CHAKULA NA LISHE
 
Wagonjwa wanywe maji zaidi
 

Na Mujahid Mwinyimvua
 

MAJI ni kitu muhimu sana katika mwili wa binadamu. Zaidi ya asilimia 55 ya mwili wa binadamu ni maji. Kwa wastani, kila mtu anahitaji maji ya kunywa lita 2.5 kila siku.

Hata hivyo, mahitaji hayo kama nilivyosema ni wastani, kwa sababu yanaweza kubadilika kwa sababu mbalimbali. Kwa mfano majira ya joto mwili unahitaji maji zaidi ya yale yanayohitajika wakati wa baridi. Au mtu mgonjwa (hasa wa homa au kuharisha) anahitaji maji zaidi kuliko mtu asiyekuwa na ugonjwa.

Mwili hupoteza maji mengi wakati wa joto kali, kazi ngumu na wakati wa ugonjwa. Kwa hiyo, lazima mtu anywe maji zaidi wakati huo ili kuziba pengo lililojitokeza.

Sambamba na hilo, mgonjwa hasa wa homa akinywa maji mengi yatasaidia kupunguza joto mwilini, sawia na kuwezesha mwili kufanya kazi yake vizuri. Kama kazi hiyo ni kama vile usagaji wa chakula tumboni.

Zaidi ya hayo, mgonjwa akinywa maji mengi yatasaidia kuzimua (to dilute) sumu iliyo mwilini mwake, ambayo imezalishwa na vijidudu vya maradhi (pathogens) au imetokana na kazi zinazofanyika mwilini. Vile vile, maji mwilini huiondoa sumu hiyo kwa njia ya mkojo.

Bila kusahau, mwili unapokuwa na ugonjwa hasa homa kali, kazi mbalimbali mwilini huathirika. Katika hali kama hiyo, mwili unapopata maji ya kutosha athari ya ugonjwa hupungua kwa kiasi fulani. Na pia, kama mwili ukipata dawa, dawa hiyo inaweza kufanya kazi vizuri.

Ni kutokana na ukweli huu, wahenga walisema kwamba maji ni uhai, na pia maji ni dawa namba moja.

Ni vyema pia, nikasisitiza kuwa maji ninayoyazungumzia hapa ni yale yaliyo safi na salama. Kuna baadhi ya nchi ambapo maji safi na salama yanapatikana kwenye mabomba ya ummah (public water supply). Lakini hapa kwetu Tanzania likiwemo jiji la Dar es Salaam (ambapo ofisi ya Rais ipo), maji safi na salama hayapatikani kwenye mabomba ya umma.

Ndiyo kusema, maji yanayosambazwa kwa wananchi na mamlaka mbalimbali za maji safi na maji taka siyo safi wala salama. Jambo hili ninalolisema ni zito na linawaudhi wakubwa linapoandikwa kwenye magazeti. Kwa sababu 'wakubwa' wengi wanapenda wasifiwe tu bila kukosolewa pale wanapokosea, au wanaposhindwa kutimiza ahadi zao kama hii ya kuwapatia wananchi maji safi na salama.

Ili kuondoa hoja ya 'wakubwa' watakaotaka ushahidi wa 'kisayansi' kuhusu ubora wa maji ya bomba, nawaomba wananchi wafanye zoezi dogo lifuatalo ambalo halihitaji shahada ya Chuo Kikuu wala elimu ya shule ya msingi au ile ya ngumbalu.

Chota maji ya bomba kwenye ndoo na yaweke kwa masaa sita au zaidi. Halafu, yatie taratibu kwenye chombo kingine. Angalia tope (uchafu) uliobakia kwenye ndoo. Nina hakika utaona uchafu ambao hutapenda tena kutumia maji ya bomba ya umma (public water supply) kama utakuwa na njia nyingine ya kupata maji.

Kwa hiyo, ninaposema wagonjwa (na wale wazima) wanywe maji safi na salama kwa mazingira ya Tanzania, ninakusudia yale maji yaliyochemshwa na kuwekwa kwenye chombo safi.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook