UMATI mkubwa wa watu uliohudhuria kikao cha mahakama mjini Sengerema hivi karibuni katika kesi inayowakabili wahadhiri wa Almallid, walipata fursa ya kusikiliza muhadhara usio rasmi.
Katika kesi hiyo shahidi wa kwanza upande wa mashtaka Padri Silvesta Ntabula alitoa ushahidi uliosisimua mahakama.
Katika ushahidi wake Padri Ntabula aliiambia mahakama kuwa siku ya tukio alikuwa akielekea kijiji cha Kalungeche kutoa huduma za kiroho lakini alipofika karibu na mhadhara wa wahubiri hao wa Almalid alivutiwa hivyo aliamua kuahirisha safari.
Alisema kilichomvutia ni igizo la Swala lililofuata mafundisho ya Biblia lililoonyeshwa na wahadhiri hao. Padri aliiambia mahakama kuwa alichukizwa na igizo hilo ingawa kilicho elezwa kilikuwa kama inavyoeleza Biblia.
Aidha alikiri kuwa Yesu hakuwa Mkiristo bali alifuata dini ya asili ya Israel. Padri Ntabula
aliongeza kuwa Waislam kusoma Biblia ni haki yao lakini aliwataka wasomee Msikitini badala ya kwenye viwanja vya wazi.
Alipotakiwa kueleza kashfa ni nini alisema kusema "Yesu si mwana wa Mungu". Hata hivyo mshitakiwa namba mbili alimpa andiko linalothibitisha Yesu si mwana wa Mungu . Kuanzia hapo majibizano ya vifungu vya Biblia baina ya shahidi na mshitakiwa yaliendelea hadi kesi ilipoahirishwa.
Washitakiwa katika kesi hiyo inayoendelea mjini Sengerema ni Athumani T. Manoni, Hussein Abdallah, Twalib Abdallah na Hussein Omar. Wengine ni Ramadhani Shaaran, Idd Swaleh, Abdallah Kabunda na Issa Rashid.
Washitakiwa wote wanatuhumiwa kutoa matamshi yanayodaiwa kuwa ni ya kashfa dhidi ya dini ya kikristo. Kashfa hizo ni pamoja na kusema kuwa Yesu sio Mungu, sio Mwana wa Mungu, hakufa msalabani na wala hakufufuka. Hakimu anayesikiliza kesi hiyo ni bwana L.Raphael.
Taarifa kutoka mjini Sengerema
zinafahamisha kuwa kesi hiyo imewavuta watu wengi ambao wengi hutoka Mwanza
Mjini kwenda kusikiliza.
--
|
|