Maoni
 
Nani kasema mnahusika?
 

Jumanne Agosti 3, uongozi wa Msikiti wa Manyema uliitisha mkutano wa waandisih wa habari ambapo walijieleza kuwa wao hawahusiki na maandamano ya Waislamu ya Ijumaa iliyopita. Maandamano ambayo yalilenga kuelezea hisia za Waislamu dhidi ya Wabunge Wakristo walioonyesha hisia zao za chuki dhidi ya Waislamu ndani ya Bunge.

Katika mkutano huo, msemaji wa Msikiti Sheikh Said Hilal alikiri kwamba waliwaruhusu askari waingie Msikitini kuwachukua wanawake.

Aidha, alidai kuwa wao hawamtambui Sheikh Juma Mbukuzi bali wanamtambua Sheikh Mkuu tu (wa Bakwata). Na kwamba wapo bega kwa bega na Imam wao Sheikh Jongo.

Maelezo mengine yaliyotolewa na viongozi ho ni kuwa si kwamba tu uongozi haukushiriki maandamano lakini hata waumini wao pia hawakushiriki. Kabla hapo Imam wa Msikiti huo Sheikh Jongo alikuwa miongoni mwa watu walioitwa kwa Makamu wa Rais ambapo walieleza kutokuhusika kwao.

Aidha, viongozi hao walilalama kuwa kuna baadhi ya watu wanaodai kuwa Msikiti huo ni wa CCM.

Pengine tuanze kwa kusema kuwa hapakuwa na haja ya kujikosha kwani hakuna aliyekuwa ametarajia kila mtu kushiriki fursa hii adhimu ya kuitetea dini ya Allah.

Kama lipo la kushangaza ni kuwashangaa wale waliowaita wasiohusika wakidhani watapata ukweli kutoka kwao, hawataupata.

Aidha, hapakuwa na waumini waliokuwa wanajitokeza kama waumini wa Msikiti fulani wakipingana na wenzao au kuwakaribisha polisi Msikitini. Kinyume chake walionekana watu mahsusi kwa sura zao wakiwa wamezungukwa na polisi wakiwaelekeza waliko waumini.

Swala ya Ijumaa ni amri ya Mwenyezi Mungu, halikadhalika Hijab. Kwa kuzingatia haki na uhuru wa dini kama inavyoainishwa katika Katiba ya nchi, serikali inawapa Wakristo siku mbili kamili kufanya sala zao kuu.

Kwa kuzingatia kuwa haki na uhuru huu wanastahiki pia Waislamu, serikali kupitia hotuba yake ya Bajeti ya Wizara ya Elimu na Utamaduni iliweka vipengele vitakavyothibitisha kupatikana kwa haki na uhuru huo kwa wote.

Katika hali ya kuonyesha chuki, dharau na kejeli juu ya amri ya Allah juu ya swala ya Ijumaa na Hijab, baadhi ya Wabunge Wakristo walisimama na kushambulia kuletwa kwa hoja hiyo.

Japo sura ya nje ilionyeshwa kuwa watu hao walikuwa wanamshambulia Waziri, lakini walikuwa wanaushambulia Uislamu na Waislamu.

Wenye japo chembe ya imani hawakuthubutu kukaa kimya kuona dini ya Allah inachezewa. Walihofia ghadhabu za Allah. Waliamua kufanya walichoweza; kwanza kusajili kwa Mola wao kwamba hawapo tayari kuridhia dini yake ichezewe. Pili kuonyesha hisia zao dhidi ya Wabunge wale Wakristo walioonyesha chuki zao dhidi ya Uislamu ndani ya Bunge.

Waislamu hawa walioamua kusimama imara kuihami dini yao hawakufikiria kabisa kwamba wale ambao hawakuguswa na damu ya Waislamu iliyomwagwa Mwembechai watahusika. Wala hawakutarajia safu yao ya uongozi kuwa na wale waliokaa meza moja na Mhe. Yusufu Makamba wakiwa "simanga" wafiwa na marehemu waliotwangwa risasi na polisi Mwembechai.

Wakati watu wakiomboleza tukio la mauaji ya Mwembechai huku wakisoma Khitma kwa ajili ya marehemu Ustadh Saleh na wenzake wapo waliokusanyika 'Ikulu' kuwaombea dua njema wale waliopongeza kazi ya polisi iliyoishia kuwaua Ustadh Saleh na kumtia kilema mtoto Chuki Athumani.

Hao hawakutarajiwa washiriki maandamano ya kupinga mwenendo hasi wa baadhi ya Wabunge Wakristo dhidi ya Uislamu. Wala haikufikiriwa kwamba wale waliochini ya uongozi wa wale waliodai kuwa kuchanwa "Yasini" (Buzuruga 1984) sio kuchanwa Qur'an, watashiriki japo kwa kukaa kimya wasipinge.

Lakini pia busara inakataa kuwa pangekuwa na uwezekano wa kushiriki wale waliochini ya Taasisi iliyopewa nguvu na michango ya Maaskofu mwaka 1994. Lisilokuwa limetarajiwa ni hili la kufikia hatua ya kuwaruhusu polisi waingie ndani ya nyumba tukufu ya Allah kuwaswaga wanawake ' wakasulubiwe'. Hili halikutarajiwa kwani hata kule Rwanda yalipotokea mauaji ya halaiki waliotafuta hifadhi Misikitini walisalimika. Ila wale waliokimbilia makanisani hawakupata salama kwani Maaskofu waliwapokea kisha wakatumia "vimobiteli" vyao kuwaita Interahamwe wakawaua. Na mpaka leo Maaskofu hao wanasakwa wafikishwe mahakamani.

Basi kama lipo la kushangaza na kustaajabisha ni hii "Sifa" mpya baadhi ya watu wanayotaka kujivika. Sifa ambayo ilikuwa ni miliki pekee ya Maaskofu wa Rwanda.
 
--
Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook