MASHAIRI
 

Ya Temeke na Ubungo
 

Wako wapi wakufunzi, wenye elimu na bongo,
Watanzuwe hizi tanzi, zenye kurudisha lengo,
Awe mmoja muhunzi, arande kwenye ulingo,
Ya Temeke na Ubungo, lengo twarudishwa wapi?

Tunarudishwa kwa juzi, kwenye kimoja kitengo,
Liwe moja hili shanzi, agawe yeye unyango,
Kama mpo watetezi, mwajuwa hii mipango?
Ya Temeke na Ubungo, lengo twarudishwa wapi?

Haja kidumu kimoja, ndani ya mingi milango,
Ajisifiye usoja, ndiye bingwa kwenye tungo,
Awe peke yake meja, wengine wote waongo,
Ya Temeke na Ubungo, lengo twarudishwa wapi?

Kwa hizi ndogo chaguzi, baba kajazwa usongo,
Ananyang’anya kwa wazi, wanyonge twakata shingo,
Keshaanza udakuzi, kuwatia watu chongo,
Ya Temeke na Ubungo, lengo twarudishwa wapi?

Ifikapo zamu yake, kunyang’anywa lile tango,
Agaridhia atoke, kiti akae Tinyango,
Hatosukuma mateke, makombora na vigongo,
Ya Temeke na Ubungo, lengo twarudishwa wapi?

Wajuzi wenye elimu, kina Soselo na Shango,
Fanyeni kila jukumu, liondoke hili zongo,
Ugonjwa huu kudumu, tunageuzwa kaango,
Ya Temeke na Ubungo, lengo twarudishwa wapi?
 

S.C. Gonga,
S.L.P. 15068,
Dar es Salaam.


Kuweka kali halali? (Sapoti)
 

Bismillahir naanza, kwa jina lake jalia,
Nataka kuwaeleza, yale yalotangulia,
Mwenzetu katueleza, Mungu alomjalia,
Kuweka kali haramu, kwa amri yake Mola.

Amri ni yake Mola, Jabiri nakuambia,
Mola kaiharamisha, na Mtumewe pia,
Laana wameahidiwa, wale walokaidia,
Kuweka kali haramu, kwa amri yake Mola.

Wanashangaza hakika, wale wanaojisifia,
Eti wao wanataka, mume kumfurahishia,
Huku linaharibika, umbo lao asilia,
Kuweka kali haramu, kwa amri yake Mola.

Laana ikikupata, nani takusalimisha,
Faida utayopata, hakuna wakumshirikisha,
Madonda utayapata, nani atakuponesha,
Kuweka kali haramu, kwa amri yake Mola.

Mola katutunukia, umbo linalopendeza,
Na nywele akatujalia, ili kichwa kukijaza,
Wala hakutuambia, kali kuitumbukiza,
Kuweka kali haramu, kwa amri yake Mola.

Hijab inawatoka, kali wanapojitia,
Kote kote watataka, kali kujionyeshea,
Madhara yatawafikia, si yakujijutia,
Kuweka kali haramu, kwa amri yake Mola.

Mungu ametuambia, yale aliyokataza,
Naye akatuambia, sheria zenye kuongoza,
Nakuweka pia, Mungu ametukataza,
Kuweka kali haramu, kwa amri yake Mola.

Tamati natamatia, ujumbe huu siku,
Jabiri kumsaidia, yale alohubiria,
Dini kuizingatia, kwa mujibu wa sheria,
Kuweka kali haramu, kwa amri yake Mola.

Fatma Saleh,
Kibasila Sec. School,
P.O. Box 20378,
Dar es Salaam.


Wake kudai talaka (swali la msisitizo)
 

Habari zinasikika, kupitia gazetini,
Wake kudai talaka, madai mahakamani,
Hivi kweli tutafika, hasa sisi waumini,
Wake kudai talaka, sheria au ubabe?

Mahakama kitwaghuti, kuamuwa waumini,
Hamuoni tafauti,  tunajitowa Manani,
Wakati hautupiti, sasa tujikwamueni,
Wake kudai talaka, sheria au ubabe?

Ndoa zetu madhubuti, sheria za vitabuni,
Amri hiyo thabiti, tangu enzi za zamani,
Na ndani ya Taurati, imenenwa usizini,
Wake kudai talaka, sheria au ubabe?

Wake kwenda kwa pilati, talaka kuzibaini,
Huwa kwetu misibati, kama sisi tuna dini,
Sawa wale Wagalatia, hawana matumaini,
Wake kudai talaka, sheria au ubabe?

Nimefanya utafiti, sababu zake ni duni,
Kama sale hawapati, wanaanzisha uhuni,
Na ngoma ya benibati, ruhusa mukiwahini,
Wake kudai talaka, sheria au ubabe?

Temeke na katikati, kwingine kote nchini,
Kila mwenye hisabati, ndoa kitu cha thamani,
Tuacheni usharati, mabalaa hamuoni,
Wake kudai talaka, sheria au ubabe?

Sisi wanaharakati, sasa tukae makini,
Dini iwe katikati, kwa sheria hukumuni,
Tusipitwe na wakati, itakuwa mtihani,
Wake kudai talaka, sheria au ubabe?

Hapa mimi ni tamati, enyi wake waumini,
Mkae mjizatiti, ndoa zenu heshimuni,
Na muzifatie shuruti, waume zetu tiini,
Wake kudai talaka, sheria au ubabe?

Zuberi Mohammed Mwinyi (Amir),
S.L.P. 61428,
Dar es Salaam.

--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook