roho za wanafunzi wa Kiafrika kule Soweto, Afrika Kusini.
Sherehe hizi kwa mara ya kwanza zilifanyika Juni 16, mwaka 1991, kufuatia Azimio la viongozi wa nchi huru za Afrika waliokutana kule mjini Abuja, Nigeria mnamo Julai 1990, kuona haja ya kuyawekea kumbukumbu mauaji hayo.
Ujumbe wa mwaka huu umekusudia kuhuisha fikra za wazazi, walezi na viongozi kutoa umbele katika elimu kwa watoto. "Elimu ya msingi ni lazima kwa watoto wote, na kwamba ni jukumu la kila mmoja wetu".
Serikali kwa upande wake imeufikisha ujumbe huu kwa walengwa. Pale Arusha ambapo sherehe hizi zilifanyika kitaifa, viongozi mbalimbali walikuwepo, tukianzia na mgeni rasmi, Mheshimiwa Edward Lowassa ambaye ni Waziri katika ofisi ya Makamu wa Rais, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mheshimiwa Mary Nagu, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Daniel Ole Njoolay, Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Watoto ulimwenguni (UNICEF) nchini Tanzania Bwana Bjorn Ljungqvist, viongozi wa Shirika lisilo la kiserikali la kuhudumia watoto "kuleana" la mjini Mwanza na wengineo.
Cha ajabu ni kwamba, uwakilishi kutoka vyombo vinavyowaongoza Waislamu, haukuwepo katika sherehe hizo au kama ulikuwepo basi ni katika uhudhuriaji wa ili mradi usio na uzito wowote.
Umma wa Kiislamu unawatazama viongozi wake kama kiungo muhimu cha kuwanusuru watoto. Kwa kuhudhuria hafla za aina hii kunapelekea viongozi hao kujifunza kutoka upande mwingine kwa faida ya wanaowaongoza.
Umaskini ni kidonda ndugu kwa familia nyingi za Kiislamu. Licha ya kushindwa kumudu kulisha familia zao, kusomesha watoto ndio kabisa ukimtajia mtu ni kama umemtonesha kidonda.
Moja ya sababu kuu ya umaskini huu ni ukweli wa kihistoria juu ya ubaguzi dhidi ya Waislamu katika elimu.
Aidha, umaskini umezaa kundi kubwa la watoto wanaohitaji kutazamwa kwa jicho la pekee. Humu wamo yatima, wenye ulemavu wa aina tofauti, watoto magerezani, mitaani, wanaojitosa katika ukahaba, mihadarati na kadhalika.
Lipo kundi lingine la akina Sheikh Sharif, wale wenye vipaji, ambao nao kwa kukosa usimamizi madhubuti wamejikuta wakidakwa na walaghai wachache, wakitumika kwa maslahi binafsi na hivyo kunyimwa haki yao ya kupata elimu.
Pamoja na matatizo yote hayo, Waislamu wanajikongoja hivyo hivyo kupigania dini yao. Wanawasomesha watoto, siku ana hela ya mchango au ada analipa, siku hana, haya tena mtoto anabaki nyumbani.
Licha ya ukweli kuwa jukumu la kusomesha linabaki kwa wazazi/walezi tumeshaona wengi uwezo wao ni mdogo, ajabu hata wale ambao kidogo ni afadhali wamekuwa wagumu kusaidia kila mtu anajali lwake.
Katika kila jambo, kunahitajika ukereketwa. Wakati ujumbe wa siku ya mtoto wa Afrika unasisitiza umuhimu wa elimu ya msingi kwa watoto wote hali ya madrasa kama vituo vya awali kulelea na kutoa mafunzo kwa watoto wa Kiislamu ni mbaya.
Nyingi ziko kwenye mabaraza ya nyumba za waasisi wake, kwa zile zilizopo ndani ya Misikiti, juu hakuna paa. Watoto wanaungua na jua, msimu wa mvua zinafungwa. Matatizo ya vikalio, majuzuu na kadhalika ni pigo kubwa kwazo, sikwambii maslahi duni ya waalimu. Bado kufundisha madrasa ni kazi tu ya kujitolea.
Wazazi wengine hawaithamini elimu ya dini, na watoto kwa upande wao wanakimbia ukali wa waalimu ama kuwa na hofu ya kutofaidika kiajira mara wamalizapo masomo.
Wapo viongozi wa taasisi na jumuia za Kiislamu wasioyajua haya. Wakati hali halisi inaonyesha kuachwa nyuma kwa Waislamu kielimu, wale wakereketwa wanaopiga kelele za madai ya ubaguzi dhidi ya Uislamu, kamwe hawatasikika iwapo kundi lingine bado ni la wajinga wasiotambua umuhimu wa kuelekeza fikra zao katika mapambano ya kuwanusuru watoto wao.
Kwa tafsiri nyingine ni kwamba, viongozi wa Kiislamu wanastahili kushikamana ili wapambane na madhila dhidi ya Waislamu na kuamsha fikra za mageuzi kwa watoto kwa kuwasaidia wazifahamu haki zao kwa misingi ya dini yao, ikiwa ni pamoja na kuwahudumia watoto wote wanaohitaji misaada, badala ya kujitenga wakitumaini udugu wa kidini ambao uhalisi wa mambo unaonyesha kutoweka polepole kwa ndugu hao miongoni mwa jamii ya Kiislamu.
Ustawi wa watoto wa Kiislamu ni kero kubwa kwa viongozi kuhakikisha watoto wote wanaipata haki yao ya elimu, na taasisi/jumuia ziwe mstari wa mbele kuboresha hali za madrasa, kujenga shule na vyuo vya ualimu vya Kiislamu huku watu binafsi wakihamasishwa kuchangia.
Si vibaya watoto wa Kiislamu
wakawa na siku yao. Ile siku ya mauaji ya Mwembechai Februari 13, 1998
iwe ni siku ya kumbukumbu. Kukumbuka ulemavu alioupata mtoto Chuki Athumani
kwa kupigwa risasi na vyombo vya dola. Hiyo ni dhulma kama ya wale wa Soweto,
hivyo watoto wa Kiislamu wanahitaji kujumuishwa pamoja, wapate fursa ya
kutoa madukuduku yao.
Na Aradha Mangungu
KILA sifa njema anastahiki Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema. Ambaye amemteremshia mwanadamu Qur'an. Amemuumba mwanadamu. Amemfundisha mwanadamu kutambua bayana kati ya kheri na shari.
Mwanamke wa Kiislamu ni yule ambaye maisha yake pamoja na vitendo vyake vyote vya kila siku vinaenda sambamba na sheria za Kiislamu. Mwanamke huyu pamoja na kutoa shahada, anapaswa pia kufuata Qur'an mujaahirin. Awe tayari kwenda na kuutetea Uislamu. Kama tunavyoambiwa ingieni katika hukumu za Kiislamu zote.
Uislamu unamtaka mwanamke ajihifadhi viungo vyake. Asidhihirishe umbo lake. Yote haya yanaenda sambamba na elimu. Bila kuifahamu elimu, basi hatutaweza kujua sisi ni nani, lipi lengo la kuumbwa kwetu na wajibu wetu.
Kufikiri kwamba elimu ni kujua historia, biolojia au fiqhi, haitoshi. Elimu ni maarifa yanayoambatana na ujuzi (Development of good taste in knowledge and good form in conduct).
Elimu kwa wanawake ni mojawapo ya mambo muhimu sana kuzungumzia na kuyafanyia kazi. Lakini swala la elimu mahsusi kabisa kwa ajili ya kumuandaa mwanamke au binti wa Kiislamu aje kuwa mama wa Kiislamu halijafanyiwa kazi. Hivyo basi kutokana na kwamba swala la elimu ya juu kwa mwanamke halijafanikiwa vyema kuongeza maneno machache na maelezo kwa ufupi hayatobadilisha the essential nature of secular education.
Katika Uislamu, elimu imesisitizwa kwa pande zote mbili (mwanamke na mwanamume): "Twaalibu llmu farii dhuwatur 'alaa kulliy Muslim wa muslimati". Na ipo Hadith nyingine isemeyo: "Twalibu Ilmu afdhuwaluinda Allah".
Mwenye kusoma kweli kweli akaona namna gani alivyoumba Mwenyezi Mungu, mashangazo na hikima zilizomo katika kuumba huko, hao ndio wanaojua kweli ukubwa wa Mwenyezi Mungu. Na katika Qur'an tunaambiwa:
"... Kwa hakika wanaomuogopa Mwenyezi Mungu miongoni mwa wanawake ni wale watalaamu (wanavyuoni). Bila shaka Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu, msamehevu". Pia tunaweza kurejea (44:10-13) na (35:28-29). Wala hakuna kinachompeleka mtu wala hakuna kinachoupeleka mbele kuliko elimu.
Mwenyezi Mungu hakutuamrisha kusoma elimu zipatikanazo kwenye madrasa tu, bali pia tusome elimu zote zinazopatikana kwenye maskuli, maacedemy, macollege au University. Malaboratory na mwinginepo. Wanawake tuwe tayari kusoma kwa bidii zote na kupata elimu hizi zote. Tuondoe fikra potofu za kufikiri mwanamke yeye ameumbwa kwa ajili ya kufanya kazi za nyumbani tu, kuhudumia familia na watoto. Na kwamba hata akisoma elimu yake inaishia jikoni. Elimu kuitafuta kwake mpaka kuipata inahitaji subira na uvumilivu wa hali ya juu. Na subira ni namna nne:
Kustahamili katika kufanya mema ambayo ni mazito kwa mtu kudumu nayo. Kustahimili katika kuacha mambo maovu ambayo ni mazito kwake kuyaacha. Kustahimiliana na viumbe wenziwe, awachukulie mabaya yao wala asiwafanyie mabaya yake na kustahimili misukosuko ya ulimwengu.
Hivyo basi katika kuyatekeleza yote haya tumewavumilieni na kustahimili mambo, ili tuweze kufanikiwa. Tusiwe wenye kuyachukulia mambo kwa pupa, kukata tamaa hakutatusaidia.
Lengo letu kuu ni kupata
dola ya Kiislamu yenye wachungaji walioelimika na walevi wa familia zilizo
bora zenye msimamo wa Kiislamu.
--
|
|