TAHARIRI
 
Umoja ushavunjika sasa ni kuujenga
 

TUNAPENDA sana kuwasikia viongozi wetu wa serikali wakizungumzia athari za kuvunjika kwa amani, umoja na mshikamano. Na kwa kweli si kupenda tu bali tunatafakari na kuzingatia kwa uzito wake kauli za viongozi hao. Tunafanya hivyo sio kwa kuwa tunapenda sana kusikia sauti za viongozi wetu au ufundi wao wa kupanga maneno; lakini kwa sababu hatupendi amani yetu ivunjike wala umoja wetu uparaganyike. Na kwa kadri tunavyoyafuatilia mambo suala sasa si kukemea na kutoa tahadhari, bali kudhibiti ufa usizidi kupanuka na kuanza kujenga madaraja ya kututenganisha.

Lakini kama mgawanyiko umetokea wakati hotuba zinaendelea, inaonyesha kuwa kauli na maneno matupu si yenye kusaidia kitu. Kwa hiyo tunapoingia katika awamu ya kuzuia mgawanyiko usiendelee tujue si kwa kauli tena bali kwa vitendo huku tukiyajenga upya madaraja ya kutuunganisha.

Lakini tunapozungumzia kujenga upya umoja wetu ni lazima tuwatambue wale walioyavunja madaraja yanayotuunganisha. Hao ndio watakaowajibika kuyajenga na hao ndio wanaopaswa kugharamia ujenzi huo.

Tulipopigania uhuru, wazee wetu waliangalia nchi na maslahi ya wananchi. Ndio maana japo walianzisha harakati hizo walikuwa Waislamu wa Dar es Salaam, waliwapokea wapigania uhuru wenzao Wakristo toka Bara na kuwahifadhi katika majumba yao. Lakini wakati wao wakifumbia macho tofauti zao za kidini, Dk John Sivalon amesema kuwa Wakristo kwa upande wao waliwaona Waislamu kama maadui. Jambo lililopelekea Jumuiya zao kama EAMWS kuvunjwa huku zile za Kikristo zikipewa kila msaada.

Lakini kubwa zaidi Dk. Sivalon anasema kuwa viongozi wa serikali walio Wakristo walijenga fungamano na makanisa yao, jambo lililofanya utendaji na maamuzi ya serikali yawe sawa na ya kanisa. Na hali hiyo Waislamu wanaitafsiri kuwa ndiyo iliyopelekea watoto wao kunyimwa elimu na kupunjwa katika ushiriki wao katika kuendesha nchi.

Haiwezi kuwepo hali hiyo ukasema kuwa mshikamano bado upo. Swali ni je, waliovunja daraja la kutuunganisha hapa ni akina nani!

Wakristo wamekuwa wakiutumia uhuru wao wa kuabudu na kuhubiri dini yao ambapo wamekuwa wakipita nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa, ofisi kwa ofisi na shule kwa shule wakigawa maandiko na kuwataka watu wamkubali Yesu kuwa ni Mungu na kwamba kafa msalabani kwa ajili ya dhambi zao.

Serikali kwa kutambua uhuru na haki hii imekuwa kiwaachia Wakristro wajenge majukwaa na kuhubiri katika kila uwanja wa wazi na viongozi wenyewe wa serikali kushiriki kufungua mikutano na kushiriki nyimbo za pambio.

Kwa Waislamu imekuwa ni kesi tofauti. Kila leo wako mahakamani na rumande wakituhumiwa kukashifu dini nyingine kwa kunukuu kwao maandiko matakatifu yanayosema "Yesu si Mungu". Je hapo unategemewa uwepo umoja na mshikamano baina ya Wakristo na Waislamu!

Wakati wimbi la kuwakamata Waislamu likiendelea huku juhudi za Waislamu kutekeleza wajibu wao wa kuihubiri dini yao ukiimarika waliibuka Wakristo waliowarushia Waislamu na Uislamu makombora ya matusi na kashfa bila ya kutoa ushahidi wowote katika maandiko yanayotambulika.

Hao hatukuona hekaheka ya kuwakamata. Lakini hata pale walipowakamata ilikuwa ni kiini macho tu. Kwani waliingia mlango wa mbele na kutokea mlango wa nyuma huku wakiwaacha Mzee Chatta Abdallah Kidagaa na Mzee Katambo wakisota gerezani kwa miezi bila ya dhamana. Wazee wale walikosa nini?.

Mwongozo na vigezo gani walitumia polisi na mahakimu Wakristo kuwaweka ndani wazee wale miezi kadhaa huku wakiwaachia huru kina Cecil Simbaulanga. Je, hapo bado tunajihesabu wamoja? Je, daraja la kutuunganisha bado lipo?

Jumuiya ya Waislamu ya Chuo cha Ushirika Moshi ilipata kupewa kiwanja na uongozi wa Chuo ili wajenge Msikiti. Haikupita muda baada ya ujenzi huo kuanza Watawa wa Kanisa Katoliki wakaamrisha kupitia serikali (Mkoa) ujenzi huo uzuiwe. Serikali ilitii na ikazuia ujenzi wa Msikiti huo.

Je, mbele ya viongozi wa serikali upo usawa kati wa Waislamu na Wakristo! Je, kama ipo hatari ya kuwagawa watu kwa misingi ya dini nani anayewagawa!

Wakati wanafunzi Wakristo wanapewa siku mbili za ibada, wanafunzi Waislamu wanategemea huruma ya mwalimu mkuu kwenda Ijumaa. Na hata huyo mwenye huruma atawaruhusu wakashwali huku wenzao wakiendelea kusoma.

Je, hali hiyo ni ya kutolea ilani ya hatari ya ubaguzi au tayari upo na je ubaguzi huo waweza kuwa daraja la kutunganisha! Yaweza kuonekana jambo la kuchosha kwa kurejewa mara kwa mara swala la Mwembechai, lakini swali ni je, kipi kiliisukuma serikali itumie jeshi la polisi lilliloishia kuwaua Waislamu kwa kufuata kauli ya Paroko wa Kanisa Katoliki. Serikali ilipochukua hatua zile imezingatia kuwa upo usawa wa kikatiba na kisheria kati ya Paroko yule na Waislamu! Je, hatua zile zilikuwa za kujenga au kuyabomoa madaraja yanayotuunganisha!

Tunapoyaandika haya baadhi ya Waislamu wapo korokoroni. Wamepelekwa huko baada ya kuchukua hatua ya kuonyesha hisia zao dhidi ya Wabunge Wakristo walioonyesha chuki zao dhidi ya Waislamu ndani ya Bunge.

Suala la Wabunge wale kuwa na chuki dhidi ya Waislamu haionekani kuwa ni tatizo. Tatizo limegauzwa kuwa hawa wanaopinga Wabunge kutumia nafasi zao kuupiga vita Uislamu.

Kina Sheikh Juma Mbukuzi wasingekuwa ndani leo kama si Wabunge wale Wakristo kumshambulia Mbunge mwenzao Muislamu na Waziri kwa kuleta hoja ya serikali inayolinda haki na uhuru wa dini kwa wanafunzi.

Mambo ni mengi lakini itoshe kusema kuwa umefika wakati wa kuukabili ukweli tunzungumzie kuyajenga upya madaraja yaliyobomolewa. Na tusingefika hapa kama viongozi wetu wangekuwa na ujasisi wa kuwakabili waliotuvunjia madaraja yanayotuunganisha.

La kutusaidia sote kama Watanzania ni kuwa viongozi waanze kuwa majasiri waache kuwastahi na kuwaonea muhali wanaotuletea janga hili la kuvunjika kwa umoja wetu.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook