SAYANSI NA TEKNOLOJIA
 
 
Windows: Mambo Mazuri ya Kuyajua

 
Tunaendelea na kutaja mbinu na ujanja wa kuifanya kompyuta yako inayotumia Windows 95/98 ifanye kazi vizuri zaidi wakati unapoitumia, au uweze kutatua matatizo mbali mbali yanayoweza kutokezea.
 

Kompyuta imegoma ghafla - ufanyeje?

Kutokana na sababu mbali mbali, kompyuta inayotumia Windows 95/98 inaweza kugoma ghafla na ikasita kufanya kazi uliyoiamrisha ifanye. Ikitokezea hivyo, utahitaji kuifunga programu iliyosababisha kompyuta kugoma (yaani ku-crash) kwa kubonyeza "saluti ya vidole vitatu," (three-finger salute), yaani Ctrl+Alt+Del. Maana yake ni kuwa unabonyeza Ctrl na kuishikilia, kisha unabonyeza kifungo cha Alt, nacho unakishikilia, na mwisho unabonyeza mara moja tu kifungo cha Del, yaani chenyewe usikishikilie. Ukikishikilia, au ukibonyeza Ctrl+Alt+Del mara mbili, kompyuta yako itajianzisha upya, yaani ita-reboot.

Ukibonyeza Ctrl+Alt+Del kikawaida hutokezea dirisha la Close Program. Kwa kutumia dirisha hilo, chagua jina la programu iliyogoma kutoka kwenye orodha itakayoonekana, na ubonyeze End Task. Ukifanya hivyo, programu iliyogoma itafungwa na kukuwezesha kuendelea kuitumia kompyuta yako kama kawaida. Kama dirisha hilo halikutokezea, kwanza jaribu kubonyeza Alt+Tab (yaani kifungo cha Alt na kifungo cha Tab kwa pamoja). Ukifanya hivyo mara kadhaa utaweza kuingia kwenye programu zote zilizofunguliwa na utaweza kuzifunga kama kawaida. Baadaye jaribu kubonyeza Ctrl+Esc, (yaani kifungo cha Ctrl na kifungo cha Esc kwa pamoja). Ukibonyeza vifungo hivyo utapata nafasi ya kubonyeza Start na hivyo kuweza kuchagua Shut Down na kuifunga kompyuta kwa njia za kawaida na za usalama. Kama njia zote hazikufaa, basi itabidi uianzishe upya kompyuta kwa kutumia kifungo cha RESET kilicho kwenye kompyuta yenyewe, (sio kwenye keyboard). Kompyuta ikiwa imegoma kisawasawa, hata siku moja usiizime kwa kutumia swichi yake ya umeme. Kufanya hivyo kunaweza kuiharibu hard disk drive.

 

Programu Iko Mbali
 

Kuna baadhi ya program ambazo mtu anazitumia mara kwa mara. Kwa mfano, Windows Explorer, au MS–DOS Prompt. Kikawaida kuzifikia programu hizo inabidi kubonyeza Start, kisha Programs, na ndio upate nafasi ya kuzichagua programu hizo kwenye orodha ndefu ya programu zilizo kwenye kompyuta hiyo. Huo ni udhia unaopoteza muda bure.

Kurahisisha namna ya kuzifikia programu hizo na nyengine unazopenda kuzifikia kirahisi, fuata hatua zifuatazo:

  1. Bonyeza Start -> Settings –> Taskbar –> Start Menu Programs –> Advanced.
  2. Kwenye upande wa kushoto wa dirisha la Exploring – Start Menu litakalotokezea, kwenye sehemu ya All Folders, bonyeza alama ya + iliyo mbele ya Programs, kisha bonyeza gurupu la programu (k.m Programs, Accessories, n.k), lenye programu unayoitaka . Kwa mfano kama programu unayoitaka ni Windows Explorer chagua Programs.
  3. Ukishaiona programu unayoitaka kwenye upande wa kulia wa dirisha la Exploring – Start Menu, ibonyezee kifungo cha kulia cha mouse na uchague Copy kutoka kwenye orodha ya mambo (menu ) itakayojitokeza.
  4. Kwenye upande wa kushoto, tafuta Start Menu, na uibonyezee kifungo cha kushoto cha mouse na uchague Edit -> Paste kutoka kwenye menu ya dirisha la Exploring – Start Menu.
  5. Lifunge dirisha la Exploring – Start Menu kwa kuchagua File -> Close, kisha bonyeza OK kwenye dirisha la Taskbar Properties. Ukibonyeza Start tena utaiona programu yako kwenye sehemu ya juu ya orodha ya programu itakayotokeza, na hivyo kuweza kuifungua programu yako kwa urahisi zaidi.
 

Laptop Isiyo na CD–ROM Drive

 
Una kompyuta ya aina ya laptop ambayo ni ya zamani kidogo, na haina CD–ROM drive, na ukataka kuweka kwenye laptop hiyo, programu fulani iliyo kwenye CD - utafanyaje?

Kama laptop yako inatumia Windows 95/98 unaweza kutumia njia ya Direct Cable Connection (tuliyoieleza kwenye makala za nyuma za gazeti hili), kuweza kuiweka programu hiyo kwenye laptop yako, kwa kupitia CD–ROM drive iliyo kwenye kompyuta nyengine yoyote ile inayotumia Windows 95/98.

Je, kama hard disk drive iliyo kwenye laptop yako (isiyo na CD-ROM drive) imeharibika na ukawa umeweka hard disk drive mpya kwenye laptop hiyo, na ukawa huna disketi zenye Windows 95, bali una CD tu yenye Window 95 - utafanyaje kuweka Windows 95 kwenye laptop hiyo?

Kumbuka, kwa hali hiyo huwezi kutumia Direct Cable Connection, kwa vile laptop yako bado haijawekewa Windows 95 kwa vile hard disk drive ni mpya!

Tatizo hili halina njia ya rahisi ya kulitatua. Kwanza, hakikisha kuwa baada ya kutengeneza partition kwenye hard disk drive mpya, umei-format kwa kutumia amri:

FORMAT C:

Itabidi pia uwe na disketi tupu kadhaa. Kama unahitaji kuiweka Windows 95B yote kwenye disketi, basi utahitaji kuwa na disketi tupu 42. Kama haja yako ni kuihamisha tu Windows 95B kutoka kwenye CD na kuingia kwenye laptop yako, basi hata disketi tupu mbili tu zitatosha. Pia utahitaji kutumia kompyuta nyengine yenye CD–ROM drive. Kompyuta hiyo, itabidi ama iwe na WinRAR au WinZip. Binafsi napendelea zaidi WinRAR. Vizuri zaidi, ichukue laptop yako ili iwe karibu na hiyo kompyuta yenye CD-ROM drive.

Iingize CD yenye Windows 95B, kwenye CD-ROM drive. Tumia WinRAR (au WinZip), kuyabana mafaili yote yaliyo kwenye CD hiyo, na pia kuyakata vipande vyenye ukubwa wa 1457500 bytes ili viweze kuenea kwenye disketi. Utahitaji kuyakata vipande kwa vile kuna mafaili ambayo ni makubwa zaidi ya 1.44MB inayoweza kuingia kwenye disketi za kawaida.

Ukitumia WinRAR, kwanza yachague (highlight) mafaili yote yaliyo kwenye CD, na kisha bonyeza Commands na uchague Add files to archive. Kitakachotokezea ni dirisha kama linavyoonekana kwenye Picha 1. Picha hiyo pia inaonyesha namna utakavyoiseti WinRAR kuweza kutengeneza vipande vya 1457500 bytes, na pia kuyafanya mafaili yatakayofanyika kuwa self-extracting yaani yenye uwezo wa kujifungua yenyewe. Kazi hiyo kubana na kuyakata mafaili, itafanyika kwa upesi zaidi kama mafaili yatakayofanyika utayahifadhi kwenye hard disk drive – yaani kwa mfano, jina la Archive liwe C:win95b.exe ili mafaili yatunzwe kwenye drive C:. Utafanya hivyo kama hard disk drive ya kompyuta yenye CD-ROM drive ina nafasi isiyopungua 65MB. Kama haina nafasi ya ukubwa huo, basi unaweza kutengeneza mafaili yenyewe moja kwa moja kwenye disketi kwa kuandika jina la Archive kuwa A:win95b.exe. Na kama una disketi chache tu, basi itabidi kila WinRAR ikimaliza kuingiza faili kwenye disketi, wakati huo huo unaiingiza kwenye laptop na baadaye unaifuta tayari kuiruhusu tena WinRAR kuingiza faili jengine kwenye disketi hiyo. Faili la kwanza, kwa mfano huu, litakuwa na jina win95b.exe. Baada ya kuiingiza disketi yenye faili hilo kwenye laptop, ni kiasi cha kutoa amri:

A:win95b

Ukifanya hivyo utaulizwa ni kwenye jalada (directory) gani faili hilo lifunguliwe. Ni vyema uwe tayari umetengeneza kwenye hard disk drive ya laptop, jalada C:\win95b ili ulitumie hilo kuhifadhi mafaili ya Windows 95B.
 

Picha 1: Kutumia WinRAR kubana mafaili na kuyakata vipande vya ukubwa wa 1457500 bytes.
 

Kila ukimaliza disketi moja utaambiwa uingize disketi ya pili mpaka mafaili yote yatakapokuwa tayari umeyaingiza kwenye hard disk drive ya laptop yako. Ukisha maliza kuyanakili, utaiweka Windows 95 moja kwa moja kwa kutumia mafaili yake uliyoyaweka kwenye hard disk drive ya laptop yako kwa kutumia amri :

C:\win95b\setup

Baada ya kuiweka Windows 95 kwenye laptop yako, unaweza kuyafuta mafaili uliyoyanakili kwenye C:\win95b ili upate nafasi zaidi. Lakini kama huna tatizo la nafasi, ni vyema ukayaacha bila ya kuyafuta kwani yanaweza kuhitajika wakati wa kuweka baadhi ya programu au vifaa vya kompyuta.

Mbinu hii unaweza kuitumia pia kuweka kwenye laptop isiyo na CD-ROM drive, programu nyingine yoyote ile inayokuja kwenye CD.

ANGALIA: Ukihitaji nakala ya WinRAR unaweza kuipata kutoka kwenye Internet au pia ulizia kutoka kwenye ofisi za gazeti la AN-NUUR.