WAISLAMU wapatao 30 akiwemo Amir Sheikh Juma Mbukuzi wako rumande kufuatia kulalamika kuwa serikali haitendi haki kwa baadhi ya raia wake.
Waislamu hao walikamatwa Ijumaa iliyopita katika Msikiti wa Manyema Kariakoo ambako walikusanyika baada ya maandamano ya amani waliyopanga kufanya siku hiyo kuzuiliwa na polisi.
Pamoja na mambo mengine Waislamu wanalalamika kwamba wanafunzi Waislamu mashuleni na vyuoni hawapati haki ya kutekeleza maamrisho ya dini yao kulinganisha na wanafunzi walio waumini wa dini ya Kikristo.
Kwa mujibu wa Tamko la Maimamu lililopelekwa kwa Spika wa Bunge wiki mbili zilizopita, wanafunzi Waislamu hawaruhusiwi kuvaa sare za shule zenye kuzingatia mipaka ya dini na hawapati fursa ya kuhudhuria swala ya Ijumaa.
Wanafunzi Waislamu wamekuwa wakikabiliwa na upinzani mkali wanapotekeleza mambo hayo hususan swala ya Ijumaa ambapo hulazimika kuchagua ama kwenda kuswali kukosa vipindi au kuendelea na vipindi kukosa swala.
Aidha, suala la hijab limekuwa kitendawili kwa wanafunzi hao licha ya kuwepo waraka unaowaelekeza wakuu wa shule na walimu wakuu kuanza kutekeleza mara moja.
Pamoja na madhila hayo Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wakichangia makadirio na makisio ya Wizara ya Elimu walikemea vikali hoja iliyowasilishwa na Waziri Kapuya iliyolitaka Bunge kulipa kibali suala hilo.
Katika hoja zao Wabunge hao walidai kuingiza suala la hijab mashuleni na kuruhusu wanafunzi Waislamu kuhudhuria swala ya Ijumaa ni udini unaoweza kuhatarisha amani ya nchi.
Wabunge hao walimtaka Waziri Kapuya aondoe hoja hiyo kama sharti la kupitisa Bajeti yake. Kufuatia shinikizo hilo Profesa Kapuya aliliomba radhi Bunge na kisha kuondoa hoja yake.
Katika kuwakamata Waislamu waliopinga msimamo wa Wabunge, polisi ilidai kuwa watu hao waliandamana bila kibali, wakasababisha fujo maeneo ya Kariako na kuharibu mali ya serikali.
Siku ya Jumatatu watu hao walifikishwa mahakamani ambako baada ya kusomewa shtaka walirudishwa rumande.
Wakati huo huo, baadhi ya watu wamelalamikia uamuzi wa mahakama wakuwarudisha wananchi hao rumande kwa madai kwamba wamenyimwa haki yao ya kikatiba.
Wamesema imekuwa ada kwa watuhumiwa wanaohusishwa na kesi za mambo ya Waislamu kunyimwa dhamana.
Kesi nyingine ambazo watuhumiwa walizuiliwa dhamana kwa muda mrefu ni pamoja na ile ya mabucha ya nguruwe mwaka 1993, kesi ya kadhia ya Mwembechai mwaka wa jana, kesi ya wahadhiri wa Kiislamu Nzega na kesi inayoendelea sasa wilayani Sengerema Mwanza.
Hata hivyo katika kuzuilia
dhamana Mwendesha Mashitaka alitoa hoja kwamba ni mapema mno wakati wa
kupewa dhamana
SHUURA ya Maimamu jijini ilikutana juzi (Jumatano) kujadili kukamatwa kwa Amir wa Shura hiyo na Waislamu wengine wapatao 96 Ijumaa iliyopita.
Kikao hicho cha Shura kilifanyika katika Msikiti wa Morogoro Ilala na kuhudhuriwa na Maimamu wa misikiti 50.
Katika kikao chao pamoja na mambo mengine Maimamu hao walitoa tamko la kulaani kile walichosema unyanyasaji unaofanywa na serikali ya CCM dhidi ya Waislamu.
Kadhalika wamelaani kupigwa na kuwekwa rumande Waislamu na kunyimwa dhamana.
Aidha, tamko hilo limesisitiza madai ya Waislamu dhidi ya serikali. Kikao hicho kilimalizika kwa kuteua Kaimu Amir.
Uteuzi huo ulikwenda kwa Sheikh Karume wa Msikiti Mujahiduun ulioko Mburahati jijini.
Sheikh Mbukuzi na watuhumiwa
wengine watafikishwa tena mahakamni Agosti 16, mwaka huu.
KESI ya madai ya "uchochezi" inayomkabili aliyekuwa Imamu wa Msikiti wa Mwembechai, Sheikh Omar Bashir imeahirishwa tena na mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa madai ya kutokuwepo kwa jalada la shauri hilo mahakamani hapo.
Akiomba kupangwa kwa tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo, Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Bw. Kisusura alidai mahakamani hapo Jumanne ya Agosti 3, mwaka huu kuwa, mpaka sasa hajapokea jalada hilo.
Alidai jalada hili limerejeshwa tena kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DPP) hivi karibuni kufanyiwa masahihisho baada ya kuwepo kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) siku kadhaa zilizopita.
Kesi hiyo yenye nambari 1621 ilifunguliwa na serikali mahakamani hapo mwaka jana na iko mbele ya Hakimu wa mahakama hiyo, Bw. G. Lwakibadila.
Awali, Wakili wa kujitegemea anayemtetea mtuhumiwa, Bw. Twaha Taslima aliiomba mahakma hiyo imfutie mteja wake kesi hiyo kwa hoja kwamba kesi hiyo imekwishachukua zaidi ya mwaka mmoja mahakamani hapo bila kusikilizwa.
Bw. Taslima aliiambia mahakama hiyo kuwa mteja wake anayo haki ya kufutiwa kesi hiyo kulingana na kifungu cha 225(5) cha sheria ya kanuni za mwenendo wa jinai ya mwaka 1984 kinachoruhusu mtuhumiwa kufutiwa kesi husika ikifikisha siku sitini mahakamani bila kusikilizwa na pia mwendesha mashitaka wa serikali (PP) au mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai wa mkoa (RCO) kushindwa kutoa sababu za msingi kuendelea kuwepo kwa kesi hiyo mahakamani bila kusikilizwa.
Wakili huyo alisema kuendelea
kuwepo kwa kesi hiyo mahakamani muda wote huo bila kusikilizwa ni sawa
na kumtwika mteja wake mzigo mzito begani na kuuacha uzidi kumtesa kwa
kumuelemea bila sababu za msingi.
MAAZIMIO ya mkutano wa siku mbili wa wanawake wa Kiislamu uliofanyika hivi karibuni katika Hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar hayakuridhiwa na baadhi ya washiriki waliohudhuria mkutano huo.
Wakizungumza mara baada ya mkutano huo kufungwa na Alhaj Ali Hassan Mwinyi washiriki hao walisema kuwa maazimio waliyoyapendekeza washiriki siyo yaliyowasilishwa kwa mgeni rasmi.
Miongoni mwa mapendekezo ambayo hayakuorodheshwa katika rasimu ya mapendekezo ni serikali kutakiwa kutunga sheria ya watu kutoikaribia zinaa na kuwepo kwa sheria itakayoruhusu Waislamu wanawake kuvaa vazi lao la kisheria shuleni na ofisini bila bughudha.
Aidha, azimio jingine lililotolewa na washiriki ni kuwa wanafunzi wa kike na kiume watenganishwe na ikiwezekana urudishwe mfumo wa kuwa na shule za wavulana na wasichana.
Vile vile washiriki hao walitaka somo la dini ya Kiislamu lifundishwe ipasavyo vijijini, kwa taasisi zinazohusika kutoa waalimu toshelevu kwani utafiti unaonyesha kuwa katika vijiji vingi nchini hakuna walimu wa dini ya Kiislamu.
Washiriki hao pia walipendekeza kuwa Baraza la wanawake wa Kiislamu Tanzania ambalo linatarajiwa kusajiliwa kama Ummu Salamah liwatafutie nafasi za masomo ya juu na fani mbalimbali wanawake wa Kiislamu na kwa kuanzia wapelekwe wanafunzi wa kike kusomea fani ya udaktari ili hatimaye kuondokana na tatizo la wanawake kuhudumiwa na wanaume hasa katika masuala ya uzazi.
Kadhalika washiriki hao walipendekeza kuwa zifanywe juhudi za makusudi kuwapa wanawake wa Kiislamu mbinu na nyenzo za biashara ili ziwasaidie kuinua vipato vyao na vya familia zao.
Walisema wanawake wa Kiislamu wako nyuma sana katika maendeleo ya jamii na hata serikali au vyama visivyo vya kiserikali vinapotoa mikopo kwa wanawake, Waislamu wanaojitokeza kuomba mikopo hiyo ni wachache.
Walisema huenda tatizo ni ukosefu wa elimu kuhusu masuala ya kiuchumi na ushiriki na ushirikishwaji mdogo wa wanawake hao katika shughuli za kijamii.
Maazimio yaliyofikishwa kwa mgeni rasmi ambayo yamepunguzwa makali ni kuwa serikali izingatie kuwa sheria zote zinazomkandamiza mwanamke zinarekebishwa au zinatungwa upya, ambapo wanawake wenyewe washiriki katika kutunga kwani ndio wanaojua matatizo yanayowakabili.
Azimio jingine ni kuwa elimu ya juu kwa wanawake itiliwe maanani ili wanawake wengi zaidi wapate nafasi ya kuelimika.
Aidha, iliazimiwa kuwa waajiriwe Masheikha wanawake katika kamisheni ya Wakfu na mali za amana Zanzibar.
Pia wanawake wapewe nafasi ya kujifunza mafunzo ya kitaaluma ya dini kama vile Fiqh, Sharia, Hadith, Qur'an na kadhalika.
Maazimio hayo yalidaiwa kuwa ni mepesi mno ikilinganishwa na umakini waliokuwa nao washiriki katika kueleza yanayowakera na ambayo wangependa yapatiwe ufumbuzi.
Aidha, washiriki walielezaea
uchukivu wao juu ya wafanyakazi wanawake wa televisheni ya serikali ya
Mapinduzi Zanzibar kuvaa hijab siku za Ijumaa pekee na kuhoji kuwa je Mungu
yuko Ijumaa tu?
--
|
|