"MHESHIMIWA Spika, ninashukuru sana. Nianze kwa kusema kwamba ninaunga mkono hoja hii ya Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba. (Makofi).
Mheshimiwa Spika, nchi hii imebarikiwa, kupata Mwanasheria Mkuu anayetoka katika kabila bora, kabila kubwa la Kisukuma. Kabila hili nimeandika sifa zake, ni kabila adhimu, kabila muhtarama, kabila nadhifu, kabila lenye wasta, kabila lisilokuwa na hashua na sifa nyingi nyingine wanazo. (kicheko/makofi).
Mheshimiwa Spika, yeye mwenyewe ni kijana aliyezaliwa na kuleleka, ana adabu kwa wakubwa, ana adabu kwa watu wa rika lake, ana adabu kwa vijana. Amebobea katika mabo ya sheria, amebobea pia katika utamaduni wa Kisukuma (kicheko/makofi).
Mheshimiwa Spika, kijana huyu pia amebobea katika utamaduni mwingine wa Kisukuma, nao ni kwamba mwanamke wa Kisukuma akifikia umri wa miaka 50 na macho yake yakiwa mekundu, akiwa mama yako, shangazi yako, dada yako basi ni mchawi huyo lazima auawe. (Makofi).
Mheshimiwa Spika, ninamuombea Mungu, na bila shaka Wabunge wenzangu wanamuombea Mungu pia aendelee na shughuli zake, hata Mungu ampe uhai mrefu atuhudumie vyema. (Makofi).
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo ninaomba sasa uniruhusu niende kwenye Katiba. Katika Katiba, Kifungu Na. 19(ii) kinasema hivi, ninamuomba nikisome: "Bila ya kuathiri sheria zinazohusika za Jamhuri ya Muungano, kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari ya mtu, ya binafsi na shughuli na unendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya mamlaka ya nchi".
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kazi ya kutangaza dini ni yangu mimi mwenyewe. Kutangaza dini ni jinsi ninavyojua mimi bora nisivunje taratibu na sheria za serikali. Kuna utamaduni hapa bungeni umeanza kuingia. Ya kwamba ukisema jambo la dini, ama wewe ni mdini au ni mchochezi, hapana. Ninalozungumzia mimi ni kero. (Makofi).
Mheshimiwa Spika, katika Qur'an Sura ya 5 aya ya 72 inasema hivi: "Bila shaka wamekufuru wale waliosema Mungu ni Issa bin Mariam". Aya ya 73 inasema hivi: "Kwa hakika wamekufuru wale waliosema Mwenyezi Mungu ni mmoja katika wale Waungu Watatu".
Mheshimiwa Spika, nimepata kulizungumzia hili suala, leo ninasema kwa mara ya mwisho ya kwamba kama hivyo ndivyo Qur'an inasema hivi na Katiba ya nchi inaniruhusu kutangaza dini yangu, basi Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba atuambie leo, inakuwaje watu wanaosema Yesu si Mungu ambayo ni maneno yamo katika Qur'an wanakamatwa, wanashitakiwa na kuwekwa mahabusu? Lazima kuna neno, nimesema zamani na leo ninarudia tena. Kuwa hata viongozi wenyewe wa dini ya Kikristo wanasema kwa Muislamu kusema hivyo si kosa. Sasa hili neno kukashifu dini nyingine, dini gani dini ya serikali? Ninaomba Mheshimiwa Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba anipe maelezo. Kwa sababu tukio la mwisho limetokea kwa wale Wanyamwezi wa Nzega. Wamekwenda watu kutangaza dini, wamekamatwa na kushtakiwa. Wamewekwa mahabusu kwa mwezi mzima. (Makofi).
Sasa nataka leo nipate maelezo sahihi. Je, kwa Muislamu kusema Yesu si Mungu hadharani ni kosa la jinai. Je, Qur'an ambayo kwa Muislamu ni kitabu kitakatifu serikali inakiona ni kitabu cha uchochezi, ni kitabu cha kashfa? (Makofi).
Mheshimiwa Spika, juzi juzi hapa, Mheshimiwa Waziri wa Kinyamwezi Ndugu Profesa A. Kapuya, ilibidi aondoe maneno fulani katika hotuba yake, ilisemekana kwamba maneno yale yana udini ndani yake. Yale maneno yalikuwa yanawalazimisha walimu wakuu, kuwapa ruhusa watoto wa Kiislamu kuvaa hijabu na kwenda kusali Ijumaa. (Makofi).
Mheshimiwa Spika, ninarudia tena kwenye Katiba, sehemu inayosema habari za kufanya ibada. Uniwie radhi Mheshimiwa Spika, ninakwenda tena kwenye Qur'an Sura ya 24 aya ya 31 inasema hivi haya ni maneno ya Mungu. Qur'an yote ni maneno ya Mungu kwa imani ya Kiislamu: "Nawaambie Waislamu wanawake, waangushe shungi zao mpaka vifuani mwao". Yaani wavae hijab. Katika sura ya 62 aya ya 9 inasema hivi: "Enyi mlioamini,kukiadhimiwa kwa ajili ya sala siku ya Ijumaa, nendeni upesi kumtaja Mwenyezi Mungu". (Makofi).
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hii ni ibada. Ni ibada ambayo anatakiwa mtu afanye. Ninachotaka kujua mimi, niambiwe taratibu za sheria zinavyosema hapa. Baada ya kuondolewa maneno yale. Mtoto wa Kiislamu anayesoma shule, bado ni wajibu kwake kuvaa hijabu. Au atavaa hijabu at the discretion ya Mwalimu Mkuu? Kwa sababu dini yake inamtaka avae hijabu. Je, mtoto wa Kiislamu anayesoma shule bado Mwalimu atapanga mambo ili ikifika saa 6.00 mchana aende akasali, au asali tu ikiwa Mwalimu anataka, na hii ni ibada. (Makofi).
Mheshimiwa Spika, kuhusu hili, ningependa niambiwe, kwa sababu mambo haya kuna tabia ya watu kuyaona madogo, lakini ni mambo makubwa. Hakuna kitu kikubwa katika dunia kama kuathiri dini ya mtu mwingine. (Makofi).
Mheshimiwa Spika nataka niseme tena wakati wa hotuba ya Waziri wa Elimu na Utamaduni, lakini yalisemwa maneo hapa kwamba Waziri Alhaj Profesa Juma A. Kapuya hafai hata kuwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pengine nilikumbushe Bunge ya kwamba Mheshimiwa Profesa Juma A. Kapuya, sidhani kuwa anataaluma ya dini ya Kiislamu. Alitekeleza tu nguzo moja ya Kiislamu. Lakini Wizara hii ilipata kuwa chini ya Waziri Padre (Ndugu Saimon Chiwanga) alikuwa rafiki yangu mimi; na Spika unamjua kwa sasa ni Askofu na hakuna mtu aliyenung'unika. Sasa huyu Alhaj tu watu wananung'unika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimesema mwanzo, ninarudia ya mwisho. Kwamba nisije nikaambiwa kuwa huyu mchochezi. Huyu ni mdini. Kwa hiyo ninakwenda kwenye Zaburi 56:1-4. Kwa ruhusa yako nitasoma: "Ewe Mungu unirehemu, maana yuko atakaye kunimeza. Mchana kutwa ananionea akileta vita. Adui zangu wanataka kunimeza mchana kutwa maana waletao vita juu yangu kwa kiburi ni wengi. Siku ya hofu yagu ninakutegemea wewe Mungu. Kwa msaada wa Mungu nitalisifu neno lake, nimemtumaini Mungu na mimi namtumaini Mungu, sitaogopa. Ninarudia, nimemtumaini Mungu, sitaogopa wewe mwenye mwili utanitenda nini?". (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru
sana. (Makofi)".
--
|
|