BARUA
 
 

Amkeni! Amkeni! Amkeni Waislamu
 

Ndugu Mhariri

WATUKUFU Waislamu mna nini hamuamki? Matukio ambayo mlitakiwa muamke na msimame kama Waislamu na muutupilie mbali Utanzania bila shaka yale ya mabucha ya nguruwe 1993. Kipindi hiki Masheikh na viongozi wetu wengi waliteswa sana pamoja na kutiwa magerezani bila dhamana. Wengine walibambikizwa kesi za uhaini kuhusishwa na mabomu pamoja na majambia makontena toka Uarabuni.

Kipindi hiki Wakristo Wameru waliuana kwa silaha za moto pamoja na kuchomeana nyumba na mashamba. Viongozi wakuu wa nchi walitumwa Meru mkoa wa Arusha kuwasuluhisha wakiombwa walinde msalaba.

Sisi tunaozea rumande Keko na Ukonga, Sheikh Kassim Juma alifariki kipindi hiki kutokana na mateso makubwa yaliyomfika.

Tukio jingine kubwa zaidi ya yote ni lile lililotokea Msikiti wa Mwembechai. Waislamu walipotandikwa risasi za moto kama ngedere kwa lengo la kuwalazimisha kumtambua Yesu ni Mungu tena ni Mwana wa Mungu tena alikufa msalabani.

Aya za Qur'an zinazotaja Yesu si Mungu wala si mwana wa Mungu na wala hakufa msalabani marufuku kuhubiriwa tena Tanzania. Risasi hizo ziliteketeza maisha ya waumini kadhaa kama wanavyoonekana kwenye "kanda za mauaji ya Mwembechai".

Ni kipindi hiki hiki Wamasai Arusha walihoji matumizi ya kodi zao. Walipolazimishwa kulipa kwa hasira walichoma moto nyumba ya Mwenyekiti wao pamoja na kughairi kabisa kulipa kodi. Wakuu wa nchi kuanzia Mawaziri hadi Rais walikwenda Arusha kuwaomba Wamasai wakubali kulipa kodi japo kwa kiwango cha chini.

Lakini haikuwezekana. Mwisho Rais Mkapa akawaomba pamoja na kuwalipa mamilioni ya fedha kama fidia ya ng'ombe wao.

Wakati huu wakiombwa Wamasai waliochoma moto nyumba na mazao pamoja na kughairi kulipa kodi ya maendeleo, Waislamu waliokamatwa maeneo ya Mwembechai na Manzese wanahenyeshwa rumande Segerea bila dhamana.

Akina Simbaulanga wanaomtukana Mtume (s.a.w.) kwamba ni malaya tena kafa kwa ukimwi nao walikamatwa kwenye kadhia hii. La kushangaza ni pale wao walipoachiwa kwa dhamana baada ya muda mfupi sana. Ndiyo! Wao ni Wakristo na mahakimu ni Wakristo. Wanafanya kazi kama Wakriso si kama Watanzania.

Tukio lingine ni hili la juzi Bungeni Mbunge wetu Mtanzania Profesa Juma Kapuya alipofokewa na Wabunge Wakristo walioapizwa kanisani kuutetea msalaba popote walipo. Wamefundishwa tangu watoto kwamba maadui wa Kanisa hapa Tanzania ni Uislamu (Kanisa Katoliki na siasa ya Tanzania bara 1953 hadi 1985 by Dr John Sivalon M.M. uk. 26) Kwa hiyo jambo lolote litakalowapa manufaa Waislamu marufuku.

Kwa nia nzuri Mbunge wetu Mtanzania alitoa maagizo kwa kila mwalimu mkuu na wakuu wa vyuo kuhakikisha wanafunzi wa madhehebu mbalimbali wanapewa nafasi ya kuabudu nyakati za sala kuu na waruhusiwe kuvaa mavazi yanayokubalika katika maadili yao.

Wabunge Wakristo CCM, NCCR na CHADEMA haraka wakaona kwa akili zao kwamba "sasa Waislamu watafaidi. Mabinti zao wataishi Kiislamu. Wataachana na sare za Kikristo zilizozoeleka tangu ukoloni. Shule zote zitaonekana za Kiislamu. Watasali sala tano shuleni, mswada huu ukipita Kanisani tutatengwa. Bungeni Wakristo ni wengi kuliko Waislamu. Na Waislamu walioko ni bendera kufuata upepo. Tumpachike Kapuya udini. Wakamvamia Profesa Kapuya naye kukosa msimamo wa kumuunga mkono, akanywea, akaomba radhi.

Kwa bahati mbaya Wabunge Wakristo hawauelewi Uislamu. Inawezekana pia baadhi ya Waislamu bungeni hawauelewi Uislamu. Muislamu akiuelewa Uislamu hawezi kuishi, kufanya kazi, kula, kutembea, kuvaa na kadhalika Kitanzania. Kila atakalofanya atafanya Kiislamu Kiislamu. Wakristo nao watafanya Kikristo Kristo. Sasa jitihada ya Wakristo ni kuwavuta Waislamu wafanye mambo yao yote Kikristo Kristo.

Kwa hayo yote mnapaswa kujua kwamba Waislamu hatujawa huru kabisa katika nchi yetu. Sasa hivi tu watumbwa chini ya bendera ya Ukristo. Ni lazima tujikomboe.

Myahudi alimvua binti wa Kiislamu ushungi, Mtume (s.a.w.) akatangaza vita vya Jihadi na Mayahudi.

A. Juma,
Dar es Salaam.



Hijab si ruksa, ni sheria!

Ndugu Mhariri

HIJAB ni nguo ambayo inasitiri mwili wa mwenye kuivaa kama sheria inavyomuamuru. Hivyo ninashangazwa na kauli ya Waziri wetu Prof. Juma Kapuya ya kuwaomba radhi Wabunge ambao walidai kuwa analeta udini kutokana na kuruhusiwa kwa wanafunzi katika swala zao kuu na mavazi yanayoendana na dini zao.

Cha kushangaza ni kwamba Wabunge wote 16 waliodai kuwa huo ni udini ni Wakristo nasi tukisema kuwa Mhe. Kapuya amefanya udini kwa kukubali hoja za Wakristo nao tutakuwa tumefanya kosa?

Jambo la msingi serikali inatakiwa itambue kwamba hijab si ruksa bali ni sheria, tena sheria ambayo isiyorekebishika kwa sababu imewekwa na Mwenyewe Muumba wa kila kitu ambaye anakijua kila alichokiumba na nini kinastahiki ili kuleta salama na utulivu kwacho na vinginevyo.

Hivyo Muumba huyo huyo mwenye kumjua binaadamu alivyo ndiye aliyemwamuru mwanamke juu ya uvaaji wa hijabu kwa ajili ya stara yake na ya viumbe wengine.

Kwa sababu hiyo serikali inapaswa itambue kwamba mwanafunzi yeyote wa Kiislamu mwenye msimamo halisi wa Uislamu na mwenye kuelewa faida azipatazo mwenye kuvaa hijab na khasara za mwenye kuiacha hijab basi hata serikali imfanye nini mwanafunzi huyo hatoivua hijab yake na wala hataacha ibada zake. Kwani twafahamu kuwa "hakuna ruksa ya kumtii kiumbe kwa kumuasi Mwenyezi Mungu (s.w.)".

Vile vile ninapenda kuwawekea wazi kuwa watakaowapata katika mtego wao huo ni wale wanaofanana na wao na wala sio Waislamu kwa maana halisi ya Uislamu. Na ndiyo makafiri wanavyozidi kuithibitisha Qur'an:

"Na wala hawatakuwa radhi (kwako) Mayahudi wala Manaswara (Wakristo) mpaka ufuate mila zao". (Qur. 2:120).

Rahma bint Salum,
P.O. Box 72740,
Dar es Salaam.



Sheikh Mbukuzi njoo Tanga pia

Ndugu Mhariri

NIMESOMA kupitia gazeti lako la Julai 9, mwaka huu kuwa Amir wa Baraza (Shuura) la Maimamu mkoa wa Dar es Salaam Sheikh Juma Mbukuzi kwa niaba ya Maimamu wenzake ametoa kauli ya kumkemea Katibu Mkuu wa CCM Bwana Philip Mangula juu ya kitendo chake cha kuukashifu Uislamu na kuwadharau Waislamu kwa kuwaita ni wala rushwa na Misikiti yao ni mapango ya rushwa.

Kauli hiyo ya Amir Mbukuzi inafaa kupongezwa na kila Muislamu popote pale alipo bila kujali mipaka ya mkoa wa Dar es Salaam kijiografia inapoishia.

Maovu kama hayo hivi sasa wanafanyiwa Waislamu wengi hasa hasa hapa petu Tanzania.

Sisi Waislamu wa Tanga tunakuomba ututembelee ili tukueleze na vituko vingine vinavyofanywa na viongozi wa mkoa huu wa serikali na chama tawala pia jinsi wanavyoboronga mambo bila kujali imani zetu.

Abdallah Mwakitara,
Duga,
Tanga.



Kama mmelala msiwalaumu walio macho

Ndugu Mhariri

NAOMBA nisajili masikitiko yangu na kuwashangaa wale Waislamu wanaowalaumu Wabunge waliofoka Bungeni hivi karibuni wakidai kuwa kuwaruhusu wanafunzi kwenda kuswali Ijumaa ni udini.

Wao wametekeleza wajibu wao wa kuupiga vita Uislamu. Kama nyinyi hampo tayari kutekeleza wajibu wenu, msiwalaumu walio makini kutekeleza wajibu wao.

Mariam Ali,
Tanga.



Mmewaelewa Wabunge?

Ndugu Mhariri

NAOMBA unipe nafasi kidogo ikiwa ni mara yangu ya kwanza kuandika barua katika gazeti hili.

Nina wasiwasi kuwa wananchi wengi hawakuwaelewa Wabunge pale walipodai kuwa wanafunzi kuruhusiwa kushiriki sala kuu za dini zao ni udini.

Walichosema ni kuwa Wakristo washiriki sala zao kuu Jumapili na Jumamosi. Ila Waislamu kupata masaa mawili kuswali Ijumaa marufuku kwani huo ni udini.

Salamu za Wabunge ndio hizo. Wanasubiri majibu kama yapo.

Adam Chakindo,
Manzese,
Dar es Salaam.



Vyombo vya habari chungeni amani nchini mwetu

Ndugu Mhariri

NAPENDA kuchukua nafasi hii finyu kupatikana kuelezea yangu machache juu ya upotoshaji habari unaoendelea kufanywa na baadhi ya vyombo vya habari.

Kutokana na upotoshaji wa vyombo vya habari (magazeti) juu ya kufikisha habari kwa walengwa, umechangia kwa asilimia mia juu ya kushindwa kwa Chama cha Wananchi (CUF) pamoja na kuwa ni wazi kuwa CUF imeshinda majimbo yote. Hila na hiana zilizofanywa na Tume ya Uchaguzi imekuwa ni kielelezo tosha kabisa kuwa CCM imeshinda kwa mbinu.

Mfano ulio hai, gazeti moja la Julai 10, mwaka huu siku ya Jumamosi limeonyesha wazi kabisa juu ya wagombea wa CUF wote (majimbo ya Temeke na Ubungo) hawakutoa picha zao kwa kuona kuwa ni kukipigia debe chama cha wananchi (CUF) la msingi waliloliona ni kuandika CUF wamevunja ndoa yao na TLP (ndoa ya mkeka) na kuwatoa wagombea wote wawili wa CCM picha zao. Si hayo tu na maneno yasiyo na msingi wowote hasa ukizingatia siku iliyofuata ndiyo siku ya Upigaji kura wenyewe.

Mpenda amani,
Seushi HB,
Same.



Ondoeni kwa mikono yenu, msilalamike!
 

Ndugu Mhariri

NAPENDA niwaombe wanafunzi wenzangu kwamba waondokane na utamaduni wa kulalamika na kusoma risala nyingi.

Sasa tuangalie tutakavyopambana wenyewe huko huko shuleni kwetu na waalimu watakaotuzuia kuswali Ijumaa au kuvaa hijaabu. na kama ni risala iwe ni ya kuwaeleza wazazi wetu na Waslamu wote wakisikia mayowe, wajue tunapambana na mawakala wa kuupiga vita Uislamu waliopo mashuleni.

Lazima tupige hatua tutalalamika hadi lini na tunamlalamikia nani? Wakati Bunge na serikali ishatoa msimamo wake?

Je, kulalamika kwetu juu ya kuuliwa Waislamu Mwembechai kumesaidia kitu?

Mwanafunzi mwenzenu
Ahmad Kimaro,
Dar es Salaam.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook