Maimamu Tanga wachanga kuwasaidia waliokamatwa Dar
 

KATIKA kuelezea hisia zao dhidi ya Wabunge Wakristo na kuwaunga mkono wenzao wa Dar es Salaam, Maimamu mjini hapa wameanza kuchangisha fedha kuzisaidia familia za Waislamu wanaoshikiliwa na polisi.

Mnamo siku ya mwanzo ya harakati hizi Misikiti miwili imeshiriki ambapo jumla ya shilingi 11,205 zimepatikana mara baada ya dua ndefu za kumshitakia Mungu kwa uonevu wa serikali ya Tanzania kwa raia zake Waislamu.

Kwenye Msikiti mdogo wa Makorora Sheikh Makame aliwaambia Waislamu kuwa kuwaombea wenzao wa Dar es Salaam ni wajibu wa kila Muislamu kwani Waislamu wote ni kama kiwiliwili kimoja, kiungo kimoja kikipata maumivu mwili mzima huyahisi maumivu hayo.

Siku hiyo hiyo ya Jumatano, Agosti 4 baada ya sala ya Isha kwenye Msikiti wa Ngazija, barabara ya 10 mbele ya Kituo Kikuu cha magari ya abiria, Imamu wa Msikiti huo Sheikh Swaleh Mwamba aliongoza dua na michango iliyofuatia uchambuzi wa matokeo mengi ya uonevu na kejeli za Wabunge kwa Waislamu uliotolewa na Ustadh Shaibu.

Wazungumzaji waliopata fursa kuchangia waliikataa hoja kuwa kuruhusiwa wanafunzi na waajirwa kuswali kwa masaa mawili siku za Ijumaa na kuvaa hijab ni udini pia hoja za wanafiki kuwa kuelezea madhila haya ni kuleta fujo na kuvunja amani.

Wakati huo huo mkanda wenye kuonesha mauaji ya Mwembechai unatazamiwa kuoneshwa kwenye Msikiti wa Makorora siku ya Jumamosi mara baada ya sala ya Isha, Waislamu kwa wingi wametakiwa kwenda kujionea. Huko huko imelezwa utaratibu wa maonesho na michango utaendelea kutolewa.

Kutoka Mwanza, Waislamu mkoani humo wamemwandikia Mhe. Rais Mkapa wakielezea kulani kwao hatua ya Wabunge Wakristo kutumia chuki zao za kidini kukejeli uhuru wa haki ya Waislamu kuswali Ijumaa na kuvaa hijab.

Katika barua yao ya Agosti 2, wamemuomba Mhe. Rais Mkapa atoe kauli bayana kuhusu uhuru wa haki ya Waislamu katika masuala hayo mawili. 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook